Delonising Education

Delonising Education

Saturday, 7 October 2017

Mlevi atamani Tunduni angekuwa mgeshi

Rais Magufuli pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo (kushoto) na Brigedia Jenerali Dkt. Paul Massawe Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba akielezea alivyoshambuliwa kwa risasi mkononi, tumboni na mguuni  wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam.
            Katika kutafakari namna kaya na wanene wake especially munene mwenyewe walivyoitikia baada ya Tunduni Liisu kumininiwa shaba na wakora wanaojifanya hawajulikani wakati wanajulikana, anatamani angekuwa mgeshi. Rejea namna munene alivyojihimu na kujilawa pale mgeshi mstaafu alivyopiga shaba. Huenda huyu Tunduni angelipata top priority kama ilivyotokea kwa mgeshi husika. hata hivyo, mlevi haelewi namna mgeshi anavyoweza kuwa muhimu kuliko muishiwa. Kama angekuwa ndata, ndata wenzake wangeliwanyaka wale waliomfanyia kitu mbaya. Na kama angekuwa munene, wote wangemwabudia na kumuogopa hata kama ni kinafiki na kwa woga.
            Tangu amiminiwe shaba Tunduni, sijasikia chama twawala kikifanya mandingo lau kutuma ujumbe rasmi kwenda Nairoberry kumujulia hali. Duh inatisha. Twapelekeshwa wapi ambapo sihasa inageuka uhasama wa kufanya mlevi. Sichokonoi wala kumchokoza yeyote, namna wanene walivyoshughulikia suala la kumiminiwa shaba Tunduni, licha ya kuwa aibu na so, inaonyesha kuna namna. Hivi kweli Tunduni angekuwa mhishimiwa wa twawala wangekaa kimya hivi? Wameshindwa hata kutoa tamko hata kwenye vyombo vya umbea! Nani hataonja mauti huyu nimsujudie?
Sasa nasema; kul nafsin zalikatu mauti yaani kila nafsi itaonja mauti. Kama wababe kama Farao aka Filauni na Nabukadnezza walionja mauti, nani atasalia zaidi ya kujilisha pepo tokana na ujuha na usahaulifu? Kama Nelson Mandela, Mzee Mchonga na wengine walipotea, nani huyu mjanja na shujaa atabakia? Shame on them all! Sijui walevi wanapelekeshwa na kupelekwa wapi iwapo wanaanza kuhukumiana na kujaliana au kutojaliana tokana na imani zao za kisiasa? Inatisha na kuhuzunisha; sina mfano.
            Sisemi kutokana na kanywaji au tujani bali ukweli mtupu au ulio uchi, naked truth. Tumefika na kufikishwa pabaya. Yaani mhishimiwa mzima anamiminiwa shaba na washenzi waliofanya hivi hawashikwi! Yethu! Laillah illa Allah! Ni sheitwan gani ametuingilia hivi kiasi cha kukosa mwelekeo huruma na utu! Japo najisemea, naamini wapo wengi wanaoshangaa kiasi cha kuhoji na kujisemea kama mimi hata kama si walevi wa kanywaji.
            Namuona Tunduni kama mdogo wangu, ndugu yangu, mbongo mwenzangu na binadamu mwenzangu anayepaswa kuhurumiwa sawa nami au yeyote yakimkuta kuhusisha hata hawa wauaji na washenzi waliotaka kumnyotoa roho bila sababu zaidi ya woga na upumbavu wao. Najitahidi kuvaa viatu vya Tunduni nimdeku mkewe na watoto na ndugu na mashabiki wake ukiachia mbali wenzake. Simdeku Tunduni sawa na nguruwe waliomuumiza. Namuona kama mwanaume, baba, mwana, raia, binadamu na asiye na hatia kama mimi na wewe na wao. Namuona Tunduni kama ninavyojiona na kukuona wewe.  Laiti wengi–hasa wale waliotaka afe–wangevaa viatu vyangu na vyake na kuondoa upumbavu wao, naamini unyama aliofanyiwa usingetokea.
            Hivi Tunduni angekuwa ndata, kweli nguruwe na wanaharamu waliomshambulia wangekuwa bado uraiani wakifaidi malipo ya jinai yao? Hata hivyo, sitakata tamaa. Kwani, malipo ni hapa hapa duniani. Laiti binadamu angejaliwa kujua yanayomgoja–sina shaka–wahalifu waliomfanyia kitu mbaya Tunduni wangelia na kusaga meno na kuchelea kutenda unyama waliotenda tokana na upumbavu na upofu na upogo wao. Hwa waliommimia shaba Tunduni wangekuwa wanaume kama si watoto si riziki, wasingetenda unyama waliotenda. Hata nguruwe–pamoja na uchafu na udogo wa ubongo wake–asingeweza kutenda upumbavu na unyama huu.
            Natamani Tunduni angekuwa mgeshi au ndata. Huenda wanene wangemuabudia na kumuogopa kiasi cha kujigonga kwake; na si kumtelekeza kama ilivyo. Inashangaza na kutisha. Kama walevi hawa wameshindwa kwenda Nairoberry hapa jirani kumjulia hali, angekuwa ugabacholini au utashani wangefanya nini? Huenda wangemtumia kwenda kufanya matanuzi kwa kisingizio cha kwenda kumjulia hali wakati wengi wanaomba anyotoke roho kana kwamba wao wataishi milele. Wako wapi akina nduli Amin, Gaddafi, Hitler na Mussolini? Wako wapi akina Osami bin Ladin na Mura Umar? Wako wapi akina Augustine Pinochet?  Wako wapi akina baby na papa Duvallier? Wako wapi akina Samuel Kanyon Doe? Nambie. Wako wapi akina Botha the Croc? Wako wapi akina Pol Pot wa Kampuchea na mahabithi wengine wengi waliofanya unyama usiomithalika? Binadamu ni nini zaidi ya kuwa manii na matope?
            Leo naongea kifalsafa ya kilevi kama mzee Mchonga na Mandela kama si Nkrumah na Lumumba. Wamanga husema: pen is mightier than a sword japo sisi tumebadili ukweli huu na kuuweka kinyume kiasi cha wageshi kuwa muhimu kuliko wahishimiwa.
            Nimalizie kwa kuhumiza usawa bila kujali tunayemjali ni mgeshi au mhishimiwa, msukuma mkokoteni au rubani au mtumwa na bwana na mtawaliwa na mfalme. Wote tulizaliwa uchi; na siku moja tutatoweka na kugeuka matope na kusahaulika. Tieni akilini;na kutenda haki mkijua kuwa ujivuni na ukatili havilipi; na malipo ni hapa hapa duniani. Pona haraka Tunduni Lissu. Aamina. Si utani. Hakika; natamani ungekuwa mgeshi au ndata kama si kuwa mwanachama wa chama twawala.
Chanzo: Nipashe J'mosi leo.

No comments: