The Chant of Savant

Wednesday 31 January 2018

Kijiwe kuendesha maombi Afrika nzima kwa ajili ya Tunduni Lissu

 Image result for tundu lissu photos
            Baada ya kuona waumini hata matapeli wakiendesha mikesha ya kuombea kaya, Kijiwe, kwa vile kina wanachama ambao ni waumini wa kweli–na si wasaka ngawira na wachumia tumbo–kimeamua kuendesha mkesha wa bara zima la Afrika kumuombea shujaa wa ukweli aliye tayari kuufia ukweli kama Plato, Tunduni mwana wa Lissu aliyeumizwa na majembuzi na wapinga maendeleo na uhuru wa kujieleza waliotaka kumnyotoa roho.
            Mgoshi Machungi baada ya kurejea kutoka kwa king’ang’anizi Bob Mugabe anakwanyua mic baada ya kuamkua. Anaronga “wagoshi nina ushongo na kijiwe na mic hasa ikizingatiwa kuwa timekaa miezi mitatu bia kukwanyua waa kubusu mic.” Anatugeukia na kutuangalia na kuendelea ‘au shiyo wagoshi? Mwenzenu nina uchungu sana. Hapa manaponiona nina mpango wa kwenda Uhoanzi kumjuia hai Tunduni mwana wa Issu aiyetaka kunyotoewa roho na wajaaana wasiojuikana ambao mpaka sasa wameendeea kutojuikana wakati wanajuikana.”
            Kabla ya uendelea, Mijjinga anampoka mic na kudema “kaka usinikumbushe shujaa huyu anayeendelea kusota kitandani. Hata hivyo, namshukuru Muumba kwani waliotaka kumnyotoa roho wameshindwa na kuadhirika.  Kama uchache utaruhusu, tutakwea pipa pamoja kwenda kumpa kampani shujaa huyu wa aina yake kaya nzima.”
            Mgoshi hangoji aendelee kufaidi mic.  Anampoka mic na kuendelea “bashi mwenzenu nina wazo kuwa tiitishe mkesha wa baa zima la Afiika ili timuombee apone haaka arejee kuja kuendeleeza mapambano au siyo?”
            Kapende ambaye alikuwa akimnong’oneza jambo da Sofia Lion Kanugaembe anaamua kula mic. Anazoza “kwa vile kwenye kaya yetu tunapendana na wote ni ndugu, hili si jambo baya. Hukuna mama makamu alivyokwenda kumpa tafu kule Nairoberry kwa wakora juzi juzi kabla ya kukwea pipa kuelekea Uholanzini? Huu ni mfano wa kuigwa.”
            Kabla ya kuendelea Mipawa anamnyang’anya mic na kudema “hili la bibi wa makamu kwenda kumdeku mie sioni kama ni dili iwapo baba mwenyewe na kipaza sauti wamekula pini ukiachia mbali kutohimiza waliotaka kumsokoine kushindwa kupatikana kwa kisingizio cha kutojulikana. Hivi kweli hawa wajalaana hawafahamiki? Au ni kuzinguana na sanaa ukiachia mbali kuwa na mkono wa mtu?”
            Msomi Mkata Tamaa anaamua kutia guu na mapema “kaka paha umeibua hoja na maswali mazito na muhimu. Haiwezekani kaya yenye ndata na ndutu na kila ghasia za usalama kushindwa kuwabaini na kuwashughulikia hawa wajalaana kama hamna namna. Kama kaya haiwezi kuwabaini na kuwachukulia hatua stahiki hawa wahalifu basi ni hatari kwa maisha ya wana kaya wote na hakuna haja ya kuwa na lisilikali ambalo kwa kizaramo huitwa sitting duck or do nothing powers that be.’
            Kabla ya kuendelea mzee Maneno anampoka mic na kuchonga “Msomi angalia hicho kikameruni. Hujui kuwa nasi tuna lugha ya kaya ambayo mnene ameamua kuipigia chapuo kiasi cha kuanza kujulikana na kuheshimika? Hivyo, kaka zoza Kiswahili au siyo Msomi?”
            Msomi anatabasamu na kuendelea “kaka usemayo ni kweli tupu. Hata hivyo, nisamehe. Kwani nilipitiwa. Hata hivyo, si vibaya kujikumbusha madude na lugha niliyokuwa natumia wakati nikisomea PhD zangu nyingi. Hayo tuyaache. Naunga mkono wazo la kumuombea Tunduni ila nina sharti. Sitataka tuwahusishe wachunaji wanaojiita wachungaji na mashehena wasije kutia laana dua yetu. Nitapendekeza tuombe sisi wenyewe na walevi wote barani tena kwa kutumia Mulungu na si miungu ya kigeni na ya kikoloni.”
            Mpemba hangoji amalize “yakhe mie sikuelewi ati.  Uniposema Mulungu wamaanishani? Wadhani wote matwahuti wasio na dini wanaowezaomba kwa miungu ya kishenzi siyo?” Kanji anaamua kula mic “mimi ungakono na guu Somi. Vote iko na dini yetu ya asili dugu yangu. Kama veve zarau dini yako basi vote nacheka veve. Sisi takwenda omba Brahma asaidie hii Tundu ipone haraka sana.”
            Msomi anakatua mic tena ‘leo Kanji umenifurahisha sana. Afadhali umesema wewe. Maana, waswahili wakati mwingine ni viumbe wa ajabu. Wanadharau na kudhalilisha mila zao huku wakipwakia za wengine hadi kufikia hata kutoana roho kama ilivyo kwa Tunduni ambaye ameumizwa kwa kutetea wana kaya dhidi ya mambo ya ajabu ajabu.  Unaweza kuzunguka jiji zima. Hutakuta nyumba ya ibada ya Kiswahili bali za kiarabu, kizungu, kihindi, na juzi juzi nilisikia za shetani kule Idodomya ambapo chizi mmoja alitaka kuanzisha. Tunajidanganya na kudanganywa bila kujua kuwa huwezi kuheshimika kama hujiheshimu na kuheshimu chako. Hili ni somo la siku nyingine hasa nikizingatia kuwa ni pana hasa kutokana na kutamalaki kwa matapeliw anaodai watenda miujiza wakati ni wezi watupu. Hawa–mnasisitiza–washirikishwe kwenye kumuombea Tunduni. Watamwombea nini wakati wana madhambi zaidi ya shetani mwenyewe? Wataomba kwa Mulungu gani wakati miungu yao ni fedha na utajiri?”
            Sofi aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kula mic “mwenzenu nikimkumbaka Tunduni huwa machozi yananitoka. Sijui tunaelekea au kupelekwa wapi ambapo udugu tuliorithi umegeuka uhasama wa kutoana roho? Tulizoea kupingana kwa hoja siyo ngumi na risasi wala kesi za kubambikiziwa”

            Kijiwe kikiwa kinanoga si mvua ikaanza kunyesha! Acha tutimke mbio utadhani mvua inaua! Waswahili kwa kuogopa mvua lakini wasiogope miwaya, sina hamu!
Chanzo: Tanzania Daima leo, Jan., 31, 2018.

No comments: