The Chant of Savant

Wednesday 24 January 2018

Mpayukaji arejea toka Ukanadani kuulizia bomba letu la bomba dear


            Baada ya Kijiwe kungojea bomba letu la bomba dear toka Ukanadani bila majibu, kiliamua kunituma mimi kama Mkiti wake kwenda kudodosa kujua kunani lau kiweze kusaidia kaya kulipata. Ndiyo maana kwa miezi minne hivi, hapakuwa na kitu ugani. Nilikwenda kutafuta nondo. Nilianzia pale alipolianzishia totoTudu Lissu kuwa bomba letu jipya la Bomba Dear lilikuwa limenyakwa kule Ukanada, wanoko walimuita mmbea wengine msaliti na mambo mengine tu ya hovyo na matokeo yake akaishia kumimiminiwa shaba kibao. Hao wameshindwa na watanyong’onyea kabla ya kupukutika mmoja mmoja.
             Sasa siku zinazidi kuyoyoma wala bomba letu kipenzi hatulioni. Je kunani; mbona mabingwa wa kuzoza na kuzodoa hawasikiki? Zifuatazo ni adidu za rejea nilizofanyia kazi. Je ni kweli kuwa kuna washenzi na matapeli wa kimataifa walioingia kayani wakijifanya wanatafuta kazi kumbe kupiga njuluku zetu waliotufanyia kitu mbaya? Kama ni kweli, inakuwaje wale wanene walioendekeza upigaji huu tunaendelea kuwapa shavu badala ya kuwazomea hata kuwaonyesha lupango? Tunawaengaenga kwa lipi wakati walituingiza kwenye matatizo tokana na upogo na ubinafsi wao? Hamkusikia munene akisema wakati wa kuzindua taarifa kuhusu mawe akilalalimika kuwa kaya ilikuwa imegeuzwa shamba la bibi kwa wapigaji kuja kujipigia kama vile haina mwenyewe? Kaya ilikuwa ikiliwa mbele na nyuma tokana na kuongozwa na machangu kimaadili . Unapowapa unene vilaza, hata hivyo, unategemea nini?
            Kwa vile majibu hayatoki; na inavyoonekana, hakuna mwenye ubavu wa kuyatoa, kijiwe kiliamua kunilipia visa, nauli na malazi kwenda zangu Ukanadani kujua kunani? Hii ni kutokana na uzalendo–na si usaliti–wa kijiwe. Hivyo, msishangae kusoma mikakati hii hasa ikizingatiwa kuwa siku zilizopita niliipa kaya mbinu ya kuepuka wapigaji wa kimataifa wanaotumia mahakama zao za kijambazi kukwamisha maendeleo ya kaya kapuku hasa baada ya munene kusema kuwa hatakuwa tayari kujidhalilisha kama waliomtangulia kukesha kiguu na njia akienda ughaibuni kubomu kana kwamba yeye ni taahira. Haiwezekani kaya inayokalia utajiri wa kutisha iendelee kubomubomu kama vile haina raslimali. Huwezi kuongoza kaya vizuri wakati unapoteza muda kuzurura na kutanua bila sababu. Kama ingekuwa amri yangu, wajalaana kama hawa ningewatia kitanzi lau liwe somo kwa wengine wanaodhani kaya hii ni shamba la chizi.
            Najua kaya yetu ilikosa raslimali moja kubwa inayoitwa kwa kisambaa smart upstairs baada ya kung’atuka mzee Mchonga. Ni pale ilipopata wavivu wa kufikiri, malimbukeni na wazuraraji kama viranja wake wakaishia kujisifia kuzurura na kubomu ukiachia mbali kuiingiza kaya kwenye mikataba ya kipumbavu na kijambazi inayoihangaisha kaya. Kama si upuuzi wao, bomba letu kipenzi wala lisingekuwa gumzo hadi tunaitana majina mabaya ukiachia mbali kuonana wabaya bila sababu zaidi ya upumbavu wa wajalaana hawa.
            Kwa vile Mpayukaji si mgeni Ukandani, nilikwenda kukutana na washikaji zangu wa zamani ambao ima niliwafundisha au kusoma nao ili tuone namna ya kuinasua kaya na mkwamo huu.  Niliwahi kutoa msaada na ushauri wa bure kuwa kaya inapotaka kufanya mambo kama haya, inapaswa iwe inatuhusisha sisi wataalamu wa mambo ili kuepusha hasara inayoweza kutokana na vitu kama hivi. Kitu kingine nilichokwenda kufanya Ukanadani ni kuona kama kuna namna kaya yetu inaweza kujitoa kwenye mahakama za kishenzi za kinyonyaji kama hizi ambazo zimekuwa zikionea kaya za Kiswahili kwa sababu zilianzishwa na wakoloni waliotuibia bila kuwafikisha kwa pilato wakalipia madhambi na uhalifu wao vizuri.
            Kabla ya kuanza msafara huu mrefu kwenye kaya hii ya Ukanada inayosifika kwa baridi, ukarimu na ukwasi wake, naomba wahusika wasiogope aibu kutokana na nyodo walizoonyesha pale totoTundu aliposema Bomba Dear au Dear Bomba yetu ilikuwa imenyakwa tokana na kudaiwa na waduwanzi na washenzi fulani matapeli wanaotaka kutuingiza mkenge.  Baada ya kutia timu niligundua kuwa kweli bomba letu dear limenaswa. Maana, unaposhughulikia tatizo kama hili lenye amri ya mahakama nyuma yake, lazima uwe umejiandaa na zana zako zote. Huwezi ukavamia inshu kama hii kwa pupa ukafanikiwa. Sana sana utalizwa kama inavyooanza kuonekana kwenye mazungumzo yasiyo makini ya kimakinikia. Ndiyo maana, nashauri, siku zijazo, wanene wetu wajitahidi kufanya mambo kwa kuyapima kabla ya kuingizwa mkenge tokana na maamuzi na madili mengine ya kilevi levi ambayo kaya yetu ilizoea kuingizwa ikiwa chini ya walevi wa madaraka na washamba wa mambo kiasi cha kupoteza muda mwingi kwenye uzururaji bila sababu za msingi. Nampongeza sana dingi kwa kukataa ujinga na ulimbukeni huu wa kujilisha pepo wakati walevi wakinyotolewa roho na ukapa na ukata.
            Kwa vile ninapaswa kufanya maandalizi ili kuepuka aibu ya kuingizwa mkenge kama hawa wanaotaka kuingizwa mkenge, nilifanya utafiti wangu kisomi na kuona ukweli ambao siku zijazo nitatoa namna ya kuufanyia kazi na kufanikiwa. Juzi nilipitia zangu Brusels kum-breaf kumjulia hali na kumwombea dua totoTundu na kumpongeza kwa kuweka mambo hadharani hata kama aliumizwa vibaya sana.

Kwa ufupi ni kwamba bomba dear letu limenasa na sijui namna ya kulinasua.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano Jan., 24, 2018.

No comments: