The Chant of Savant

Wednesday 24 January 2018

Msamaha wa rais usigeuzwe dili kusaka umaarufu

Image result for photos of babu seya
            Mwishoni mwa mwaka jana, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, kwa mamlala aliyo nayo kisheria, alifanya kilichowastua wengi kwa kutoa msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha kumbukukumbu ya uhuru wa Tanganyika. Katika msamaha huu wa rais, ulihusisha hata wale waliokuwa hawatarajii acha kutarajiwa kuachiwa kama vile wale waliokuwa wamepatikana na hatia ya kubaka, ambayo kisheria, hawakupaswa kusamehewe. Hili lilizua malalamiko toka kwa watetezi wa haki za binadamu hasa baada ya wasamehewa kuonekana wakijivinjari kwenye viwanja vya ikulu. Wanaopinga hili walisema kuwa linawapa ujasiri waliotenda makosa ya ubakaji.  
Hata hivyo, si lengo la makala hii kujadili uhalali au mamlaka ya kufanya hivyo. Niseme wazi kuwa rais alitumia mamlaka yake kuwaachia alioona wanafaa kuachiwa baada ya kujiridhisha, kupitia vyombo vyake kuwa havunji sheria, hasa katiba aliyoapa kuilinda, kuhifadhi na kuitetea kama mkuu wa nchi.   Pia, si nia ya safu hii kuhoji kama rais alizingatia maslahi mapana ya wahanga wa baadhi ya jinai ambazo zikitendeka na mtuhumiwa akakutwa na hatia hapaswi, kisheria, kupewa msamaha kama ubakaji. Kwanini nagusia hili? Ni kuepusha kuonekana kama rais amefanya makosa kutokana kufanya ambacho kisheria hakiruhusiwa wala kukubalika hasa tukizingatia sheria kama sheria na heshima na haki za waathirika wa baadhi ya makosa. Wapo ambao wameishaanza kutumia kuachiwa kama mtaji wakizunguka huku na huku wakivutia vyombo vya habari kuwahoji. Wapo wanaodai kuwa wanafanya waliyofanya kama ishara ya kumuunga mkono na kumshukuru rais. Rais keshawaachia inatosha. Hana haja ya kuendelea kusikia mambo yenu. Heri mkae kimya na kumshukuru Mungu na rais kimya kimya badala ya kutafuta usupastaa unaoweza kuwaponza baadaye.
            Makala ya leo inajikita kwenye kadhia mbili, yaani wasamehewa kutaka kutumia fursa hii ama kutafuta umaarufu wakisahau kuwa msamaha hauondoi kosa la jinai walilopatikana nalo na ile ya wasamehewa kurudia kutenda makosa ya jinai kiasi cha kuonyesha kuwa msamaha wa rais ni kama dhihaka au una makosa kwa kuachia watu ambao hawakupaswa. Hivyo, ushauri wa kwanza, ni hawa wahusika kujua kuwa kusamehewa na rais, siyo fursa ya kutafutia umaarufu au kurejea kwenye maisha ya jinai bali kujrekebisha na kuomba Mungu wasiburuzwe tena mahakamani.  Pia wahusika wajue kuwa msamaha wa rais ni jambo ambalo ni sawa na bahati nasibu. Katika nchi inayofuata sheria vilivyo na kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa misamaha kwa wahusika, kusamehewa na rais tena kwa makosa yasiyosameheka, saa nyingine ni jambo ambalo linaweza kuitwa muujiza hasa ikizingatiwa kuwa kufanya hivyo, kunaweza kuleta madhara kwa mamlaka au kuifanya iangalie upya uamuzi wake na kuziba mwanya wa makosa kama yalitokea ima katika kuchunguza tabia za wahusika na mazingira ya kuhukumiwa au sheria.
            Hakuna kilichoshangaza safu hii kama kuona baadhi ya wahusika ambao si raia wa Tanzania, kuonyesha kaubabe fulani ambapo kwa nchi za wenzetu siku walipoachiwa wangefukuzwa nchini. Ni ajabu kuwa Tanzania haikufanya hivyo kwa sababu ambazo mamlaka inajua yenyewe. Kitu kingine kilichonisukumba kudurusu wazo hili ni ile hali ya wasamehewa kutokana kosa walilofungwa nalo. Tumeona wengine wakisema hadi kutoa machozi kuwa ima walionewa au kubambikizwa kesi tofauti na hawa wanaosaka umaarufu kwa sababu tu wameachiwa na rais.
            Wahusika wanapaswa kujua kuwa rais aliwasamehe si kwa mamlaka tu bali tokana na huruma yake. Hata kitendo cha baadhi kukaribishwa ikulu kilizua utata hasa kwa waathirika wa kadhia waliyoshitakiwa nayo wasamehewa na kupatikana na hatia na kufungwa maisha. Sijui wazazi wa watoto na watoto waliofanyiwa vitendo hivyo, huko waliko, wanajisikiaje? Je hawa wasamehewa wangetaka nini kifanyike kama vitendo walivyokutwa navyo hatia vingetendwa kwa wapendwa wao, watoto, dada, shangazi au ndugu zao? Japo naweza kuonyesha kama nawabagua wahusika, kwa vitendo walivyopatikana navyo hatia na kufungwa, wajue kuwa Tanzania ni taifa lenye huruma. Maana kwenye nchi nyingine ikiwamo yao, ukishafungwa imetoka.  Kusema ukweli, kuna kipindi Tanzania tunakuwa wakarimu sana kiasi cha kutia shaka kama kweli tunajua thamani ya utaifa wetu.
            Mbali na wanaosaka umaarufu na kushindwa kuomba msamaha au kuonyesha kuwa wamejutia makosa yao, wapo wanaotumia fursa ya kusamahewa kama kuitukana mamlaka iliyowapa upendeleo huu. Kwani, tayari wengi wameisharejeshwa kule wakiwa wametenda makosa ya jinai kuiachia mbali baadhi kuwa mikononi mwa vyombo vya dola wakisubilia kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria baada ya kupatiakana na ima silaha au kujihusisha kwa njia moja au nyingine na jinai.

            Tumalizie kwa kuwataka wasamehewa kuwa na fadhila. Watende mambo mema. Wale walioachiwa kama nilivyioanza kwa makosa yasiyosameheka, wasijione ni wajanja au wasitumie msamaha wa rais kutafutia umaarufu na kuonyesha ubabe. Kwani, wale waliowakosea, licha ya kuwa watu, wana makovu ya mateso yao. Kwa wale ambao si raia wa Tanzania, wazidi kumshukuru Mungu.  Kwani ingekuwa nchi nyingine, jambo kama hili lisingefanyika tena bila serikali za kwao kuiomba serikali lau kufikiria kuchukua uamuzi kama huu wa ajabu. Pia, tumshukuru rais kwa kuwa na huruma muhimu afuate sheria na taratibu ili kuondoa malalamiko.
Chanzo: Tanzania Daima, Jan., 24, 2018.

No comments: