The Chant of Savant

Wednesday 3 November 2021

Misiba ya Msiba, Somo kwa Wachumia Tumbo

Hakuna ubishi. Kipindi cha awamu ya tano, kuna mambo mengi mazuri na ya maana yalifanyika. Sambamba na hayo, pia kulikuwa na mambo mengine ya aibu, mabaya na ya hovyo yaliyotokea. Hii ndiyo sifa ya binadamu kuwa na mambo yote mabaya na mazuri yenye heshima na hata ya aibu. Leo tutaongelea somo linaloweza kutokana na namna baadhi ya wenzetu wanaopata fursa ya kuwa karibu na watawala wanavyoweza kutumia vibaya ukaribu huu kwa ima kuwaumiza au kuwahujumu wenzao hata kuwaibia. 
Leo tutagusia kisa au tuseme tamithiliya ya Msiba (siyo jina lake halisi), ‘mwanaharakati huru’ kama alivyopenda kujikweza na kujinasibu–––ambaye, hata hivyo, hakuwa huru–––– ambaye hivi karibuni alianza kupoteza umaarufu na uhuru wake. Wakati wa utawala uliopita Msiba alitikisa kweli kweli hasa kwenye mitandao akimshambulia, kumuumbua hata kumzushia kila aliyemtaka asijue kuna mwisho wa kila jambo chini ya jua. Msiba alitengeneza misiba sawa na genge la wahalifu lililojulikana kama ‘watu wasiojulikana.’ Kwa wanaokumbuka, hakukupita siku bila Msiba kupata mtu wa kupelekea msiba au misiba. Msiba aliumba na kuumbua maadui huku akitaka aonekane mzalendo namba moja kuliko hata Rais. Ama kweli ivumayo haidumu.
 Hivi karibuni mkono wa kutoa haki ulimtembelea bwana Msiba kwa kumkuta na hatia nyingi mojawapo ikiwa ni kuwadhalilisha watu jambo ambalo limeilazimisha mkono wa haki kumuamru alipe mabilioni ya shilingi ambayo bila shaka hana wala hatayapata maishani mwake. Kimsingi, Msiba––––kama alivyoibuka–––amezama. Amegeuka kituko baada ya wale aliotaka kuwageuza vituko kukataa kuwa vituko na badala yake wakamfanya yeye kituko. Msiba amegeuka msiba wake mwenyewe. Baada ya kibao kubadilika, wahanga wake waliamua kumshitaki au kumsulubu kama alivyowasulubu. Bila kukoma, walimshinda karibu katika kesi zote. Hadi sasa hatujui ni kesi nyingine ngapi zitafunguliwa. Sina haja ya kutaja orodha nzima ya watu aliowakwaza na kuwaumiza ambao mahakama imewapa haki yao.
Kwa namna Msiba alivyojitengezea umaarufu asijue ndiyo alikuwa akiita misiba yake, wapo waliomuona kama mwanaharakati huru kweli na wale waliomuona kama mtu wa kujipendekeza ambaye, hata hivyo, alitesa na kuwatesa wengi bila sababu za msingi zaidi ya njaa na tamaa zake. Wapo waliomuona mzalendo wa kweli; na wapo waliomuona kama mchumia tumbo na kibaraka wa kawaida aliyeendeshwa na tamaa na upogo ili kujipatika mlo wake wa kila siku ukiachia mbali ushufaa. Msiba, alichafua jina la vyombo vya habari licha ya kuwaumiza wenzie. Kwa waliomjua kama mwana tasnia, walidhani hii ndiyo tabia ya waandishi wa habari wakati siyo. Waliomtambua kwa kabila lake, wapo waliodhani kuwa hii ndiyo tabia ya watu wa kabila lake mambo ambayo si kweli. Kila jamii na tasnia ina watu wema na wabaya.
 Kwa upofu na upogo, Msiba aliamini hakuna mwisho wa utukufu na utukutu. Nadhani hata waliomtumia hawakujua hili na kama walilijua walilidharau. Msiba alidharau na kusahau misemo miwili maarufu. Aliyepo juu mngoje chini na hakuna marefu yasiyo na ncha; ukiachia mbali ule usemao binadamu hupanga na Mungu hupangua. Msiba alijikweza na kukwea kila kiriri asijue kuna bonde kila baada ya mlima. Ama kweli wahenga walisema. Kiburi ni silaha ya mpumbavu. Kuna haja gani kujilisha pepo na kumtegemea mwanadamu badala ya Mungu aliyemuumba? Nani alijua Msiba, pamoja na wengine kama yeye waliotesa, wangeteseka tena ghafla bin vuu kama watoto wa zamani wa mjini walivyozoea kusema? Tuliwaona wengi waliotesa na kutisha na hatimaye wakatoweka. Kwa kumbukumbu ya jana, nani amesahau watesaji kama Salva Rweyependekeza aliyesifika kwa kujipendekeza wakati wa awamu ya nne au Dan son of Jonah wakati wa awamu ya tatu? Nani amesahau jamaa mmoja ambaye Hayati Christopher Mtikila alipenda kumuita gabacholi mmoja aliyewahi kumuita first lady shemeji wakati wa awamu ya pili?
Saa tujifunze kwa kujiuliza. Je Msiba anayo haya mabilioni anayodaiwa? Je atayapata wapi? Je ataweza kulipa au kuendelea kuishi na kongwa ya kuumbuka? Je kama Msiba hataweza kulipa–––jambo ambalo liko wazi–––haki ya walalamikaji itatolewa na nani? Ama kweli, aliyeko juu–––huna haja ya kumpandia–––mngoje chini. Muhimu–––kama unahisi umedhulumiwa au kuonewa, muombe Mungu–––atafanya kile ambacho hutegemei wala kuwazia. Nani alijua kuwa kuna siku ingepita bila Msiba kuja na kashfa, tambo na uongo wake bila hata kupepesa wala kuona aibu. Hata hivyo, Msiba ana bahati. Alikashfu kila mtu asijue mwisho wa siku zitamrudia tena kwa hatari na mapigo zaidi ya wahanga na walengwa wake. Yote haya yamesababishwa na uchumia tumbo ambalo mara nyingi hufanya mwenye kuwa nao asitumie kichwa wala ubongo kufikiri zaidi ya tumbo na utumbo. Hutumia njaa kutatua kila tatizo bila kujua kuwa mwisho wa njaa mara nyingi ni baa kama siyo kujikuta kwenye jaa. Ingekuwa katika baadhi nchi majira zetu, angekimbia nchi siku ulipotangazwa msiba wa mkuu wa serikali iliyomfumbia macho. 
Tumalize kwa kuwaonya wengi kuwa kuna haja ya kuwa na hofu ya Mungu, kuwajali wengine, kuepuka kujilisha pepo hata kama una madaraka au uko karibu na wenye madaraka. Duniani hakuna jipya. Tulishawaone wengi wakikwea milima mirefu ya heshima na utukufu na ushufaa na kuishia kwenye mabonde ya aibu. Kwa wanaowakumbuka akina Isaka Malyamungu kibaraka wa Idi Amin imla wa Uganda, wanaweza kutwambia namna utukufu wa kibinadamu usivyo mali kitu. Somo kuu ni kwa wenye madaraka kuwa makini na watu wanaowazunguka au wanaokuja wakijifanya wanawapenda au kuwaheshimu wakati ni waharibifu wa kawaida au wachumia tumbo na wasaka ngawira.
Chanzo: Raia Mwema leo 

No comments: