The Chant of Savant

Saturday 27 November 2021

Muungano wa Afrika na Ubinafsi wa Watawala

Taarifa kuwa baraza la Mawaziri la Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) inayoleta pamoja nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda limeridhia uanachama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni habari njema si kwa DRC bali hata kwa wenyeji wake na eneo la Maziwa Makuu kwa ujumla hasa ikizingatiwa kuwa DRC si nchi ndogo wala maskini kulhali. Kwa kujiunga na EAC, DRC inapunguza uwezekano wa kuvamiwa na vinchi na vikundi vya kihalifu vilivyokuwa vimezoea kuivamia na kuiibia raslimali zake za thamani na lukuki ilizojaliwa. Pili, DRC inapata wenzake wanaoweza kuisadia hata kwenye vita inayoendelea kwa sasa kama nchi husika zitaacha ubinafsi na upogo na zikawa kitu kimoja kweli. Kwani, hali tete nchini DRC inasababisha ukosefu wa usalama si kwa nchi hizo tu bali hata eneo zima la Maziwa Makuu (GLR).
         Baada ya kujiunga kwa DRC–––kama wakuu wa jumuia hii wangekuwa wanaona mbali na si wabinafsi–––wangeungana haraka na kutengeneza ji nchi moja kubwa na lenye nguvu kisiasa na kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa DRC ina ardhi kubwa na raslimali zinazoweza kuifanya nchi hii iwe nae neo kubwa kuliko nchi yoyote ya Afrika bila kuzungumzia vyanzo vikubwa vya raslimali za thamani. Mbali na DRC, Tanzania nayo ina ardhi na raslimali nyingi ambavyo  vikiongezewa na ujio wa DRC vinaweza kufidia kwa nchi nne yaani Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda ambazo hazina ardhi wala raslimali zaidi ya watu wake ambao nao mchango wao si haba.
        Akiwa nchini Afrika Kusini Rais Uhuru Kenyatta aligusia suala mipaka akisema wazi kuwa iliwekwa ili kutunyonya na kuwahudumia wakoloni lakini siyo kutuhudumia wala kutuendeleza kama wakazi wa nchi zetu. Hili ni jambo zuri. Ila viongozi wengi wanaongelea kuondoa mipaka na kuungana mbele za watu lakini nyuma ya pazia wanakwamisha juhudi za kuunganisha nchi zao kwa kuhofia kupoteza madaraka na ulaji wake. Huu ni ukweli mchungu na unaoudhi ambao wengi hawataki kusikia. Kwanini Kenyatta hajawaambia wenzake wa Afrika Mashariki ambao tayari wana Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kama wao si kikwazo kikubwa kinachozuia muungano wa EAC na Afrika kwa ujumla? Kenyatta aliongelea kugawanywa kwa wamasai na waluhuya kati ya Tanzania na Kenya na Kenya na Uganda mtawalia. Alitolea mfano wa ndugu wawili wa baba na mama mmoja, Moody Awori aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya na mdogo wake Aggrey Awori ambaye alikuwa alikuwa Waziri kwenye serikali ya Uganda akiwa mganda  tokana na kurithi shamba lililokuwa Uganda baada ya kugawanywa kabila lao kati ya nchi mbili zilizoundwa na wakoloni. Mifano tunayo mingi. Hata hizi nchi tulizoundiwa na kujivunia kwa sasa si chochote wala lolote bali kongwa za kikoloni. shingoni mwetu kama mataifa na jamii.  Wakati wa kuunganisha Afrika ni sasa. 
        Mwaka 2015 nilitoa kitabu kiitwacho Africa Reunite or Perish nikiongelea umuhimu wa kurejesha muungano wa Afrika na faida zake. Niligusia mambo kama vile umaskini ambao unaweza kuondolewa na muungano wa Afrika pale itakapokuwa imeondokana mambo yanayoifanya iwe maskini kama vile utitiri wa marais, majeshi, benki kuu, visa, kutokuwa na uhuru kwa waafrika kwenda watakapo wakati watakapo kwenye bara lao na mengine mengi kama vile. nchi nyingi kufanya biashara na mataifa ya mbali huku yakikwepa majirani zake wa kubambikiwa wakati wao ni kitu kimoja. Mfano mdogo ni pale unapokuta nchi haina dawa za malaria wakati haikosi mabomu ya machozi.Mfano mkubwa niliotoa ni kuangalia matumizi ya majeshi yetu kwa kila nchi ikilinganishwa na huduma za jamii.
        Ukisikiliza maneno matamu na mazuri ya Kenyatta, yanatia moyo. Hata baba wa taifa, Hayati Mwl Julius Nyerere alizoea kuongelea na kupigania muungano wa Afrika. Lakini hakuna kilichofanyika tokana na marais kunogewa na urais na kulitekeleza bara letu kiasi cha kuonekana wakoloni zaidi ya wale wa kizungu. Kadhalika, Baba wa taifa la Ghana, Hayati Kwame Nkrumah alitaka Afrika iunganishwe mara moja kama ilivyogawanywa. Lakini Nyerere alitaka iunganishe taratibu kiasi cha kushindikana. Tujiulize; kama siyo ubinafsi na uchu wa urais, nini kimewazuia kuuganisha Afrika kama siyo kuendekeza ubinafsi na ukoloni wakati wakijua fika kuwa hivi vichi tulivyo navyo vimegwa na wakoloni ili kutudhoofisha, kututawala, na kutunyonya waafrika? Hata hivyo, baada ya kupata uhuru wa bendera, wakubwa wetu walishindwa kuviunganisha tena kwa kuogopa kupoteza urais wao.
        Tumalize kwa kuuliza maswali yafuatayo hata kama yanaudhi:
    Je tutaendelea hivi hadi lini wakati tunajua chanzo cha udhalili na umaskini wetu kuwa ni kuendelea na mipaka ya bandia ya kinyonyaji na kikoloni iliyowekwa na wakoloni?
    Je kuungana kunahitaji wafadhili toka Ulaya kiasi cha kuendelea kusuasua wakati tatizo siyo nia ya wananchi bali uchu wa urais wa watawala wetu japo si wote? Je wananchi wetu wanasemaje ikizingatiwa kuwa ndiyo wahanga wakubwa wa ukoloni huu wa kujitakia?
        Mwisho, kwanini tusianze sasa kama Jumuia ya Afrika Mashariki tukatoa mfano kwa wengine ambao wanaweza kuvutiwa na mafanikio yetu? Badala ya kuendelea kuwadanganya na kuwahadaa watu wetu na dunia kuwa tuna nia ya kuunganisha Afrika kama kitendo cha kujivua ukoloni wa kujitakia, watawala wetu wafikie mahali waamue kuwa wakweli. Waseme wazi wanavyopenda, kunufaika na kuridhika na mgawanyiko wa Afrika kwa vile unawapa madaraka binafsi au waachane na tamaa binafsi tuunganishe nchi zetu haraka sana kwa faida kubwa ya wote. Wananchi wako tayari.  Hivi kweli ukiwauliza wamasai wa Namanga, wajaluo na wakurya wa Musoma au wahangaza wa Ngara kuunganisha nchi zetu, kweli watakuwa na sababu yoyote ya msingi kupinga wakati mipaka imegeuka kama kongwa kwenye shingo zetu? Kuna haja ya kuacha uvivu wa kufikiri––––nikikopa maneno ya Hayati Benjamin Mkapa––––na kuanza kuunganisha nchi zetu haraka k ama zilivyogawanywa mwaka 1884 kwenye mkutano wa kijambazi wa Berlin. EAC lazima iwe mwanzilishi wa muungano wa Afrika.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: