The Chant of Savant

Saturday 6 November 2021

Waraka kwa Wale Wasakao Busara na Watawala

Hekima inasema kuwa unaweza kunipiga na kunifanya nilie lakini huwezi kunizuia kulia kwa sababu kulia na kulalamika ni haki yangu. Unaweza kunichukia lakini huwezi kunilazimisha kukupenda wala siwezi kukulazimisha kunipenda japo unaweza kufanya nikupende au nikuchukie kulingana na unavyonitendea. Kunipenda na kunichukia ni haki yako kama ilivyo haki yangu na yeyote kukupenda, kukuponda au kukuchukia japo chuki hailipi wala kujenga zaidi ya kuharibu na kusababisha mafarakano hata maangamizi. Kuna chuki ya msingi. Kuuchukia ubaya na ujinga hata jinai ni chuki safi inayozidi upendo au mapenzi ya maafa na ubadhilifu na uhalifu. 
        Unaweza kuniumiza lakini huwezi kunizuia kuugulia au kuhuzunika hata kulalamika. Kwani, ni haki yangu. Unaweza kuniua lakini huwezi kunizuia kufa wala kunifufua. Unaweza kunidharau lakini huwezi kunilazimisha kukuheshimu. Unaweza kunidhulumu lakini huwezi kunilazimisha kufurahia dhuluma yako wala huwezi kuepuka madhara na matokeo ya dhuluma. Unaweza kunfunga lakini huwezi kufunga akili wala mawazo yangu.kwani, hakuna jela linaloweza kuyazuia kuwa huru na hivyo kutoroka tena bila kuvunja milango wala kuwahagaisha walinzi. Unaweza kunitesa lakini huwezi kutesa sifa wala tunu zangu. Unaweza kunilazimisha ila huwezi kunifanya kuhiari.
Unaweza kunichafua ila huwezi kunisafisha. Kwani madhara yanakuwa yameishafanyika. Nani awezaye kuvunja kikombe au yai akaweza kuviunga? Unaweza kunipuuzia ila huwezi kunifanya nikujali. Unaweza kunidanganya ila huwezi kuua ukweli. Unaweza kunipaka matope ila huwezi kuzuia wengine kukufanyia hivyo. Wewe adui yangu unaweza kunipata matope lakini marafiki zangu wakanipaka manukato. Unaweza kuniona mie si chochote wala lolote lakini kwa watu wangu mie ni kila kitu. Kwako mimi ni tope hata jiwe lakini kwa watu wangu mie ni maziwa hata dhahabu kama siyo almas. Unaweza kunitakia mabaya hata mema ila huwezi kuyaamuru au kufanikisha utakalo. Unaweza kufanya wema ukalipwa ubaya na ukafanya ubaya ukakurudia usizuie. Hakuna aliyetenda ubaya akalipwa wema japo watenda mema mara nyingi hulipwa na Mungu baada ya wale waliowatendea mema kuwalipa ubaya. Hapa ndipo dhuluma huanzia japo haiishi hapo.
        Waja jifunzeni kuwa na busara na maarifa kwani ndiyo madaraja pekee yaiunganishayo leo na kesho ukiachia mbali kuwa kiungo cha jana. Je asiyejua jana yake aweza kuijua kesho yake? Je leo si kesho ya jana na jana leo ya juzi? Tafuteni ujuzi na kuutumia kwa utu na haki ili msigeuke waganga njaa na fisi waliojificha kwenye ngozi ya kondoo wakiwaumiza wengi. Je hatunao wengi wanaojiita watenda miujiza na wenye kuweza kutatua matatizo yetu wakati wao ndilo tatizo letu kubwa. Pia muwapo na elimu ya kufaa, elimu halisi, muwe wanyenyekevu kama njiwa lakini si kama kondoo. Muwe wasuluhishi na washauri wa kuleta ufanisi wa jamii na si wenu binafsi. Ni rahisi kusoma lakini ni vigumu kuelimika hasa mwenye kufanya hivyo kama atatanguliza umimi mimi badala ya jamii.
Nani aweza kuwa salama nje na si ndani ya jamii?                                 Hamkuambwa kuwa mtu pweke ni uvundo hata awe mfalme tajiri na msomi? Mtu ni watu na utu wa mtu si vitu alivyo navyo bali kuwa mwenye utu na uungwana mbele ya wenzake. Huwezi kuwa mtu wakati utu wako umejengwa kwenye vitu kama utajiri elimu na madaraka. Mtu wa hivyo si mtu kitu bali mlafi na zandiki asiyejua afanyalo. Maana ili kukamilisha utu wake wa vitu lazima atawauza watu asijue naye ni mtu.
        Kuna haja ya kujikomboa hata kama ni gharama. Kiazi hakishiki jembe lakini huipasua ardhi. Maji hayana nyundo lakini huupasua mwamba. Je utelezi haumuangushi tembo? Ni busara ya haya? Hakika kila penye udhalili ipo nguvu na hakuna nguvu isiyo na udhaifu.
        Hakika malimwengu ni darasa kubwa na pana kwa wenye akili. Katika masomo yote busara ni tunu kuliko mali. Busara ina nguvu kuliko bomu. Maana kichaa aliye na bomu azidiwa na mwenye akili aliye mikono mitupu. Je wajua busara ya tembo kulala nje ilhali ndege ana kiota tena chenye joto mwanana? Ni wangapi wana vichwa vikubwa lakini akili kidogo? Hakika ukubwa wa kichwa ungekuwa ndiyo wingi wa akili tembo angevumbua kila kitu.
Je ni wapumbavu wangapi wanajisifu na tunawasifia kwa upumbavu wao? Je kati ya wapumbavu na wenye maarifa ni wapi wengi duniani? Tatizo kubwa la waja ni kila mmoja kujifanya hayamhusu. Hakuna dhambi mbaya kama kuona uovu ukitendeka usikataze halafu ukaanza kulalamika lalamika. Kufanya hivi hakuna tofauti na mainzi mafu kwenye mzoga unaoshambuliwa na mbweha na mbwa mwitu. Wenye hekima ni kama tumbusi. Tumbusi humfukuza hata simba kwenye mawindo yake. Yeye hana wala hajui kulalamika bali kutenda.
Tofauti na tumbusi ashambuliaye wana wa wenzie, wenye akili huokoa wana wa wenzao. Maana wanajua dunia siyo wao tu bali mwendelezo wa maisha kama mbio za kupokezana vijiwe. Tofauti na tumbusi ategemeaye ukali wa makucha yake, wenye busara hawategemei ukali wa maarifa yao bali kanuni za maisha za kiutu. Kwa wenye maarifa, kuwa nayo ni ukombozi kwa dunia tofauti na tumbusi ambaye ujasiri wake ni wa kujaza tumbo tu. Huyu hana tofauti na wale wenye kutumbia utumbo kufikiria badala ya ubongo. Wengine hutumia makamasi kufikiria badala ya ubongo. Heri ya tumbusi; yeye ni hayawani na siyo hayawani mtu ageukaye hayawani kutokana na kuwa mtumwa wa tumbo. Kama nyoka angepewa miguu asingepewa sumu.
Chanzo: Raia Mwema jana.

No comments: