How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday 24 September 2024

Mume Si Fedha, Elimu, wala Madaraka


 

Hivi karibuni kumezuka matapeli hata wadhalilishaji, tena wengine wasomi, wajiitao wataalamu wa ndoa na saikolojia ya mwanamke wanaipotosha jamii hata kuiibia kwa kisingizio cha kutoa ushauri juu ya ndoa. Watu hawa, kwa kujua na kudandia mfumo dume, wawe wanaume hata wanawake, waganganjaa, waganga wa kienyeji, na viongozi wengi wa dini wa kujipachika wamejigeuza wataalamu wa saikolojia ya ndoa na wanawake. Wanatoa ushauri ambao hauingii akilini vinginevyo mwenye kuuchukua na kuuamini ima awe na mjinga hata mpumbavu wa kutupwa, kuzidiwa, kutapatapa au kukata tamaa.
            Hivi karibuni tulitumiwa clip ya mshauri anayetambulishwa kama daktari wa saikolojia. Jamaa huyu anaongea bila aibu tena kwa mjumlisho (generalisation) na kujiamini. Anadai eti wanawake ima ni kama watoto au ni watoto kwenye masuala ya kutafuta fedha. Anadai kuwa kila mwanamke anaamini kuwa kila mwanaume ni gwiji wa kusaka pesa. Hivyo, wanaume wasilalamike wanapokuwa hawana fedha. Je hii ni kweli?
            Sisi kama wanandoa ambao tumedumu kwenye ndoa kwa miaka 27 tumestushwa na ushauri huu wa ajabu na hovyo. Kwa kutumia ujuzi na uzoefu wetu, tumeona huu ima ni kutojua, udhalilishaji wa akina mama au hata kuganga njaa.  
    Kwanza, haiwezekani wanawake wote, kama binadamu yeyote, wakawa na tabia sawa katika jambo moja, yaani uwezo wa mwanaume kutafuta fedha. Hata wanyama hawana tabia moja inayofanana kwa wote kwenye jambo moja. Hata mbuzi hawafanani kitabia. Mmoja anaweza kupenda kushambuliwa mashamba na kula mazao. Mwingine anaweza asipende kushambulia mashamba kwa vile alishaumizwa alipofanya hivyo nakadhalika.
         Kimsingi, uwezo wa mtu wa kutafuta au kutotafuta fedha unategemea mambo mengi kama vile mipango, motisha, uzoefu, malengo, makuzi, ndoto, aina ya jamii anamotoka, muda, mazingira, aina ya shughuli anayofanya kumuingizia fedha nakadhalika
        Pili, ni imani potofu kufikiri kuwa kila mwanamke, ima ni tegemezi au anaolewa kufuata fedha na si kutekeleza malengo na mipango yake kama binadamu. Hivyo, licha ya kuwa udhalilishaji na uongo, ni ujinga na upofu kudhani kila mwanamke anaingia kwenye ndoa kutafuta au kufuata fedha. Ingekuwa hivyo, wanaume maskini wasingeoa. Haimaanishi kuwa hakuna watafuta fedha katika ndoa hasa wanaosukumwa ima na tamaa binafsi au baadhi ya mila za kinyonyaji kama vile kutaka mume awe buzi la kumtunza mhusika na watu wake. Hii siyo kwa wote.
        Tatu, ni imani potofu na kutowajua wanawake kama binadamu wa kawaida wenye uwezo sawa na wanaume kudhani kuwa ni tegemezi kwa wanaume, hivyo, wanafikiri kuwa kila mwanaume ni mashine kutapika fedha yaani Automated Teller Machine (ATM) ambayo huwa haiishiwi au kukosa fedha. Hata ATM, wakati mwingine, huishiwa fedha na kungoja wahusika waongeze nyingine.
        Nne, kuna wanawake matajiri ima wa kutafuta au kurithi wanaojua kuitafuta, kuitunza na kuitumia kuliko wanaume ambavyo pia wapo wanaume wa namna hii. Unapodai eti wanawake wote wanaamini wanaume ni ATMs, unajikumbusha kuwa wapo matajiri, wasomi, wenye madaraka tena makubwa kuliko waume zao? Hawa nao si wanawake?
        Tano, ni wanaume wangapi waliooa wanawake matajiri kama vile Mtume Muhammad aliyemuoa Khadija mama aliyerithi utajiri mkubwa licha ya kuwa mfanyabiashara maarufu zame zile kule Makka. Je hili nalo watalisemeaje hawa watalaamu wetu wenye kutia shaka? Je waliioa tena wanajulikana toka kwenye familia maskini nao vipi?
        Pamoja na utaalamu, usomi na mengine kama hayo, wengi tunashauri kutokana na maisha yetu yaliyojengwa katika misingi fulani. Hivyo, usishangae mshauri unayemuamini au kumtegemea sana, akashauri kitu kisichokuingia akilini. Hivyo, tunasema asemacho kinaweza kuakisi ya maisha yake binafsi ambayo pia yanaweza kuhitaji ushauri japo yeye ni mshauri. 
        Binadamu hawezi kukimbia maisha na tabia zake. Kinyonga hata abadili rangi zake vipi bado ni kinyonga. Kama umesomea ushauri na maisha yako hayafanani na unachoshauri au unashauri utopolo, jua kuna tatizo. Faida za kitu chochote lazima zianze nawe. Huwezi kuhubiri maji ukanywa mvinyo. Kwa ufupi, katika ndoa, mume au mke si elimu, fedha, au madaraka bali ni mume au mke basi. Mengine, ni makandokando tu.
Chanzo: Mwananchi J'pili.

No comments: