How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday 25 September 2024

Kwanini Tumeamua Kuwa Wafungwa wa Hiari?


Mafyatu wenzangu naomba nianze na swali la kifyatu. Umewahi kujiuliza ni kwanini tumejigeuza au kugeuzwa wafungwa katika magereza ya kujitakia tena kwa kuyajenga wenyewe? Naona yule anatikisa kichwa. Nadanganya au huoni? Nenda uishiko. Kama kuna kibopa, angalia mjengo wake. Kila mjengo uitwao mjengo, umezungushiwa kuta. Je kuna tofauti gani na gereza? Je hili ndilo jibu? Je tatizo ni nini? Je tufanye nini? Je hatujiingiza hasara wakati njuluku ya kuondoa insecurity ni ndogo kuliko ya kujenga mikuta?

 Hata magereza yana nafuu kwa sababu unatumikia kifungo chako unaachiwa huru. Hili gereza la kujitakia ni la maisha. Kuwa huru ima ufe au upae mbinguni na mwili wako kama kile kitegemezi cha Josefu wa Nazareti kwenye zile ngano za zamani. Pia, unaweza kuwa huru kama utakuwa apechealolo aka kapuku.Japo ukapuku ni kitu kibaya, lau unakupa uhuru ambapo ukwasi unawafanya mafyatu wenye nao kuishi magerezani tena ya kujitakia na kujilipia. Hapa ndipo ulipo mzizi wa shule ya leo.

Acheni ufisadi kwani unazalisha wizi iwe ni wa kujitakia au kulazimika.

Tumegeuka jamii ya mijizi, mibaka, na vibaka. Mtu analala maskini. Anaamka tajiri. Hatuhoji wala kushuku ni miujiza gani amefanya! Hivi hawa mafyatu wanaokokotoa mafyatu badala ya kokoto mbona hawakokotoi hawa majambizi? Leo jambizi linatufyatua na njuluku zetu. Badala ya kulifyatulia mbali likafyatukia ima gerezani au kuzimu, eti tunaliabudia. Ebo! Enyi mafyatu wakumbaff, nani aliwaroga hadi mkafyatuka kinyume na kuabudia majizi na masanamu?

Mie Ntume Fyatu kwa mafyatu nasema, fyatueni majizi na majambazi wa njuluku zenu bila kujali cheo wala saizi. Inakuwaje mnaabudia mihalifu na kuwadharau madingi waadilifu waliotumikia jamii kwa uadilifu maisha yao yote wanaishi kimaskini wakati vibaka waliozaliwa jana wanaishi na kuogelea kwenye utajiri usio na maelezo wala kueleweka? Tell me. Naona yule anacheka akidhani sikijui kitasha wakati nilizaliwa utashani na kukulia umakondeni. You get it or it gets you? Usinicheke kwa kuongea broken ingilishi wakati wewe unaongea kiswanglish kama waishiwa wa njengoni. 

Mafyatu wa hovyo na wenye roho za wizi wanasema eti ujanja kupata. Ujanja si kupata ni umepata kihalali? Kama wewe umetumia kalamu kuiba, kwanini mafyatu wasitumie mapango kukuibia? Kama umetumia mtutu kuiba, nawe lazima tukunyake. Kama unateka wenzako na kuwapoteza, lazima tukunyake liwalo na liwe. Unapofyatua au kupiga njuluku za mafyatu, unatengeneza jamii isiyo salama na maskini. Wanene wanazidi kuiba ili kujenga mikuta na kuongeza walinzi wasijue kifo kinapenya hata kwenye moto.

         Hata ujizungushie mibomu ya nyuklia, kifo kikiamua kukutembelea kinakunyotoa roho tu. Je hizi kuta zinakupa uhakika wa kutofanyiwa kitu mbaya? Hebu jamanini tufikiri pamoja. Tumeishiwa akili hadi tunajisalimisha kwa jinai tena jumla na kirahisi hivi? Nani katuroga ingawa fyatu simo?

            Huwa nashangaa kuona mafyatu wakishangaa wafungwa wanapokuwa wamelindwa. Kwani, hao mandingi wenu hawalindwi kama wafungwa? Hawafungwi na ulaji wao tena mwingi wa haramu? Kama siyo wafungwa, kwanini wanalindwa? 

        Mbona mimi silindwi? Si kwamba mie sina njuluku za kuweka mabaunsa, sina kwa sababu siyo mhalifu wala siyo mshamba na wala usalama na uhai vyangu havitegemei ulinzi bali uadiilfu wangu. Hivyo, sihitaji makandokando wala makomando, kunilinda au kujieleza. You know what I mean. Nani anapenda kuishi kama msukule kulindwa wakati ulinzi wa kweli ni kugawana na kutendeana haki? 

        Hapa Ukanadani, majumba yetu hayazungushiwi kuta bali maua. Unaweza hata kulala mlango wazi na usiwe na hofu kwa vile kila fyatu hapa anakula na kushiba. Hili ndilo jibu la kuwa huru na salama. Pia, hili ndilo kubwa nililojifunza utashani. Lazima wanene wahakikishe wadogo wanapata milo yao yote mitano kwa siku. Nani anataka ulinzi wakati ulinzi wenyewe bandia? Anayelinda Mungu. Huoni hata papa na wachungaji mbali na wachunaji wanaojifanya kutenda miujiza wanalindwa na binadamu na bunduki kwa vile hawamuamini Mungu wanayemhubiri na kutumia kutengeza njuluku? Mie siyo bwege wa kupatikana nikidhani nimepata kama wao wanaolindwa kama wahalifu.

            Leo naandika kwa uchungu tokana na mafyatu wangu walio wengi wanavyosota. Pia, wote tunaangamia na kuangamizana tokana na kutoa majibu yasiyo sahihi katika matatizo yetu kama jamii ya mafyatu. Ukitaka jamii iliyo safi na salama, tenda haki. Hakikisha kila fyatu anafyatua milo yote mitano kwa siku uone. Badala ya kupoteza njuluku kwenye vikuta na walinzi, unakuwa na ulinzi wa uhakika. Huku hutuogopi ndata wala kutekwa. Nani atamteka nani wakati utekaji ni jambo la kijima na kinyama? Hata waanimo hawatekani. Huku waanimo wana haki sawa na mafyatu. Hivyo, usishangae jirani yako kuwa sungura tena aliyenona asiyeogopa kufyatuliwa na fyatu jangili kama huko.’

            Leo, nawataarifu kuwa nimeastaafu siasa. Hivyo, nitakuwa nafyatua mambo ya kijamii na siasa kwa mbali pale nitakapohisi kufyatuliwa. Wasalaaam.

Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: