Tokana na uzoefu, kwa kuona au kusikia, tunajua wanandoa wanaoishi maisha ya utengano usio na ulazima au sababu. Wanatenganishwa na aina na mihangaiko ya maisha kama kufanyia kazi sehemu tofauti. Pia, wapo wanaoishi mbali mbali tokana na mazoea na mila za baadhi ya jamii. Mfano, kuna jamii au makabila yanayoamini kuwa lazima wawe na mashamba na mifugo vijijini walikozaliwa. Hivyo, mara nyingi, mama ndiyo hupewa jukumu la kuangalia mali za familia huko kijijini. Utasikia mtu anasema kuwa mke wangu anaishi kijijini kuangalia ng’ombe au mashamba. Hukuoa wala mkeo kuwa mke wa ng’ombe, mbuzi, kuku, na mashamba bali mwenzi wako wa karibu anayepaswa kuwa nawe wakati wowote.
Japo wanalazimishwa na maisha, je, hilo ndilo jibu au njia pekee ya kuweza kuishi kwa ufanisi bila kujitesa hata kuwatesa watoto wao? Je, wanaofanya hivyo, wanajua madhara ya kufanya hivyo? Hivi, hakuna njia nyingine ya kuishi pamoja na wahusika wakakuza uchumi wao?
Leo, tunadurusu ndoa ya kuishi mbali mbali na madhara yake. Tunajua. Ili familia ifanikiwe na kustawi lazima iwe na kipato. Hata hivyo, kwanini uchumi uchukue nafasi ya mambo mengine? Kwa wanaojua raha na adha za ndoa, kuishi mbali mbali kunaweza kuwa chanzo kikubwa cha kuregarega na kuvunjika ndoa.
Kuishi mbali husababisha upweke si kwa wanadoa tu bali hata watoto kiasi cha kuleta changamoto katika malezi ya watoto. Wakikuyu Kenya na makabila mengine karibu yote ya Kenya ukiondoa ya Pwani, wana utamaduni wa kwenda mijini kutafuta na kuwaacha wake zao walee watoto peke yao. Nini madhara ya hili? Watoto huwa karibu na mama zao na kuwathamini kuliko baba zao japo huwahangaikia na kuwawezesha kimalezi kujiandaa kwa ajili ya maisha ya baadaye ambapo wahusika watakuwa wameishiwa uwezo kiasi cha kuwategemea wasipate msaada waliotegemea wala kukusudia.
Sisi ni wazazi. Tunajua mapenzi ya wazazi kwa Watoto ingawa wakati mwingine mapenzi yanaweza kuwajengea chuki dhidi ya wazazi wote au mzazi mmojawapo. Kwa uzoefu wetu, tunawashauri wazazi wasiwaishie watoto bali wawandae kuyapokea, kuyakubali, na kuyakabili majukumu yao ya baadaye watakapokua badala ya kujiumiza na kuwaumiza kwa kuwaandalia urithi wa vitu ambayo wengi huvifuja tokana na ukosefu wa uzoefu na maandalizi. Mnapowaishia watoto au kutaka muwaachie kila kitu, wakikua watafanya nini? Tunashauri wazazi wawafundishe watoto kujitegemea kwa kuwaandaa kifani na kisaikolojia bila kujiumiza ukihangaika na kuwaachia watoto eti mali. Japo si vibaya, je wao watakapokua watafanyia nini akili na vipaji vyao? Kwetu, urithi mkubwa kwa watoto ni kuwazaa, kuwandaa kwa kesho yao ambayo ni tofauti na ya wazazi tena wengi ambao hawakurithi hata kijiko zaidi ya kuzaliwa.
Hakuna urithi mkubwa kama vile kuzaliwa, kulelewa, na kuandaliwa kwa ajii ya maisha ya baadaye ambao ni bora kuliko fedha, mali, na vitu. Wapo wazazi waliolelewa na kusoma kwa taabu. Wakishapata fedha, huwaharibu watoto wao wakichelea wasipitie magumu waliyopitia wasijue ndiyo shule pekee iliyowafanya wafanikiwe. Kwa mfano, unampeleka mtoto International School kwa vile wewe hukuisomea au kushindana na majirani na ndugu. Akimaliza, unagundua umetengeneza kuku wa kizungu. Unafanya nini zaidi ya kumlaumu na kumuona mwanao kuwa mzembe usijue maandalizi aliyopata kule hayafanani na uhalisia wa maisha? Hili la malezi ya kisasa, tutalipa Makala yake maalum.
Mbali na ugumu wa malezi ya watoto, kuishi mbali mbali kunaweza kuwa chanzo cha vishawishi pande zote hasa lijapo suala la ‘stahiki’ ya wanandoa kimapenzi. Je, huwa wahusika wanafanyaje lijapo suala hili au tuseme tendo la ndoa ambalo katika ndoa ni lazima na muhimu? Ndiyo maana likaitwa tendo la ndoa. Hatupendi kuwahukumu, ila kuna uwezekano wa wanandoa wa aina hii kuwa na namna ya kulipata kiharamu japo si wote na pia, yawezekana wengine wakaishi pamoja na bado wakachepuka. Hilo, tunaliacha kama swali na changamoto kwa wanandoa kutafuta jibu.
Tumalizie kwa kusema. Ni hatari kwa wanandoa na watoto wao kuishi mbali mbali. Msihangaishwe na kesho ya watoto wenu. Kwani, kama mlivyoweza nyinyi, nao wataweza.
Chanzo: Mwananchi Jpili leo.
No comments:
Post a Comment