The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 19 August 2026

Kabla ya kupanga mahari durusu sifa za waolewaji

Kuna mtindo mchafu umezuka wa kutafuta kupata utajiri wa haraka kwa njia ya mahari. Kwa lugha rahisi, huu ni uuzaji wa mabinti zetu tokana na ukosefu wa ubunifu na kufikiri. Japo mahari ni sehemu na hitajio la jamii nyingi kama shukrani kwa wazazi kuzaa, kulea na kutunza mabinti zetu tunaoozesha.

  Katika kudurusu dhana ya mahari, leo tutajikita kwenye mantiki na matatizo yatokanayo na dhana nzima. Tuanze kwa swali. Kweli binadamu anaweza kutathiminiwa na kupata thamani yake? Hatujui kama wale walafi wapendao kutoza mahali kubwa kama hujiuliza swali hili kabla ya kuweka kiwango kikubwa cha mahari ambacho siku hizi kimepanda utadhani kuna kinachouzwa na kununuliwa. Mfano, unakuta binti hajafundwa wala kulelewa vizuri halafu wazazi wanataka mamilioni ya fedha kama mahari! Wengine wanatoza makumi ya ng’ombe kama mahari ili kujitajirisha haraka.
            Tukizingatia kuharibika kwa dunia ya sasa na umomonyokaji wa maadili, unakuta binti lina tabia chafu, huni, na mengine mengi japo si wote lakini wazazi wanataka mamilioni ya fedha kama mahari. Kama tutakuwa wakweli, kuna wengine, kama mahari ni dili walipaswa kutolewa mahari ya fisi au nyoka na si ng’ombe tokana na ubovu na uoza wao. Kwanini wanaotaka kutajirika kwa mgongo wa mahari hawajui kuwa wanafanya maisha ya watoto wao na wa wenzao (waoaji) kuwa magumu!
            Baada ya wahusika kuweka ndani fedha au ng’ombe, binti akiteswa watamlaumu nani zaidi ya ujinga na tamaa zao? Watoto wetu siyo bidhaa tuwauze kwa tamaa, ulafi, na uvivu vyetu. Kinachoshangaza, ukiwauliza hawa wapenda mali kwa kuuza wenzao, wao walitoa mahari kiasi gani, utashangaa.
        Tukitafakari tabia za mabinti wetu hasa wale wenye tabia mbaya, wapo ambao mahari yao ilipaswa iwe fisi au nyoka tokana na walivyo hatari wachunaji wa mabuzi wanaotaka kujitajirisha  wao familia zao maskini kupitia ndoa bila huruma. Kwani, hawapo mabinti na wazazi wanatakao kutumia ndoa kama chimbo la fedha na utajiri?
        Kabla ya kutaka kuwatumia wenzako kujipatia utajiri wa haraka na haramu, jiulize. Ungekuwe wewe ndiyo muaoji, ungependa utenzwe hivyo ua ni yale ya mkuki kwa nguruwe? Kwa wazazi wanaopenda na kuwathamini mabinti zao na maisha yao ya baadaye, viwango vikubwa vya mahari ni jambo lisiloingia akilini hasa ikizingatiwa kuwa hao wanaowauzia hawa mabinti wanaweza kuwatesa kwa kisingizio cha kuwatolea mahali kubwa.
        Isitoshe, ukubwa wa mahari unachangia sana vijana wengi kutooa au kuolewa hadi wengine wanazalishana na kuanza maisha ya ndoa si kwa kutotaka kufuata taratibu bali kulazimika. Ndoa kama taasisi muhimu inalenga kuwakutanisha wawili wapendanao kujijenga na kuishi pamoja na si kukomoana na kunyonywa hata kuuzwa utumwani eti kisa mali na tamaa ya mali.
Ni aibu kubadilisha mwanao na fedha au wanyama. Wazazi tufikie mahali tukubali majaliwa yetu yatokanayo na juhudi, majaliwa, na mipango vyetu.  Pia, tukubali na kuelewa kuwa mabinti zetu, sawa na wanetu ni binadamu kama sisi wanaopaswa kuheshimiwa, kulindwa, na kuthaminiwa.
        Kabla ya kumaliza, tutoe funzo kuwa wote wanaotaka kutajirika kupitia mabinti zao wajifunze kwa Waislam ambao huruhusu binti kujipangia kiasi cha mahari ambayo, pia, si ya wazazi bali yake. Japo hili ni suala la kidini, lina funzo kubwa. Unapomruhusu bintiyo kupanga mahari yake, hawezi kumuumiza au kumchuna anayempenda na kuamua kuanza naye maisha. Isitishe, binti akiachiwa haki na uhuru wa kuchagua mahari, ataangalia mahitaji yake na mwenzake na mahari yake apewayo yaweza kuwa mtaji na nyenzo katika maisha ya ndoa anayoenda kuanza.
        Japo ni vigumu kwa binadamu kubadilika kirahisi na haraka, kuna haja ya kubadilika ili kuepusha mateso wakumbanavyo mabinti na unyonyaji wa wale wanaowao. Pia, tuchukue funzo na somo toka kwa mababu na nyanya zetu ambao mahari zao zilikuwa nafuu na vitu vilivyokuwa vinapatikana na kila mtu alikuwa na uwezo navyo. Mfano, wapo waliotolewa mahari ya jembe, mbuzi, mmoja na vitu vingine visivyomuumiza wala kumnyonya yeyote hadi watu kulazimika kukopa hata kuiba ili wapate mahari.
Chanzo: mwananchi J'pili iliyopita.

No comments: