Tuesday, 10 June 2008

Hawa ni wezi au waheshimiwa?


Huwa napata utata na wakati mwingine kinyaa itajwapo heshima sijui cheo cha mheshimiwa! Huwa nashangaa sana hasa nionapo wanaoitwa waheshimiwa. Wengine hawana wala hawastahili heshima. Wananuka ufisadi. Ni mafisadi hadi kwenye mifupa. Ni mafisi.
Chukua mfano watu waliofukuzwa kazi kwa kushiriki kwao ufisadi wanaoendelea kuitwa waheshimiwa. Hivi kweli hawa ni waheshimiwa? Wana heshima gani iwapo walitenda mambo ya aibu? Waliobainika kuiingiza nchi kwenye mikataba ya kiwizi ya uwekezaji kama vile Richmond na mingine mingi, kweli nao ni waheshimiwa? Je hawa waliojichukulia mali na pesa za umma kwa kutumia madaraka siyo wezi kweli hata kama tunawaita waheshimiwa? Wapo wengi wake kwa waume. Ukiwaona wana sura za binadamu. Lakini ndani ni mafisi watupu.
Je sisi tunaowaita waheshimiwa wakati tunajua ni majizi nasi tunastahiki heshima kweli? Je heshima ni maneno au matendo?
Wanasheria wanasema: mharifu ni yule aliyetenda kosa la jinai au aliyeshuhudia asiripoti au aliyeshirikiana na aliyelitenda. Kisheria mharifu ni yoyote anayeshiriki kutenda kosa la jinai ima kwa kujua au kutojua hadi atakapobainika vinginevyo.
Je hawa waliofukuzwa madarakani kutokana na wizi na ufisadi siyo majizi hata majambazi kweli? Kwangu ni majambazi. Nina sababu:
Kwanza hawajawahi na hawataki kujitetea zaidi ya kukaa kimya huku wakifanya maigizo na usanii vya kisiasa ili waonekane hawana makosa wakati wanayo ili muda upite tusahau. Hatutasahau wala hatutawasamehe.
Pili, ukiangalia historia zao na mazingira hata ya ukwasi wao, hutahofia wala kusita kuwaita majizi. Tunao wengi. Wamo bungeni, serikalini,misikitini,makanisani hata majumbani.
Tunao kwa mamia. Wapo wanaotumia madaraka kujitajirisha huku umma ukiendelea kuwa maskini. Wapo hata wanaotumia neno la Mungu kuwaibia watu maskini na wajinga wenye shida za kimaisha. Ukiwaona utawajua. Hupenda kujisifu na kujisifia. Wanapenda kuabudiwa na kuonekana malaika wakati ukweli hawana tofauti na ibilisi mwenyewe. Maana tulionywa. Ibilisi wa mtu ni mtu aweza kuwa wewe hata mimi. Aweza kuwa mtukufu hata tajiri na msomi. Ibilisi ni ibilisi hata aitwe mchungaji, mheshimiwa, kizito na mfadhili na makando kando mengine mengi.
Hivi aliyesababisha watanzania kulanguliwa umeme siyo jizi tena kubwa lao? Na huyu aliyesababisha madini yetu kuwaneemesha wawekezaji ilhali sisi tunazidi kuwa maskini? Aliyeghushi vyetu vya elimu yake na kutoa rushwa wakati wa uchaguzi siyo mwizi kweli? Vipi kuhusu aliyetumia bunduki kuingilia madarakani? Vipi kuhusiana na mtu asiye na sera za kutukomboa bali kututumia badala ya kututumikia?
Tuzidi kuhoji na kuhoji. Vipi mheshimiwa anayejizungushia mabaunsa na walinzi kila aina. Je anamuogopa nani kama siyo matendo yake machafu nyuma ya pazia?
Hebu fikiria juu ya mtu anayetoa toa ahadi asitekeleze hata moja. waswahili husema; haja ya mja kunena, muungwana ni vitendo. Je asiyetimiza hili siyo mshenzi hata akiitwa mheshimiwa?
Mfikirie anayewadanganya watu. Anasema hili leo kesho lile. Je huyu anayostahiki hata chembe kuitwa mheshimiwa? Mbona uheshimiwa umevamiwa kiasi cha kuwa uishiwa? Mbona uheshimiwa umekosa thamani kiasi cha kutumiwa na majambazi?
Sipingi. Kuna watu na heshima zao. Lakini pia wapo wengi waitwao waheshimiwa wasiostahili hata nusu ya heshima. Wapo wenye silha, hulka na tabia za wanyama waitwao waheshimiwa.Kuna watu wanapaswa kuwa gerezani siyo bungeni wala uraiani. Hebu fikiria anayewatisha watu ima kwa bunduki au neno la Mungu wakati yeye ni tapeli. Hebu fikiria mtu anayewaganywa watu ili awatawale kama yule mshenzi wa kiingereza aitwaye Lugard alivyotufanyia.
Jaribu kufikiria zaidi. Hebu jielekeze kwa mtu anayesimama kwenye viwanja kama vile vya Jangwani akatangaza kutenda miujiza wakati hana lolote bali janja ya kuwaibia wajinga wengi.
Je hawa hawapo? Siku moja tulikuwa tunajadili ni kwanini nchi za kiafrika haziendelei ilhali zimekuwa na serikali kwa zaidi ya miaka 50. Tuligundua mdudu mmoja mbaya sana akiziangamiza nchi hizi. Anaitwa ulafu na ubabaishaji.
Tembelea Afrika kuanzia kaskazi hadi kusi mashariki na magharibi. Utakuta watu wanaojifanya wanawapenda watawaliwa waliwa. Watajionyesha kama wapenda maendeleo wakati wao ni vikwazo vya hayo maendeleo ndoto. Wanaishi maisha ya kifalme wakizungukwa na makapuku wa kunuka. Wao na familia zao, kupitia ujambazi fichi wa kimfumo hawana tofauti na kupe. Wanawanyonya watu maskini kwa kisingizio cha upuuzi uitwao kuchaguliwa!
Wanaficha mabilioni ya fedha Ulaya. Wanachekiwa afya zao na kutibiwa Ulaya. Wameua hospitali, zahanati,shule, mashamba,viwanda na kila aina ya mradi. Bado majizi hawa wanawahadaa watu wanaweza kuwaletea maendeleo. Kwao watu ni familia na marafiki zao. Wameishiwa kiasi cha kushindwa hata kujitambua. Bahati mbaya na watawaliwa nao wameendelea kuuziwa mbuzi kwenye gunia kana kwamba hawana akili wala macho! Bado wanahanikiza wakiwaita majambazi waheshimiwa. Mobutu yule jambazi wa Kikongo naye aliitwa hadi mtukufu. Daniel Moi kule Kenya eti naye aliitwa mtukufu! Kenyatta bingwa wa kupora ardhi eti naye anaitwa baba wa taifa! Ameanzisha taifa gani iwapo nusu ya wananchi wa Kenya hawana ardhi? Je huyu siyo fisi mtu aliyekuwa akijificha nyuma ya madaraka na uheshimiwa?
Hata nifungwe au kupigwa mijeledi, sitawaheshimu waheshimwa majambazi waliotamalaki kwenye nchi za kiafrika. Sitaacha kuwaambia kuwa wao ni majizi na siyo waheshimiwa.
Kinachonikere sana ni kuona wezi hawa waheshimiwa wakitukoga kwenye mitaa ya wazito kwa ukwasi wao. Wengine wamezidisha kufuru. Eti bado wamo bungeni badala ya Ukonga! Eti kuna wanaopanga kurejea kwenye medani ya uongozi kwa kishindo baada ya kunyea kambi! Jamani hadi mtajwe majina ndipo mstuke!
Kama kuna waheshimiwa ningependa kuwapa heshima zote si wengine, ni wale waliofungwa kwa makosa madogo madogo kama wizi wa kuku. Ni wale wanaobeba zigo la taka la waheshimiwa wezi.
Tuhitimishe. Kuna haja ya kubadili mfumo wetu wa kijambazi unaotoa uheshimiwa hata kwa majambazi. Kuna kila sababu ya wasomaji na wananchi kwa ujumla kuanza kutafuta jibu la kejeli na matusi haya kuhusiana na cheo cha mheshimiwa. Mheshimiwa au mwizimiwa?
Leo sisemi sana . Nawashauri wale waheshimiwa-fisadi wanaojijua kuwa mibaka na majambazi, waachane na siasa na kwenda kuzimu. Salamu kwa Bilionea wa vijisenti na chenga kwa sana , mvi nyingi Eddie Ewassa, Niziro Kadamage, Pesatatu, Jigoda, Muigai na waheshimiwa mafisadi wengine.

Source: Dira ya Tanzania Juni 10, 2008.

2 comments:

Anonymous said...

Kazi nyingine matata iliyosimama!
Sasa sijui hawa mafisadi wanasoma haya maneno au ndio hivyo tena wanazipa jicho halafu wanapiga chini!
mmmh!!nahisi wako wengi hivyo wanasikilizia mpaka mmoja wao atakaposhindwa kuvumilia maneno ya hekma ambayo WaNANCHI wanatoa day mpaka day, yanayokongoroa hata mioyo ya FIDADI DUME, ndipo waanze kujieleza!
Tusubiri tuone.
Lakini kazi nzuri, bado nafanya utafiti kumtambua Mwizimiwa Pesatatu.
Mchizi.
ukowazi@yahoo.com

Anonymous said...

Tena na tena kazi nzuri.
Twendelee kupiga mawe tuuuu...Mpaka wazaliwe mafisadi wengine baada yakuanguka kwa hawa wanaofikiri wamesimama.
Mchizi.
ikowazi@yahoo.com