Wednesday, 25 June 2008

Kijiwe chawafukuza mafisadi

SIKU hizi Mpayukaji nimepanda cheo. Naitwa Nabii Mpayukaji (Mungu Anizidishie Neema-MAN).

Ndiyo nimerejea kutoka kwenye maulaji ya mkutano wa Sullivan. Kijiwe kimekaa kama kamati ya kuokoa mali za Watanzania na kutoa amri ya kufukuzwa kazi wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi. Tufanyeje baada ya mkuu kututosa? Kwa ufupi nilikaribishwa kwenye mkutano huo. Nilikutana na marafiki zangu wa zamani muhimu akiwamo Olusegun Aremu Okikiola Matthew Obasanjo, rais wa zamani wa Nigeria aliyetoa cheche.

Alitupa hotuba kabla ya kuisoma. Baada ya kupeana mikono na kukumbatiana, nilimsifu kwa hotuba nzuri na ya kusisimua iliyowaacha mafisadi wakubwa wakizizima na kujuta kwanini walimkaribisha mpayukaji Obasanjo na mimi.

Kuna mijitu ilinyimwa aibu! Unajua wakati Obasanjo akimwaga cheche, jamaa lilikuwa likichekelea utadhani utani! Mzee Obasanjo alitoboa kuwa nchi ya Musa sasa imevamiwa na mdudu na inanuka, hivyo mkuu aisafishe akijisafisha na yeye mwenyewe.
Hayo tuyaache. Mgosi Machungi analianzisha: “Wazee timewaita ii kutoa shinikizo na hanikizo kufukuza watu tinaowatuhumu kuuza kaya.”


Kabla ya Mgosi kuendelea, Mbwa Mwitu anadandia mic. “Afadhali. Maana baada ya kusikia mipasho kapa ya Lupaso na kuwa bize na kumzika mkolimbwa Balaliii, hawa wahuni walidhani tutasahau. Hii kaya ni yetu si ya mama zao akiwamo na mkuu. Lazima tuwawajibishe watu kama kijiwe cha Idodomya kilivyowafanyia akina Ewassa, Kadamage na Bangusilo M7ha.”

Makengeza anapaaza sauti na kusema. “Tuwataje kwa majina wajijue tunawajua na tunataka waachie ngazi mara moja.” Mara Wanakijiwe wanahanikiza: “Toboa, Toboa.”
Makengeza anaendelea: “Hakuna haja kuzunguka wala kuogopa. Yupo Mkurugenzi wa Taasisi ya Kulinda na Kueneza Rushwa, Dk. Ed Oshea. Huyu anatuhumiwa kujilimbikizia mimali itokanayo na ufisadi.”


Anakwanyua kombe lake na kugida kahawa na kuendelea: “Yupo Grei Mgonjwa wa EPA. Anatajwa kwenye mama wa wizi pale Banki Kuu. Pia yupo Emmie ole Naakome wa Thieves and Insiders Community - TIC.”

Kabla ya kuendelea kumwaga razi, wanakijiwe wanahanikiza: “Taja wote mkuu ajue tunajua na hatuwataki hata kama yeye kwa sababu zake anawataka.” Makengeza anaendelea: “Kuna Johnison Mwananyika anayejifanya wakili mkuu. Pia yupo…”

Naye Kapende hajivungi. Anaongeza: “Mbona hujawataja mafisadi tuliowapiga kibuti hivi karibuni wanaong’ang’ania kijiwe cha Idodomya? Acha niwataje. Hawa ni Eddie Ewassa, Niziro Kadamage, Ibra Bangusilo M7ha, Bazee Pesatatu Miramba, Jose Muigai, Endelea Chenga, na wengine.”

Mara Mpemba anadakia: “Yakhe hujataja wote ati. Mboni Sammy Chitaahira aliyeghushi vyeti huntaji? Pia hata Blunders Goosebelt alotoa rushwa?” Mara anakumbuka jambo. “Hata huyu Maasha anayetajwa kuwa nyuma ya pesa ya EPA naye atajwe hata kama amemwajiri Riz, huyu mtoto wa nkuu.”

Anabusu kashata na kuendelea: “Mie siku zote nshangaa nkuu! Adhani hatujuwi hawa wanavonajisi kaya? Watimue hawa ati. Tushachoka nao.” “Mpemba umenena. Jitu bila aibu linang’ang’ania ofisi ya umma utadhani ya mamake! Tumechoka na majambawazi yaitwayo waheshimiwa wakati hayana heshima bali ulafu,” anapayuka Mkurupukaji anayemaliza kuweka nakala ya gazeti la Tanzania Daima mezani linapogombewa kama mpira wa kona.
Mchunguliaji anatia guu. Amekunja uso: “Hii mijitu sijui imeingiliwa na nini? Sijui inampa nini mkuu hadi anaivumilia? Au lao moja sawa na Tunituni?”


Kabla ya kujibu Mbwa Mwitu anajibu: “Hujui! Imeingiliwa na mdudu aitwaye ufisadi! Haina tofauti na mafisi wala mbwa. Pia mnaotegemea mkuu awafukuze wenzake mfikirie upya. Tangu lini ngamia kamcheka nundu ng’ombe? Lao moja tu piga ua.”

Kijiwe hakina mbavu, hasa anapotamka neno kuingiliwa. Maana siku hizi Kiswahili kimevamiwa na wachafuzi wanaobadili maana. Lakini kwa tafsiri na maana yoyote watu hawa wameingiliwa na kitu kisicho cha kawaida. Inashangaza wanavyoweza kuwatumikia mabwana wawili, mali na umma! “Lazima wameingiliwa tu. Huwezi kuwadanganya watu nawe ukajidanganya kama wanavyofanya kukalia ofisi za umma wakiwa hawana udhu, utashi na uwezo,” alitilia mkazo Makengeza.

Kabla ya kuendelea, mara Kapende alikwanyua mic. “We unashangaa uongo wakati ndiyo umekuwa ndiyo sera ya kaya hii! Iko wapi safari ya kwenda kula mana na asali aliyotufunga nayo jamaa? Huoni ndo tunazidi kuchanja mbuga kuelekea Misri? Tutashindaje iwapo Firauni anapewa kila aina ya utetezi na kinga? Sijui kwanini aliamua kumuita mwenzie Firauni!” Bila kutoa taarifa mara Mpemba alidakia na kuja na pwenti iliyoamsha mizuka ya kijiwe. Alikuwa na gazeti moja mkononi lililokuwa limemnukuu mbunge akisema hapatatosha na patachimbika bila jembe kama ufisadi utaendelea hata kama NEKI inawasafisha mafisadi kama TAKUKURU ilivyojaribu ikishindwa.

Akiwa anatikisa kichwa kwa hasira anasema: “Jama mie baada ya kuchangia niliamua kusoma gazeti la leo. mwaona huu mwanko mpya wa wabunge wenye akili? Wakiri kaya ishauzwa zamani. Hapa kazi kwetu kuanka na kuwakabili hawa maruhuni wallahi.”

Msomi Mkatatamaa utadhani kashikwa pabaya! Anakwanyua mic na kuanza kutoa cheche: “Wanaotaka mkuu awafukuze mafisadi waliomo maofisini wanakosa pwenti. Hivi amfukuze nani iwapo wote lao moja? Au hamjajua ubia huu? Hamjui ulaji huu uliosaidiwa na takrima uliwezeshwa na hiki mnachokiita ufisadi?”

Anavuta kombe lake na kupiga tama tatu na kuendelea: “Ukitaka kujua kuwa tunampigia mbuzi gitaa angalia Ewassa alivyotimuliwa na Bunge baada ya mkuu kujifanya hayamhusu. Pia angalia nyuma ya pazia Ewassa na wenzake wanavyozidi kunema.

“Yaani hata kiama kinawasifu kuwa hawakutenda makosa! Tungekuwa na watu wenye akili mbona hata huko Idodomya wangekusikia? Tungekuwa na vichwa si maboga mbona Ukonga ingeishajaa zamani? Nani alianzishe iwapo wote wameoza? Kama nisemavyo daima ni waliodanganyika kuamka na kuchukua chao bila kuchelea lolote wala yeyote.

“Kwanza mafisadi pamoja na kuwa na rungu wameishachoka na kusambaratika, sema wanakaya wanashindwa kumalizia. Baada ya kutimliwa Ewassa wamedhoofu. Ni kama kumsukuma mlevi kama tutataka kuwatoa nishai wanahizaya hawa.”
Anatukana bonge la tusi na kuendelea. “We waacha waendelee kucheza makida makida wasijue alama za nyakati zimebadilika. Nimeona upuuzi wa NEKI. Eti inamsafisha Ewassa! Nani aweza kumfufua maiti? Mbona NEKI imejua kututukana tusi zito!


“Naye anajidanganya anaweza kurudi kwenye ulaji kama mzee Mwinyi! Anacheza na mzimu na laana za Mchonga nini? NEKI imefanya upuuzi kama wa Chitaahira? Ila wajue hatutakubali kuendelea kugeuzwa mashamba yao na mashoga zao na vyangu wenzao.
“Kinachokera sana ni kuona watu wazima wakifanya mambo ya kitoto. Hivi hawajui kuwa kwa kaya yenye neema kama yetu haipaswi kuishi kwa kuomba omba ingawa wakuu wanajisifia na umatonya huu wa mchana?”


Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anachomekea: “Pakua aa sorry pasua kaka wa kitabu.” Msomi anatabasamu na kuendelea: “Sasa tutoe msimamo. Tuwatake wale wote wenye kuchukia ufisadi waamke tuwakabili mafisadi. Pia kijiwe kiandae maandamano ya kulaani upuuzi wa Neki na kuwaunga mkono wabunge wenye akili kama Annee Kilangoo Malichelea, Lazarus Nyarandi, Silaha na wengine.”

Ananigeukia na kusema: “Muulize Nabii Mpayukaji hapa.” Sisemi kitu natabasamu kwa kupewa maujiko.
Anaendelea: “Mafisadi mliomo maofisini mwetu jiandaeni lazima tutachenjiana siku si nyingi.”
Akiwa anajiandaa mara gari la Stivi wa Tunituni lilipita, tukalirushia mawe na kutawanyika.
Source: Tanzania Daima Juni 25, 2008.

No comments: