Thursday, 5 June 2008

Mpayukaji na mipasho kapa na utumbo ya Lupaso

Baada ya kutoka Ziroziro, kijijini kwa Mkolimbwa, Daudi Ballali, gavana wa zamani wa Banki kuu yenye mawizi makuu na kutokuta matanga nyumbani kwa marehemu, niliamua kutimkia zangu Lupaso kusikiliza mipasho kapa ya Mwana wa Matonya mjasiriamali damu damu.

Sikwenda Lupaso kusaka hisani kwa mtu aso hisani aishie kwa kutegemea hisani ya watu wadogo kwake.

Nilipita Nakapanya nikajionea Chamaki nchanga (panya) anavyotafunwa utadhani hakuna dini!

Nieleze kwanza. Watu wamepigika kule sina mfano. Wamepigika hadi kufakamia uongo na misaada makapi itokanayo na ukwapuzi kwenye kaya! Hayo tuyaache yana pake.

Nikiwa natafakari hili na lile tayari kusikiliza kitakachoongelewa hasa kuhusiana na madai ya ufisadi wa familia nzima na genge la marafiki, mara niliona gari lenye namba za ANBEN likiwa limesheheni misaada yenye nembo za Kanada.

Sijameza mate naona jingine la Tanpower, mara la Fosnik, la Kiwira hilo, la TASAF, mara la Fursa sawa kwa First ladies, mara Kagoda, Deep Green Finance, Tangold na mengine mengi kama haya!

Nikiwa nashangaa shangaa mara mzee wa dole tupu bingwa wa mipasho asiye na bendi anasimama mimbarini kumwaga cheche. Jamaa anaijua mipasho japo zamani ilikuwa viwanja vya wachovu kujimwaga na mitusi yao waliyoiita taarabu.

Mzee huyo. Anaanza kumwaga cheche-longo longo. Ajabu niseme. Anasema uongo mchana kweupe na watu wanauamini kiasi cha kumdanganya naye kwa kumshangilia wakati wanashangilia misaada makapi aliyokuja nayo. Hapa haijulikani anayemgeuza mwenzie bwege!

Anasema kwa kinywa kipana. "Wanaosema nilikwanyua njuluku ni waongo, waongo waongo na huu siyo uongo niaminini"

Anaendelea baada ya kufuta kinywa kilichojaa mapovu. "Hawa hawana lolote isipokuwa chuki ya kuwanyima hisani."

Kweli kuna binadamu walinyimwa aibu. Baba zima linatema uongo na kujisifu limewajibu wabaya wake! Yaani unapayuka uongo mweupe huku ukiwaita watu waongo wakati muongo tena mkubwa wewe!

Moyoni najisemea. "Mbona huyu anajivua nguo hadharani akidhani watu hawajui yake? Au laana za Nchonga;mwe!"

Eti anadai tusisikilize uongo wa wale! Tusikilize wako? Mbona hawa waliotaka fadhila ni wa kuchongwa? Au anaongelea fadhila kwa familia yake na marafiki zake na wawekaji?

Jamani uongo ni uongo hata unenwe na mkubwa au msataafu.

Tulidhani angekana kuwapo na kuwa na uhusiano na ANBEN ambayo tunaambiwa ni vifupi vya majina yake na mamsap wake. Mbona anaumbuka. Mbona naona magari ya ANBEN, Tanpower, Fosnik na upuuzi mwingine yamesheheni hapa?" Nilijiuliza bila kujijibu.

Hivi uongo ni upi? Kudai jamaa alikwapua kiasi cha kupanajisi patakatifu pa patakatifu? Mbona aliyeanza kusema ni Mchonga maneno na vinyago vya Mpapure aliyemchonga yeye? Au naye alinyimwa fadhila? Utajuaje huenda alinyimwa fadhila ya kulindwa Azimio lake la Arusha na watanzania wake.

Give the devil its due. Kwangu kama Yuda angekiri kuwa alipewa vipande vya fedha awe salata wa Mwana wa Adam ni ukweli hata kama Yuda ni salata.

Hivi uongo ni upi? Kusema Kiwira ilitwaliwa tena kijambazi; au kusema Bi Mkubwa alikuwa mfanyabiashara tena Chinga kama nonihino wake tena akiwa patakatifu pa patakatifu? Je uongo ni kusema kuwa Fosnik ni kampuni mtoto au ANBEN ni baba na mama lao?

Jamani tunapelekwa wapi kule ambako watu wazima wanafanya mambo ya kitoto mchana kweupe?

Zamani tuliamini kuwa waganga njaa ni wana muziki peke yao hasa wa mipasho na ndomboro! Kumbe tulinoa. Mbona wapo wengi tena wanacheza ndomboro makanisani huku wengine wakicheza ndomboro kwenye majukwaa ya kisiasa!

Kumbe hata kwenye siasa kuna wachovu na wachumia tumbo tena wenye majina. Mie nilidhani jamaa angetoa hata salamu za rambi rambi kwa mtumishi wake Daudi Ballali mkolimbwa aliyewatumikia wenye matumbo wakaishia kumtoa kafara ili siri zao zisitoke!

Nasikia aliyemkolimba anajulikana na ni mtu ambaye huwezi kumtarajia. Jamaa ana sumu kali. Lakini naye mwoga. Anapenda kupendwa wakati hapendi maendeleo yetu.

Hayo ya Ballali tuwaachie wapayukaji wa pale kukuu wanaosema kwa vinywa utadhani vimegeuka njia ya kutolea uchafu!

Tulidhani Mkahapa angegusia anachojua kuhusiana na Kagoda, Meremeta, Deep Green Finance, Tangold na kutoa maelezo juu ya jinsi alivyoweza kujenga mahekalu pale Mkuzi na Sea View bila kusahau pale YMCA ukweni.

Tulidhani angeelezea anachojua kuhusiana na M bank. Tulidhani angeelezea jinsi dili la Net Group Solution lilivyotoa faida kwa mjasiriamali na shemegi zake.

Tulitegemea angetoa taarifa juu ya mafanikio ya kampuni za kikaburu alizoziamini akazipa Air Tanzania na marehemu NBC ambayo nasikia ilifanya miujiza kurejesha pesa ya manunuzi ndani ya miezi.

Jamaa kwa kukufuru sina mfano. Eti anasema anaishi kwa pensheni! Au ni yale ya akina Fred walioishi kwa kukopa kwenye mifuko ya pensheni wasirudishe ili waonekane wanaishi kwa pensheni?

Hivi jamaa huwa ana washauri au washauri wake ni Nick na Ann na Fossie? Maana matapishi aliyotapika hata kama alitapikia kwao alikokuwa amepapiga kibuti kwa muda mrefu, yamemvua nguo.

Anasema bila aibu eti tunaodai alikwapua tulinyimwa hisani naye! Nani amuombe hisani kiumbe anayelindwa kama mtoto mchanga. Nani atafute hisani kwa mtu ambaye ujio wake ulitokana na kufanyiwa hisani ya kuaminiwa na mzee aliyekuwa hana wa kumrithi asijue alikuwa akimwamini nyoka mayai?

Nani angetaka hisani kwa mtu aliyekuwa hajui atokako wala aendako? Juzi nilisikia wazee wa kizanaki wanataka kumtema kwenye familia yao maana hawana mila ya kuza mibaka. Sijui nao waliposikia mipasho kapa ya Lupaso walisemaje na kujisikiaje?

Hivi na Kikwekwe aliyasikia haya matapishi ya Lupasho? Kama kweli anamaanisha anachosema kuwa anadhamiria kuikomboa kaya toka Misri alipoiacha Filauni Mkahapa, basi inabidi arejee kufikiri upya kuhusu kinga yake ya kishikaji.

Naona nambari wahedi imeishaanza kujitenga na jamaa.

Jamani kuna haja ya kuacha uvuvi wa kufikiri kama jamaa. Kwanini tusimtafutia chumba pale Ukonga ili angalau ajifunze kupima maji kabla ya kutia mguu?

Juzi alizomewa tukatuma Fanya Fokyo Ukome. Ila tujue watu wamechoka na kuna siku wataacha kuzomea wafanye kweli. Maana wanaoibiwa na kudanganywa ni wao wanaoishi maisha ya kipensheni wakati wezi wachache wakiibia mifuko ya pensheni na kuwadhihaki wanaishi kwa pensheni.

Kabla ya kumaliza siwezi kuacha kuonyesha mstuko na unywanywa niliopata baada ya kuona gwiji wa falsafa akigeuka gwiji wa uongo na lugha za kihuni. Kusema ukweli nilistuka na kumuomba Mungu asiniadhiri hadi kufikia hatua kama hii ya kugeuza domo kuwa bomba la kutolea uongo na uchafu.

Nimalizie kwa kumtaka jamaa aache uhuni kama alivyosema jamaa mmoja wa wapingaji. Badala ya kuja na uhuni aje na ukweli. Ikibidi atubie wanakaya ni watu wa amani wanaweza kumsamehe ili mradi arejeshe njuluku zetu na kutoa ushahidi dhidi ya wale aliowapendelea wakaneemeka wakati sisi tukizidi kuteketea na kuongopewa.


Mwisho naomba ukisoma waraka huu uuchane. Maana haukulengwa kuchapishwa magazetini bali inaonekana kuna mhariri kibaka ameuiba na kuutoa. Ni top secret. Nimefanya hivyo ili kumlindia heshima mtu mzima hovyo watoto wasije wakausoma na kujua uhovyo wake wakatucheka wote.
Huo ndio waraka juu ya mipasho kapa toka Lupaso kule kwenye nchi ya wangumi. Hii ni nchi ya kufikirika msije mkaikosea na Lupaso ya Mtwara.

Source: Tanzania Daima Juni 4, 2008.

2 comments:

Anonymous said...

Nakubaliana sana na article hii. Tumechoka kudanganywa kijinga jinga. Eti ni watu ambao
"nilikataa kuwapendelea" ambao wanaeneza maneno haya ya uwongo. Huyu mtu anatufanya sisi watoto kwamba hatuwezi ona mambo yalivyowazi. Au labda ujumbe aliotaka kutoa ni kwamba hawa watu wanaeleza ukweli baada ya kutopendelewa na wao pia, baada ya kuona misululu ya mashemeji, mamsap n.k. wakipendelewa!mmh?
Unajua huyu mtu kwanza sijui hajui tuuu, au basi ndio kiburi. Kama mzalendo kweli asingejifungia kijijini kwake huko na angetoka na kutoa maelezo kamili ya vitu anavyojua. Maana ni dhahiri kwamba majifungu ya mipesa imebebwa isivyo halali, hivyo basi kuonyesha kwamba anaitakia nchi mema na pia kuonyesha mfano bora kama kiongozi mstaafu angetoa maelezo kamili na kujibu maswali ili upelelezi uendelee, na mishowe tujipatie mafisadi wetu, tuwatupe ndani wapunguze uzito kwenye debe tu,na hiyo ni kama huruma badala ya kutingwa vitanzi!
Lkn ni kwa nini hafanyi hivyo? Inawezekana kweli kwamba washauri wake hawajampatia kidokezo hicho?Swala zima ni wazi kwamba hafanyi hivyo kwa sababu itakuwa ni kama ng'ombe aliyenona kujipeleka mnadani.

Anonymous said...

Ni kweli. Kama angekuwa mzalendo na mkweli na anaitakia nchi mema angetoa maelezo kamili ili upelelezi uendelee na tujipatie mafisadi wetu, tuwatupe ndani wakapunguze uzito kwenye madebe.
Lakini kwa sababu akifanya hivyo atakuwa ni kama ng'ombe aliyenona anayejipeleka mnadabi anaishia kuwadanganya wanakijiji huko kwao.
Kiufupi twampa pole tu na danganya toto zake. Tusubiri tu hawa viongozi "watakatifu" wa nchi watakapoweka woga na aibu pembeni, na kutimiza wajibu wao wakumzoa jamaa toka huko Lupaso, na kumweka kitimoto mpaka atakapotupa full stori.