Monday, 16 June 2008

Uongo wa Mkapa na wa maadui zake upi wa kweli?


Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, hatimaye, hivi karibuni, rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliamua kujitokeza ili ahesabiwe.
Akiwa kijijini kwake ambako alikuwa amepasahau wakati wa utawala wake huko Lupaso, Mkapa alisema wanaomtuhumu kutumia vibaya madaraka, kujipatia na kujilimbikizia mali yeye na mkewe, mwanae, mkamwana, kivyele na marafiki zake ni waongo!
Kauli hii iliyoandamana na nyodo na tambo ikilenga kuwaonyesha watanzania kama wavivu wa kufikiri ilinitibua kiasi cha kupandwa na presha.
Mkapa aliyezoea kuwaita watanzania wavivu wa kufikiri asijue naye ni mtanzania, alijisemea asijue nini itakuwa tafsiri ya maneno yake ambayo wengi wameyachukulia kama uongo na kutapatapa.
Mkapa, bingwa wa kujenga na kubomoa hoja, kipindi hiki alishindwa kuzijenga zaidi ya kuja na hoja zilizombomoa zaidi.
Wengi tulidhani:
-Angeingia kwa undani kwenye shutuma kuwa alijipatia ukwasi mkubwa akiwa madarakani.
-Angeelezea alivyoweza kujenga mahekalu ndani ya miaka kumi kitu kilichomshinda kwenye zaidi ya miaka thelathini aliyokuwa serikalini. Rejea kufichuliwa kwa mahekalu yake ya Mkuzi Lushoto, Sea View na mengine ambayo kadri siku zinavyokwenda yatafichuka.
-Angeongelea ushiriki wa mkewe, mwanae, mkamwana, kivyele na marafiki zake kwenye unyakuzi wa machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira.
-Angeongelea makampuni yake ya ANBEN (vifupisho wa Anna –mkewe na Benjamin).
-Angetoa hata tathmini na ripoti ya utawala wake. Maana aliondoka kimya kimya bila hata kuaga!
Inapofikia mtu mzima tena aliyewahi kuwa kiongozi wa nchi kusema uongo mchana kweupe; akitushinikiza tuuamini uongo wake na kuukataa ‘uongo’ wa wanaosema ukweli, jua ni hatari tena kubwa.
Mkapa bingwa wa salamu ya ‘mambo’ kweli ana mambo tena makubwa!
Ili tusimuonee Mkapa, tuangalie nani anasema uongo na nani anasema ukweli.
Mkapa anasema wanaodai alifuja madaraka ni wale waliokwenda kwake kutafuta upendeleo akawanyima! Mbona kama ni upendeleo, aliufanya. Sema kinachogomba ni kuwapendelea wanafamilia yake na wawekezaji dhidi ya watanzania.
Bila upendeleo mtu kama Daniel Yona angeweza wapi kumilki mgodi wa makaa ya mawe? Bila upendeleo mwanae na mkamwana wake wangewezaje kumilki kampuni la Fosnik (Foster na Nicholas-Mkapa)?
Mkapa anasema wanaomshutumu ni waongo. Huu ni uongo. Mbona wanaomshutumu ni watanzania? Mbona tunaosema hivyo hatumjui Mkapa wala yeye hatujui? Na isitoshe, Mkapa anayeishi kwa hisani ya Kikwete angetoa upendeleo gani kwa mtu ambaye hakuwa karibu naye kama akina Fredrick Sumaye walioishia kuwa muujiza wa miujiza kukaa madarakani mrefu huku wakipwaya?
Mkapa sasa ni mzee. Kuepuka kuwa mtu mzima hovyo, anapaswa kueleza ukweli badala ya kutafuta visingizio. Tumkumbushe. Aliwahi kusema uongo kuwa sera yake ilikuwa uwazi na ukweli ilhali, nyuma ya pazia, ilikuwa kinyume-uongo tena mkubwa.
Mkapa katika utetezi wake ametoka kapa kweli kweli. Mwitikio wa umma juu ya maneno yake umekuwa hasi kiasi cha kutisha.
Tazama kabla ya kuja na utetezi uchwara - kama ambavyo yeye angeuita- aliishazomewa na vijana wadogo kiasi cha serikali kutoa vitisho ikidhani umma utanyamaa!
Chini ya utawala wa Mkapa uongo ulitawala kuliko ukweli. Alitudanganya kuwa uwekezaji ungeleta tija tusijue tija yenyewe ilikuwa kwake na watu wake!
Muulize kwanini serikali ya sasa inafanya majadiliano na wawekezaji kuondoa vipengee vya kijambazi. Muulize, kwa mfano, taifa lilipata faida gani baada ya kuligawa shirika letu la Ndege-Air Tanzania au marehemu Benki ya Biashara-NBC.
Muulize kuna nini pale Tanesco alipoingiza kampuni la kikaburu kwa mtutu wa bunduki. Muulize pale IPTL kuna nini zaidi ya kuwa shimo la kuzamisha pesa ya watanzania huku wakilanguliwa umeme kuliko hata nchi zlizokaa chini ya vita kama Burundi , DRC na Somalia .
Haya ndiyo maswali ya kiutu uzima anayopaswa kujibu Mkapa badala ya kuja na uongo wa kutaka tuamini uongo wake dhidi ya ukweli anaouita uongo.
Siku ya kufa nyani miti huteleza. Mkapa akubali alifanya makosa tena makubwa. Angekuwa safi , nimjuavyo, angewafedhehesha wanaomshutumu badala ya kujifedhehesha mwenyewe.
Kwanini imechukua miaka kujibu ingawa na majibu yenyewe hayana kichwa wala miguu? Mbona aliyemtengeneza, Mwalimu Julius Nyerere aliposhutumiwa na marehemu Oscar Kambona kuwa alikuwa na pesa nyingi nje aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kujibu?
Kwanini Mkapa aende kujibia kijijini kwake? Je alikuwa akiwakimbia waandishi wa habari au kutaka kulifanya suala zima kuwa rahisi na la kisiasa kiasi cha kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu? Kwa mtu makini asingesema ni uongo kimkato. Badala yake angeonyesha uongo ni upi na ukweli ni upi. Je imekuwaje Mkapa tuliyemjua kugeuka mfa maji hivi? Ama kweli asiyejua hajui hajui kuwa hajui na akijua kuwa hajui basi huwa hajui.
Je huu nao siyo ukabila na kuishiwa kimkakati? Hii ni tahadhari kwa rais Jakaya Kikwete kukomesha mchezo huu mchafu. Siku hizi umezuka mtindo wa mafisadi kwenda ‘kujitakasia’ majimboni kwao baada ya kutoa takrima ya misaada uchwara. Kwanini misaada leo na siyo wakati alipokuwa madarakani? Kwali hujafa hujaumbika! Na aliyeko juu mgoje chini huku avumaye baharini papa.
Bahati mbaya kwa watu wetu, kutokana na umaskini wa kutengenezwa na tawala fisadi, wanakubali kutumiwa; kama sindano ambayo hushona nguo nyingi ikabaki uchi! Hata hivyo, hii siyo kinga. Pema ujapo pema ukipema si pema tena na sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.
Sisemi Mkapa anafanya utoto. Lakini kuna haja ya kuacha kufanya utoto kwenye mambo ya kiutu uzima. Mtoto huosha tumbo lake akajiridhisha ameoga mwili mzima.
Kwa ubishi na tabia ya Mkapa angekuwa safi asingeishi kutegemea ulinzi wa Kikwete ambaye ni mdogo kwake kwa kila kitu. Kinachoendelea ni ushahidi tosha kwa Mkapa hakuwajibika. Hata Kikwete ambaye serikali yake inakumbwa na kashfa lukuki asingemlinda kama siyo kuchelea yatakayomkuta baada ya kuachia madaraka kama Mkapa.
Tungetaka Mkapa, mkewe, mwanae, mkamwana, kivyele na rafiki zake waeleze ukweli. Wakane au wakubali.
Au kama Mkapa na wenzake ni safi kama tunavyoongopewa basi wakubali:
Kushitaki wale wanaowashutumu kwa kuwachafulia majina na kuwazulia.
Pili Mkapa awataje hadharani hawa wabaya wake wa kuchongwa.
Akubali kuchunguzwa na matokeo ya uchunguzi yaweke hadharani.
Tuhitimishe kwa kumshauri Mkapa aachane na kutafuta visingizio. Badala yake arudishe mali zetu huenda umma unaweza kumsamehe. Na kama ataendelea na majibu yake yasiyoingia akilini atazidi kuudhi umma kiasi cha kuamua kumshughulikia kwa nguvu zake. Pia azingatie kubadilika kwa alama za nyakati. Zamani wateule walikuwa hawaguswi. Leo wameanza na zomea zomea. Kesho wanaweza kufanya kweli ajikute msambweni kama ilivyotokea Zambia na hivi karibuni itakavyotokea Malawi na hatimaye Tanzania .
Hata Edward Lowassa hakujua wala kuamini angetimuliwa kwa aibu kama ilivyotokea.

Source: Dira ya Tanzania Juni 17, 2008.

No comments: