BAADA ya Waislamu nchini kuhanikiza wakitaka, pamoja na mambo mengine, na kama, sore, mahakama ya kadhi mkuu, nasi wana kijiwe tumeamua kupitisha azimio la kuitaka sirikali iridhie tuanzishe mahakama ya kadhia, sambamba na hii ya kadhi kama itairuhusu.
Tuna sababu nuzuhu na nzuri tu kutaka ianzishwe mahakama hii tukufu ya kadhia ambayo, kimsingi, itaikomboa kaya kutoka kwenye meno na makucha ya majizi wachache wanaotumia vibaya mamlaka.
Kwa ufupi lengo la mahakama hii ni kupambana na dhambi kuu iitwayo ufisadi ambayo mara nyingi inatendwa na mafala wanaojiona wajanja wakati ni mafala tu.
Chini ya mahakama yetu, mafisi na mafisadi wote watavuliwa nguo na kuchapwa bakora kabla ya kunyongwa hadharani ili liwe somo kwa wote wenye mawazo finyu na hulka za kifisi na kifisadi.
Pia chini ya mahakama yetu ya kadhia, atakayezini na akabainika amefanya hivyo, kama atakuwa mwanaume, shurti abakwe na mwanamke azibwe sehemu yake ya dhambi ili asirudie kitendo hiki kichafu.
Mwanamume atapigwa picha akifanyiwa ufirauni huu ili zisambazwe ajulikane alivyo cho…wahalifu wengine tutakaoshughulikia ni wale wanaoghushi vyeti na shahada ili wapate ulaji.
Hawa tutawapofua macho ili wasiweze kuona tena na kwa hiyo waanze kuomba omba badala ya kukiibia kijiwe. Pia tutawakata mkono wa kulia ili wasile tena mali ya umma. Ikumbukwe.
Sisi hatuna magereza. Hivyo adhabu zetu nyingi ni kufagia viungo na kunyotoa roho. Unadhani bila magereza kama tutapendekeza vifungo tutawafungia wapi zaidi ya kuadhirika?
Pia chini ya mahakama hii, tutahalalisha pombe na kupiga marufuku ulevi, hasa ule wa madaraka. Wale wote waliokwisha kukumbwa na ugonjwa wa kulewa madaraka, watafungwa maisha ili kuepusha kuiharibu jamii.
Kwa atakaye kunywa pombe akalewa adhabu yake ni kwamba akiingia peponi baada ya kurudisha namba atakunywa soda na maji baridi tu. Maana atakuwa amefanya kosa kubwa, yaani uchoyo na kuvuka kiwango kilichowekwa cha kunywa kwa ajili ya afya.
Wanaume watapaswa wavae ninja, nao waonje joto ya kuivaa hasa sehemu zenye joto kama vile pwani. Pia tutafanya hivyo ili kina mama wasiwatamani.
Atakayegundulika kutembea bila kuvaa ninja atachapwa bakora hamsini na kupigwa marufuku kutoka nje kwa miaka mitano. Dini yetu inahimiza wanaume wavae ninja ili kuleta usawa na suluhisho baina ya jinsia mbili ambazo zimekuwa zikinyonyana na kutumikishana ukiachia kudhalilishana.
Mahakama yetu inatamka wazi kuwa wanaume wengi ni waongo wa kupindukia. Ni mabingwa wa kutoa ahadi lakini wasitekeleze. Ni mabingwa wa usanii na ujambazi mbuzi.
Wanawaahidi kina mama kuwapeleka Kanani, wanaishia kuwapeleka motoni. Waongo wote watakatwa midomo ya juu ili kila wapitapo wajulikane na wananchi wawaepuke na kutowasikiliza.
Pia chini ya mahakama ya kadhia, itakuwa ruksa kuchanganya dini na siasa. Chini ya mahakama hii, watu wa dini watafanya siasa kwa kujificha nyuma ya majoho yao na wanasiasa watatumia nyumba za ibada kueneza siasa zao.
Katika mahakama ya kadhia, dini na siasa vinachanganyikana na haviwaki kama ambavyo matapeli fulani wamekuwa wakiwatisha wanakijiwe ilhali wao wanavichanganya vitu hivi.
Pia mahakama yetu itatoa tangazo la thamani kwa binadamu. Mwanamke mmoja ana thamani sawa na wanaume watatu. Tulifikia ugunduzi huu baada ya kubaini kuwa wanaume wengi ni mafisadi na mafisi kuliko wanawake na wanadanganywa kirahisi na nyumba zao ndogo kama tulivyoona kwa Kingungo Ngumbaru Mwehu pale Ubungo, Benjaa Makapa na Anibeni, Dadi Balallii, Njaa Kaya anavyotumiwa na Salama Hatari kwa sasa na Anna Mgando na wengine wengi. Hivyo hata kwenye mahakama yetu, ushahidi wa mwanamke utakuwa na nguvu kuliko wa wanaume wawili hata watatu.
Pia wanaume wamegundulika kuwa waharibifu kupindukia. Wanawatelekeza hata watoto ukiachia mbali kuwazalisha ovyo kina mama wanaowakimbia na kuwaachia watoto. Pia uchunguzi wetu umegundua kuwa wanaume wengi hupoteza pesa nyingi kwenye nyama choma, manywaji na nyumba ndogo.
Hivyo kuwakomesha ni kuwatungia sheria ngumu ili kuwaadhibu na kuwadhibiti. Pia chini ya mahakama yetu, wanaume watakuwa wakipeleka watoto kliniki na kuwalisha wawapo nyumbani.
Pia mahakama yetu itahalalisha kiti moto ili kupunguza bei ya nyama ya ng’ombe na kuzidi kuuawa kwa viumbe hawa wasio na hatia. Tutafanya hivyo ili kuangalia kama kweli homa ya nguruwe H1N1 ni hatari. Tutawatumia watu wetu kufanyia majaribio kama wanavyotumiwa na mafisadi wa kiutawala kwa sasa.
Mahakama tukufu ya kadhia pia inatamka wazi kuwa imani asilia ndizo zitoe muongozo wa kuendesha kaya badala ya hizi nyemelezi za kikoloni na kimapokeo. Chini ya mahakama hii, majina yote ya kigeni na kishenzi yatafutwa na dini zote zitaomba radhi kwa umma kwa kutuita washenzi, makafiri na wapagani.
Chini ya mahakama hizi, dini zote nyemelezi na za kimapokeo zitatozwa kodi kubwa kutokana na kuchuma mahali ambapo hazikupanda, hasa kwa njia ya sadaka.
Tutapiga marufuku matangazo ya miujiza ya kiwizi ya kuwaibia wanakijiwe huku tukipiga marufuku makelele ya mahubiri na kuitana kwenda kusali.
Chini ya mahakama ya kadhia, rais atapaswa kuwa mtu asiye na dini yoyote ya kimapokeo isipokuwa ya asilia. Na kaya itaendeshwa kwa sheria za mizimu na mababu.
Chini ya mahakama ya kadhia, wafadhili wote watapaswa kutulipa riba wanapotukopesha maana sisi ni watu wa nchi takatifu tupaswao kufaidi utajiri na matunda ya mataifa ya nchi nyingine.
Pia chini ya mahakama ya kadhia, wakoloni weupe wataruhusiwa kurejea ili kuwaondoa hawa weusi ambao wamethibitisha kuwa wezi, walafu na wenye roho mbaya ukiachia mbali upogo na upofu.
Chini ya mahakama ya kadhia, umri wa kuoa au kuolewa ni miaka 30 ili wahusika wawe wameishaanza kujitegemea na kufundwa. Hakuna cha kuonjana au ‘engagements’ ambazo zimeonekana kuwa kichaka cha umalaya.
Pia chini ya mahakama hii tukufu, watuhumiwa wote wa ufisadi hawataruhusiwa kukaribia nyumba za ibada wala kutoa michango na misaada yao huko.
Pia chini ya mahakama hii, wanasiasa watakaogundulika kuwadanganya wananchi, watakatwa midomo na kufungwa ili wasiendelee kuiharibu jamii.
Sheria ya mahakama ya kadhia itatangaza wazi kuwa Bunge, ikulu na sehemu nyingine za usanii zigeuzwe mabaa ili watakaoingia humo wajulikane ni walevi ambao ulafi wao utawakosesha manywaji huko peponi.
Chini ya mahakama ya kadhia, waheshimiwa wote wanaoutumia uheshimiwa kuwaibia walala njaa wataitwa wadharauliwa na watakaogundulika kuendelea kuwaibia wananchi, adhabu yao itakuwa ni kuvishwa magunia na kutandikwa bakora uchi hadi warejeshe pesa yote waliyolipwa kwa kuhadaa umma.
Chini ya mahakama yetu tukufu, wezi wote walioibia kaya watanyongwa bila kujali kama walikuwa wakubwa au wadogo. Kwa mfano baada ya kupitishwa mahakama hii, wezi wenu wa Kiwira, EPA, Kagoda, Richmond, watauawa kwa kuchomwa moto kama vibaka ili liwe somo kwa wengine wanaopanga kufanya makufuru kama haya.
Pia tutafufua makaburi ya wale waliokufa bila kuadhibiwa na kuzichapa bakora maiti kabla ya kuzizika kwenye mashimo ya taka. Kwa wale waliokimbiziwa nje ya nchi, tutatuma mahakimu wetu wawahukumu huko huko na nchi itakayokataa kushirikiana nasi, basi watu wake watakuwa halali yetu tutakapowateka.
Huu ni mwanzo wa madai. Baada ya kupata mahakama ya kadhia, tutadai na kodi ziendeshwe kwa imani ya dini yetu huku tukihanikiza baadhi ya mambo yapigwe marufuku.
Tutapiga marufuku kuongezeka kwa watu wasio wa dini yetu ya asili. Tutawarejesha kwenye kundi ima kwa pesa, ulaghai hata nguvu ili mradi tuwe na wafuasi wengi tuweze kuitawala kaya na hatimaye dunia nzima.
Chanzo: Tanzania Daima Julai, 29.2009.
2 comments:
Mpayukaji,you have left me speechless. Shime wabongo wenye UBONGO wa kutafakari. KAZI KWENU.
AHSANTE SANA.
Imetuliua ni jokes(ashakum si matusi) full of ujumbe mzito.
Post a Comment