The Chant of Savant

Saturday 21 August 2010

Kikwete anahitaji msaada wa haraka sana





Kwa wanaofuatilia afya na shughuli za rais Jakaya Kikwete, watakubaliana nasi kuwa si mzima kiafya hata kisiasa. Utawala wake licha ya kuzungukwa na aibu na utata ni tatanishi na legelege kama afya na sera vyake.

Alifungua dimba la kuanguka mwaka 2005 alipoanza kampeni za urais awamu ya kwanza, akafuatia mwaka 2009 na akafuatia mwaka huu kwenye ufunguzi wa kampeni zake za lala salama. Hatujui: ataanguka mara ngapi tena toka hapa. Ila ukiangalia ukaribu wa anguko la mwaka jana na mwaka huu, unaweza kutabiri kuwa atazidi kuanguka muda si mrefu toka sasa. Je hii inatokana na afya yake kuzidi kudhoofika kiasi cha kufichua uharibifu uliokwishafanyika mwilini ingawa madaktari, Kikwete mwenyewe hata chama chake hawataki hili lijulikane?

Kwanini afya ya rais wa nchi -ambaye ni public figure- inafanywa siri kama hamna namna? Kikwete anatukumbusha kinachoendelea nchini Misri ambapo rais Hosni Mubarak anaweza kukata roho wakati wowote kutokana na kuzidi kushambuliwa na kansa ingawa mamlaka nchini humo hazitaki kukubali hili.

Hata kiongozi wa PLO, Yasser Arafat, afya yake ilipodhoofika, ukimya na usiri vilitanda kilio kikaja kufichua na kutibua kila kitu. Hata mwizi wa DRC, Joseph Desire Mobutu, na wapambe wake alificha kudhoofu kwa afya yake hadi yalipomkuta yaliyomkuta na akaitema DRC aliyoichukulia kama shamba lake na ukoo wake na waramba viatu wake.

Marehemu Oumaru Yar'Adua, rais wa zamani wa Nigeria, alikufa kwa mateso makubwa baada ya waliomzunguka kumtesa kwa kuficha ukweli kuhusiana na kudhoofu afya yake. Hata hivyo, uongo huu wa kujidanganya-self deception haukufua dafu kwa kanuni ya maumbile. Mauti yalimfika Yar'Adua na walioficha ukweli wakaumbuka. Je kwanini hatutaki kujifunza kutokana na ukweli huu wa kihistoria? Je tu majuha na wapuuzi kiasi hiki!

Je Kikwete ni mzima kweli kwa maana halisi ya neno? Swali hili muhimu linachanganya sana ingawa unaweza kutumia ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) kupata jibu. Angekuwa mzima, asingeogopa kupima afya yake na kuweka wazi matokeo kabla ya kugombea. Kuna vitu viwili Kikwete hatafanya na hataki akumbushwe kufanya-kupima afya yake na kutaja mali zake.

Hili pia lingemfaa hata mgombea mwenza Dk Gharib Bilal ambaye naye minong'ono imeshaanza kusikika kuwa afya yake si mulua.

Leo tutatoa ushauri wa bure. Kikwete bingwa wa kumtegemea mtabiri wake Shehe Yahya Hussein, anapaswa kurudi kwake na kukubali amwambie ukweli ambao alimpa kinyume pale alipotabiri kuwa atakayempinga atakufa. Je alimaanisha vinginevyo kutokana na lugha zao za sanaa kama ambayo Kikwete aliahidi maisha bora akimaanisha maisha balaa? Maswali ni mengi kuliko majibu. Kilicho wazi, hata hivyo, ni kwamba afya ya Kikwete ni ugogoro mtupu hata ifanywe fumbo vipi. Hata ndege wanajua hili fika.

Je hii inaweza kufumbua fumbo ni kwanini Kikwete hupenda ziara za nje? Ndiyo. Wengi wanadhani huenda kule kutibiwa kisirisiri. Kuondoa utata na imani kama hizi, kuna haja ya Kikwete kupimwa afya yake na matokeo yake kuwekwa hadharani. Vinginevyo mengi yatasemwa hasa yasiyopendeza ukiachia mbali wasi wasi juu ya mshikamano wa taifa.

Somo jingine la Kikwete kama watanzania wataweka maanani ni ishara ya kuanguka kwenye kura kama wizi wa kura hautavumiliwa. Maana, kimsingi, Kikwete hajakidhi matakwa ya watanzania wala kufanya lolote zaidi ya kuwa balaa. Angalia muungano unavyozidi kubomokea mikononi mwake chini ya uongo uitwao maridhiano ambayo kimisngi ni janja ya wazanzibari kurejesha taifa lao kwa mlango wa nyuma. Angalia mafisadi wanavyozidi kuiteka serikali huku wanaowapinga wanapatilizwa kama ilivyotokea kwa Lucas Selelii na Thomas Nyimbo na wengine. Rejea kupeta kwa Rostam Aziz, Edward Lowassa, Andrew Chenge na wengine ambao, kimsingi, ndiyo mihimili ya Kikwete ya ufisadi unaoendesha serikali yake.

Tuombe Mungu atufumbulie fumbo hili. Tumuombe sana afichue hii siri ya afya na sera zenye ugogoro.

Tunachukua fursa hii kumtakia Kikwete apate nafuu mapema. Muhimu, tunamuomba akubaliane na ukweli kuwa ukweli huwa haukimbiwi wala hauwezi kuuawa hata ukicheleweshwa vipi.

Penye kufuka moshi shurti kuwa na moto na mwanzo wa ngoma lele. Kuna siku mtakumbuka ujumbe huu na siku si nyingi. Katika kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI tukio kama hili limeonyeshwa vizuri pale mkuu wa mkoa wa Chelewa Gibbons Likupatile (Kikwete) linapompata na kuanguka na kuzimia jukwaani alipokuwa akijaribu kuwaongopea wananchi wa Mizengwe (Tanzania) kabla ya serikali fisadi ya Mizengwe kuangushwa kutokana na harakati takatifu zilizoasisiwa na kuratibiwa na mkongwe wa ukombozi Mzee Njema Waithaka mhusika mkuu wa riwaya ya SAA YA UKOMBOZI.

Tusiseme mengi. Soma utafahamu mengi.
Yetu macho. Kikwete, hata CCM, wanahitaji msaada na si kutoka kwa Shehe Yahya au mitandao ya kijambazi ya CCM bali watu wenye ithibati na ujasiri kumwambia apumzike. Uzuri ni kwamba hila zao zimegundulika. Si Kikwete wala Yahya. Wanadanganyana na kutumiana. Hakuna anayempenda wala kumsadia mwenzake zaidi ya kudharauliana na kuchuuzana. Angalau hili limejulikana. Enough is enough tuseme na wakiri. Kwani, tuendako, ataumbuka bure.

Hebu angalia wapuuzi wanavyoanza kuondoa picha ya tukio kwenye mitandao wakidhani wataficha ukweli. Ukweli haufichwi milele bali kwa kitambo tena kidogo. Ajabu wakati wakifanya haya wanasahau kuwa maneno ya mwisho ya Kikwete kabla ya kuanguka ilikuwa ni tambo kuwa ameimarisha uhuru na haki za binadamu hasa vyombo vya habari na haki ya kupokea na kutoa habari. Kuhujumu links zenye picha hii si kufichuka kwa unafiki wa kilichokuwa kikisemwa hadi Kikwete kujisifia? Au ni yale yale kuwa Kikwete akisema hili humaanisha lile?

Tulipata habari za kuanguka kwa Kikwete kupitia UGHAIBUNI ya Evarist Chahali na Jamii Forums. Lakini baada ya muda mfupi picha ya tukio iliondolewa kwenye mitandao. Tunadhani hii ni hujuma. Si utashi na mapenzi ya walioiweka ili ulimwengu ujue ukweli. Hata hivyo walikosea. Maana ukweli ulishasambaa na kujulikana.


HAKIKA, KIKWETE NA WALIOMZUNGUKA NA KUMZUGA WANAHITAJI MSAADA WA HARAKA. Mungu wakomboe watanzania.

3 comments:

Anonymous said...

Kudos mkuu kwa uchambuzi uliokwenda shule. Lazima ukweli usemwe hata kama unauma. Huyu jamaa aisee ni balaa hafai heri aumbuke.

Anonymous said...

Sasa isije ikawa ana matatizo ya kiakili. Ni kifafa? Ni mtindio wa ubongo? Ni nini?

Isije ikawa tunaongozwa na KICHAA!!!

Mola Atusaidie jamani. Au tu alisahau kunywa dawa za kuongeza nguvu (VVU)???

Anonymous said...

Asante Mzee Mpayukaji. Huu ndiyo uandishi tunaoutaka usiohofia kitu au kujikomba. Kikwete ana matatizo na anahitaji msaada tena haraka kama ulivosema. Sijui madaktari wake sasa watatwambia nini
Mungu tuondolee habithi huyu kama ulivyofanya kwa Ditopile.
Nasikia Kikwete na Rweyemamu ni waathrika wa muda mrefu.