The Chant of Savant

Thursday 5 August 2010

Kaya imepoteza maadili, imebaki na madili

BAADA ya walevi kubamizwa mkenge kwa miaka yapata five, ngwe nyingine ya kuwakaanga zaidi inakaribia kuanza. Zama zile waliahidiwa maisha bora. Mara yakafanya mutation yakageuka bora maisha. Hatujakaa sawa yakazidi ku-mutate. Sasa si maisha bora tena wala bora maisha bali maisha karaha!

Kutoka hapa kama siyo kudedishwa basi kitakuja kitu kipya yaani maisha balaa.

Ajabu ya maajabu, sijui ni kutokana na ulevi au utaahira? Sijui na kweli sijui. Walevi wanaendelea kuaminishwa kuwa maisha balaa yanaweza kuwa bora wasijue baada ya maisha balaa kifuatacho ni mauti hata kama wafao hawazikwi.

Huwezi kuwa na watu unaoweza kuwaita zobab dhakar kwa Kiarabu au tuseme nzi dume ambaye huchafua kila jike, ukategemea kupata maisha bora. Watakuchafua kama walivyokuchafua mwongo uliopita.

Hata hivyo tusiandikie mate ilhali kidau kimeishafurishwa wino. Kuingia kwa daktari Silaha kwenye nyang'anyiro hili kidogo kunaweza kuonyesha njia. Ila kwa vile walevi ni walevi wanaweza wasimpe tafu ili kuondoa hiki kiwingu ambacho kimesababishwa na mafisi na mafisadi twawala.

Leo mzee mzima siongelei habari za kijiwe changu tu bali hata kaya kwa ujumla ili kutoa tathmini itakayowasaidia wapika kula waamue nani wa kupiga kibuti.

Nshasema. Mungu awape nini walevi! Kuja kwa daktari Silaha ambaye ni silaha ya kweli dhidi ya ufisi na ufisidunia, kama walevi watatumia lau common sense, kwaweza kuwa ukombozi.

Wazungu husema no research no right to speak yaani kama hukufanya utafiti huna haki ya kupayuka. Acha mzee mzima nimwage tathmini kwa statistics za maneno si figures maana figures zinaboa au siyo. Nimeongea umombo ili msijesema nami nilighushi shahada zangu za udaktari na uchungaji.

Katika kipindi cha miaka five iliyopita ujambawazi iwe wa mibunduki au mikalamu ulizidi sana hadi profesa mwenzangu Jwani Mwaikusa akadedishwa. Kwanza ngoja ninyamaze kidogo nilie kwa heshima na kumbukumbu yake.

Hapa sijaongelea ujambazi wa kupandisha bei za bidhaa kutokana na lisirikali kuchezea uchumi hadi pesa ya madafu inaporomoka hadi watu wanatumia midola badala ya mikwenje.

Wakati ujambazi huu ukitamalaki, ukosefu wa ajira ndiyo usiseme. Bila kuwa na mtu unayemjua au kutoa rushwa hasa kwa kina mama ile ya ngono hakuna kibarua. Ukienda kwa magabacholi nako unyanyasaji ndiyo usiseme.

Wakati huo huo bado wasanii fulani wanakwambia hayo ndiyo maisha bora! Ukikosa kazi, maisha bora! Ukishinda kwenye misongamano barabarani, maisha bora! Maisha bora au maisha balaa? Nani anamdanganya nani hapa? Zindukeni basi mfanye kweli angalau msimu huu.

Hili la ukosefu wa ajira huwa linapandisha hasira zangu nikikumbuka jinsi wanene wa wafanywakazi walivyowasaliti na kulala kitanda kimoja na watesi wao li-sirikalini. Hapa bado hujagusa kupunjwa masihara iitwayo mishahara.

Wakati haya yakiendelea biashara ya bwimbi ndiyo usiseme. Mateja yanazidi kuongezeka kiasi cha kutisha hasa mtaani kwangu pale kwa Mfugambwa Manzese. Ukijitia kupambana na bwimbwi wanakugeuza bwimbwi.

Ubabaishaji nao ndiyo usiseme! Mijitu inaiba kula na kughushi vyeti inajiita midokta wakati ni vihiyo watupu lakini bado inapeta kwenye ofisi za ulaji za umma zilizogeuzwa vijiwe! Kaya sasa is going to dogs!

Nije kwenye hili la wanene kuhonga waliwa kwa upuuzi mdogo kama mishiko mashati khanga na upuuzi mwingine. Hamkumsikia yule mwakilishi wa mkuu wa kaya alivyobabwa akigawa noti kama hana akili nzuri? Hayo ndiyo ma-life bora kwa wote. Wewe umo? Shauri yako unaliwa ukiambiwa unakuja juu umetukanwa!

Juzi nilipanda gari tena la mnene. Unajua ilikuwaje? Lilimgomea mnene kutokana na kugoma kunyweshwa mafuta yaliyochakachuliwa na hakuna anayestuka! Ngoja sasa na ile njiwa ya mkuu inyweshwe haya madude muone. Msiniulize wala kusema sikusema mie nabii wa Mungu.

Bila kurekebisha hili tutakuja kutupiana mimawe kama kule kwa akina Mwaka na twambombo halafu muanze kulalamika eti tunatishia amani na mshikamano wenu wa ulaji wa kula bila kunawa.

Maisha usipime. Yamegeuka balaa hadi akina Lyatongolwa kujigeuza Kijagazi wa Njaa Kaya ili kuganga njaa. Kwenye siasa usipime. Hamjaona jinsi kwa Chama Cha Jeuri kilivyonyongwa na jamaa yangu Joni wa Kutu-Tenda?

Nani anajali wakati tunaambiwa hii ndiyo demokrasia ghasia ya wanene kuwala wadogo? Hamjaona wakubwa wanavyoghushi vyeti na kuendelea kutesa huku mnaoambiwa ofisi wanazofuja ni zetu mkizidi kuteseka?

Nasisitiza. Bila kuwapiga teke hawa wahalifu tukubaliane. Kaya itaendelea kuwa shamba la bibi nanyi mtaendelea kuliwa kama migebuka pale Kazuramimba na Buzebazeba.

Nashangaa ile tume ya kukuza na kupuuza rushwa inavyowakamata wanaotoa mshiko tu huku ikiendelea kuwaminyia hawa vihiyo! Sipendi taasisi inayofanya kazi kibaguzi na kipuuzi. Sasa ndiyo nini kushika wale ukawaacha wale waendelee kula?

Itakuwa ni kufanya ufisadi kama nitamaliza tathmini hii ya kisomi bila kutaja kukua kwa tatizo la uchafuzi wa mazingira na maadili. Kwa sasa kaya haina maadili bali madili. Mazingara yamepanda chati kuliko mazingira. Anayebisha aende Bwagamoyo aone matapeli wa tunguli na makombe wanavyovuna noti. Kama bado hujaamini nenda kwa yule tapeli wa nyota.

Hakuna sarafu yenye upande mmoja bali mbili. Kadhalika katika maisha haya balaa, kulikuwa na maisha bora. Hujasikia? Kufa kufaana. Hata kula kulana. Habari nzuri ni kwamba wakati wanakaya wakinyotoka roho kwa umaskini, wanene na vitegemezi vyao walizidi kunawiri na kufungua mikanda ili kubukanya zaidi.

Anayedhani hii ni chuki au uongo basi awaangalie walioko kwenye maulaji hasa mkuu na bi mkubwa hata vitegemezi vyao. Wote ni mashavu nhinhaa. Unacheza na ulaji wa dezo nini?

Naona TAKUKURU wanakuja. Acha nitimke kabla hawajaninyaka kutokana na mpango wangu wa kwenda kuwahonga vijisenti na vijisimu walevi ili wanichague.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 4, 2010.

No comments: