How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Tuesday, 10 August 2010
Tumtawaze Kikwete Mfalme Wetu
SINA haja ya kumsakama Rais Jakaya Kikwete na waliomzunguka. Naandika makala hii kwa nia ya kumtahadharisha juu ya staili yake ya kutawala kwa faida yake.
Nalalamikia mchezo mchafu unaoanza kuzoeleka ambapo wake na watoto wa wakubwa wanatumia nyadhifa za wakubwa kujineemesha kifedha na kisiasa.
Hivi karibuni yametokea malalamiko dhidi ya watoto maswahiba wa vigogo wawili wa chama na serikali, yaani Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambapo watoto wao Ridhiwan Kikwete na Januari Makamba wametajwa wazi wazi kuwa nyuma ya shinikizo lililosababisha kuachia ngazi mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Hamad Yusuf Masauni kwa tuhuma za kughushi vyeti vya kuzaliwa. Hatuna utetezi na hili ingawa linatia shaka kwa nini achaguliwe kwanza bila kuliona hili?
Januari pia analalamikiwa na Mbunge wa Bumbuli William Shellukindo kwa kuanza kampeni za ubunge mapema akitumia wadhifa wa baba yake.
Pamoja na shutuma hizi kutolewa dhidi ya wawili hawa si Kikwete wala Makamba hata CCM wamejitokeza kutoa maelezo au karipio!
Hapo juu nimeeleza kuwa Kikwete atawazwe kuwa mfalme wetu wa kwanza. Ukiangalia utawala wake wa kishikaji anavyouendesha, utakubaliana nami kuwa kuna tatizo kubwa tu.
Hebu piga picha juu ya unavyomuona mkewe Salma kwenye shughuli mbali mbali sehemu mbali mbali anavyopokelewa kama kiongozi wa nchi. Kwa nini anapokelewa hivyo? Simpo. Ni mke wa rais.
Salma amekuwa na nguvu kuliko hata baadhi ya mawaziri. Anaongozana na misururu mirefu ya magari na kupokelewa kwa mbwembwe zote za kikubwa utadhani ana ukubwa wowote Kikatiba!
Hapa hatujaongelea asasi yake isiyo ya kiserikali japo inaendeshwa kiserikali aliyoianzisha pindi tu mumewe alipoingia Ikulu ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Wengi wenye akili tulidhani Kikwete hata Salma wangejifunza kutokana na madudu yaliyofanywa na mtangulizi wake Anna Mkapa anayetuhumiwa kujineemesha kwa mgongo wa Ikulu akitumia asasi yake ya EOTF.
Swali ambalo huwa linajirudia vichwani mwa wachambuzi ni kwa nini aanzishe asasi baada ya mumewe kuwa rais kama kweli analenga kufanya anayofanya kwa nia safi?
Nani anajua ripoti ya ukaguzi ya mahesabu ya asasi husika ukiachia mbali kuendeshwa na mtu mmoja kisiasa hasa kumpigia kampeni mumewe?
Isije kuonekana tunamsakama Kikwete na mkewe. Nitajie asasi ya Hilary Clinton alipokuwa mke wa rais au ya Michelle Obama mke wa sasa wa rais wa Marekani. Hazipo. Hawana haja ya kujidhalilisha na tawala za waume zao kujiingiza kwenye biashara ya ubuyu.
Nionyeshe ofisi ambayo amewahi kugombea Chelsea Clinton. Hakuna. Kwake mapambano ya maisha ni suala binafsi linalopaswa kufanyika kwa uhuru na si utegemezi.
Leo Salma, Ridhiwan na Khalfan wamo kwenye safu za juu za CCM na Chipukizi ukiachia mbali wadogo zake Yusuf na Mohamed waliokuwa kwenye orodha ya wagombea wa uwakilish@ � ��� ?��
Kinachotia shaka hapa ni kuvunjika kwa maadili ya demokrasia. Maana hawa wanaobebwa na pakacha la Ikulu hawaoni hata aibu kudhalilika kwa kutegemea migongo ya wazazi au waume zao.
Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC) pamoja na uroho wake hakuwapa ulaji watoto wake chamani na serikalini zaidi ya kuwaruhusu wadokoe kwenye hazina za nchi zao.
Sikusikia wake zao wakiwa na asasi za ulaji wala kupenda kufanya shughuli za kisiasa.
Niliwahi kushauri Kikwete afanye kama imla wa Uganda Yoweri Museveni.
Amteue mkewe waziri na kumpa kitengo cha ulinzi hata ushauri mwanae. Akiwapa nafasi hizi angalau tutakuwa na jinsi ya kuwapima hata kutaka wawajibishwe kwa vile tunajua mamlaka ziliwateua.
Lakini kwa sasa inakuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na kuwa na mamlaka yasiyo ya kikatiba.
Hivi kweli ilihitaji PhD Kwa Kikwete kujua kuwa kumteua Januari kuwa msaidizi wake kungeleta mgongano si wa kimaslahi ukiachia mbali kujuana?
Sasa kama rais hawezi kuona hili bado ana chembe ya udhu kustahiki kurejea tena Ikulu? Ili afanye nini kwenye ngwe ya lala salama zaidi ya kusimika ufalme wake na familia yake na ulaji wa lala salama?
Hapa hatujagusia marafiki tena wenye kila tuhuma za uoza. Alipomteua swahiba na muwezeshaji wake mkuu Edward Lowassa ambaye baadaye alikuja kumtoa sadaka kunusuru ufalme wake uliokuwa umefanya kufuru, wenye akili tulijua ufalme tuliohofiwa unawadia.
Mna habari kama Lowassa angegoma kujiuzulu angekuwa bado ni Waziri Mkuu?
Hapa hujagusa watu wanaotuhumiwa kuwa nyuma ya wizi wa mabilioni toka kwenye Benki Kuu wakitumia makampuni mengi hewa.
Ukitaka kuliona hili vizuri jikumbushe jinsi rais alivyomuokoa rafiki yake marehemu Ditopile Mzuzuri alipomuua mtu kabla ya mkono wa Mungu kuingilia kati.
Kumbuka, hapa hatujagusia ufisadi unaofanywa na walio karibu na mfalme ukiachia mbali serikali yake kusifika kwa matumizi mabaya ya pesa ya umma huku mfalme akiitalii dunia na mke wake.
Je kwanini ufalme wa Kikwete unazidi kudumu na kufanikiwa? Simpo: woga na mazoea mabaya ya kifisadi wa kimfumo wa Watanzania ambao wanaweza kubeba kila mzigo bila kunung’unika.
Huu ni upunda na umkokoteni na upakacha ambavyo huwa haviulizi aina ya mzigo viubebao. Je hali itaendelea kuwa hivi? Ni mawili. Tumtose au kumtawaza Kikwete mfalme wetu wa kwanza kama tutashindwa kumngo’a kwenye uchaguzi huu aliopanga kununua kwa bilioni hamsini.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 10, 2010.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment