How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 5 August 2010

Tumebaki na siasa za uchakachuaji




CHAMA chochote cha siasa kikibinafsishwa na wafanyabiashara na kikajivua jukumu la ukombozi lililolengwa na waasisi wake, basi hugeuka kuwa moja wa maadui wa wananchi.

Ndivyo kilivyotokea kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hakina tena mwelekeo wa uongozi. Kimsingi kimefisidika. Katika mazingira haya, uchaguzi ama huwa uchakachuaji au uchafuzi wa demokrasia.

Nasema hivi kutokana na uchakachuaji, kama ufisadi, kuanza kuwa sera rasmi ya CCM.

Rejea serikali kushindwa hata kuadabisha wanaojulikana kuchakachua mafuta hadi magari ya ikulu yananyweshwa mafuta machafu.

Hii ni kutokana na kupeana ulaji na tenda kwa misingi ya kujuana, ukiachia mbali kunyima na hivyo kuhujumu taasisi za umma za kushughulikia huduma hizo.

Jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Ndio mtindo wa Rais Jakaya Kikwete na chama chake kuchangiwa shilingi bilioni 50 eti kwa ajili ya uchaguzi.

Fedha zote hizi za nini, kwa mgombea anayemaliza muhula wake wa mwisho, kama siyo za kuwahongea wananchi waliofanywa maskini na serikali hiihii ambayo bado inawachangisha pesa.

Hapa hujaongelea matumizi mabaya ya mali za umma kama vile magari, ndege na hata fedha taslimu – kulipana posho wakati rais akijinadi kwa kisingizio cha kukagua miradi ya maendeleo.

Jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Kama rais anaweza kuchangisha shilingi bilioni 50, safi na chafu, kwa ajili ya 'kushinda', kwanini wabunge nao wasitenge vibilioni vyao walivyovuna kwa kuwauza wananchi kwa wawekezaji na matapeli wengine wa kiuchumi ingawa si wote?

Je, huu si uchakachuaji wa haki? Ukitaka kujua nimaanishacho, rejea kukamatwa kwa kadi bandia ambazo zinalenga, bila shaka kuwachakachua (kurudufu idadi ya wanachama) ili kupata maruhani na misukule ya kupiga kura.

Na huu ni utaratibu uliozoeleka hasa ikizingatiwa kuwa serikali imekuwa ikilipa mabilioni ya shilingi kwa wafanyakazi hewa bila kuchukua hatua, ilhali watu wetu wanazidi kuwa mafukara.

Leo hii tunajua hata thamani ya kura ya Mtanzania. Tunajua kuwa shilingi bilioni 50 ni bei ya jalada ya urais. Je, ubunge nao ni kiasi gani – vinokia, vitenge, fulana, pilau, ulevi?

Chini ya siasa za uchakachuaji CCM imegawanyika sana ingawa kwa juujuu tunaonyeshwa chama kilichoshikamana.

Kuna mitandao hasidi kama ile dhidi ya Samuel Sitta. Rejea kugunduliwa njama za kutaka kuwahujumu “makamanda wa vita dhidi ya ufisadi” kama Dk. Harrison Mwakyembe, Sitta, Lucas Selelii na wengine.

Angalia kutochukuliwa hatua kwa watuhumiwa wa ufisadi mkubwa serikalini; kwa mfano walioshiriki katika ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kuto Benki Kuu (BoT).

Chunga kimya kilichopo juu ya ujambazi wa kuchefua uliofanywa na makampuni kama vile Kagoda, Deep Green Finance na wengine, ambapo vinara wake ni wagombea tena wanaopigiwa upatu na wazito wa chama kama Katibu mkuu Yusuf Makamba.

Rejea kitendo cha waziri mkuu Mizengo Pinda na Makamba kumuomba mbunge wa Igunga, Rostam Aziz aliyetuhumiwa kuwa nyuma ya Kagoda kuendelea kugombea wakati ana mawaa.

Pinda alikaririwa hapo Mei mwaka huu akisema, “Rostam kama wewe ulijiona huna uwezo wenzako wameona...kauli ya wengi ni ya Mungu.”

Makamba alisema ameacha shughuli zake nyingi ili aende Igunga … kwa kutambua mchango wa Rostam kwenye chama cha CCM na uongozi mzuri jimboni kwake, ndiyo maana nimekuja.”

Ajabu, licha ya kuwa na wala na watoa rushwa wanaochakachua haki zetu, utakuta wengine ama ni wale waliotuhumiwa kwenye kashfa nzito za uhujumu wa taifa au walioghushi vyeti.

Anayepinga kuwa hawana ridhaa ya CCM na CCM haina sera ya uchakachuaji ajiulize ni kwanini serikali yake haiwachukulii hatua za kisheria.

Waingereza husema, “Show me your friend I will tell you who you are” – nionyeshe rafiki yako nitakueleza wewe ni mtu wa aina gani.

Wananchi wanapaswa kuvunja ndoa hii haramu na hatari ya wafanyabiashara wezi na CCM.

Je, unawezaje kuwa na uchaguzi huru na haki bila tume huru ya uchaguzi kama si uchakachuaji hata uchafuzi?, CCM inapenda na kulinda Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC).

Ukiangalia jinsi CCM inavyojivua jukumu la ukombozi na kujiingiza kwenye uchakachuaji, kuna kipindi unaweza kudhani wale wote waliokamatwa kwa kutoa rushwa wameonewa kutokana na mtandao waliomo.

Maana kwa mazingira ya sasa, inawezekana asipatikane hata mbunge mmoja wa CCM wa kurejea bila kutoa rushwa.

Rejea maneno ambayo hayakukanushwa na chama wala wabunge ya mbunge aliyeamua kustaafu kwa madai kuwa amechoshwa na kuombwa rushwa, Chrisant Mzindakaya.

Vilevile, kwa historia ya utendaji, CCM na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni kitu kimoja. TAKUKURU haiminiki na si huru (none bias); na hili lilionekana vema wakati wa kashfa ya Richmond.

Je, wale waliotaka kuitumia TAKUKURU kipindi kile, hawaitumii kwa sasa kulipiza visasi, ikichukuliwa kuwa ni vinara wa mtandao unaodaiwa kuundwa na wale wanaotuhumiwa ufisadi dhidi ya wale wanaopambana nao?

Katika mazingira haya, hata TAKUKURU ikimkamata rais, haiwezi kurejesha heshima na imani yake kwa umma. Dawa ni kuoindoa chini ya rais na kuifanya kuwa tume huru sambamba na tume huru ya uchaguzi.

Uchakachuaji ni balaa na huua nyoyo. Mkuu wa wilaya au waziri mzima anakamatwa kwa kutoa rushwa, lakini si serikali wala chama, kinatoa tamko la angalau kukaripia.

Je, hapa kuna kusonga mbele kwa mwananchi wa kawaida mbebeshwa mizigo kama punda kihongwe?

Huu ni msimu wa uchaguzi. Kitu muhimu kwa wapigakura ni kukiadhibu CCM kwa kuwauza na kuwasaliti ukiachia mbali kuwatelekeza. Hili liwe somo kwa wengine tunaoweza kuwakasimisha madaraka hapo baadaye.

Hakika umefika wakati wa kuzika siasa za uchakachuaji za CCM.
Chanzo: MwanaHALISI Agost 5, 2010.

No comments: