Kabla ya kuingia undani wa kile nitakachokiandika, nachukua fursa hii kuwapongeza wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuchagua kuwa na serikali ya mseto au ya umoja wa kitaifa hapo Agosti mosi. Kwa matokeo yaliyotoa kibali kuanzishwa serikali hii, si ufanisi kwa zanzibar tu bali hata bara. Wameonyesha njia na uvumilivu na mapambano yasiyoshindwa vya muda mrefu.
Tukirejea kwenye ujumbe wa leo, japo mie si mtabiri, kama tutasimama imara dhidi ya wizi wa kura na unyanyasaji wapiga kura inapotokea kutaka kuzuia wizi, natabiri tutakuwa na serikali mseto au ya umoja wa kitaifa hivi karibuni.
Ukiangalia kuingia kwa silaha ya moto yaani Dk Wilbrod Slaa kwenye mbio za urais zilizokuwa zimeanza kuchosha kutokana na kutawaliwa na ving'ang'anizi walioshindwa mara nyingi huko nyuma, kuja wa Slaa si bure. Licha ya kutoa mbadala, kunaleta kitu kipya ambacho watanzania wanakihitaji-ukweli katika kupambana na ufisadi.
Chama Cha Mapinduzi kinaweza kujigamba kuwa na kila kitu. Ieleweke. Kinakosa kitu kimoja ambacho CHADEMA wanacho-kufanya kazi kwa vitendo badala ya maneno kama CCM. Uko wapi utekelezaji wa ahadi alizotoa rais anayemaliza muda wake na mgombea na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete? Hakutimiza hata moja. Heri angekiri kama mtangulizi wake Benjamin Mkapa kuwa sera za CCM hazitekelezeki. Je tunahitaji sera zisizotekelezeka ukiachia mbali watu wasio na uwezo wala visheni ya twende wapi kama ilivyojidhihirisha kwenye kipindi kinachoisha?
Kabla ya kudodosa zaidi, naomba niwarejeshe wasomaji wangu kwenye wizi wa kura ulifanywa mwaka 1995 ambapo kwa utafiti wa haraka tokana na kuhoji watu kwenye mikoa ya kati niligundua kuwa mgombea wa NCCR-Mageuzi wakati ule alikuwa ameshinda kutokana na kupmbanishwa na mtu ambaye hakuwa akijulikana wala kuijua nchi. Hivyo CCM waliweka wakachukua wakamtangaza mtu wao.
Kuondokana na hili, mwaka huu tuhakikishe hatukubali kufanyia uhuni huu. Tukisimama imara inalipa. Rejea kilichotokea nchini Zimbabwe na baadaye Kenya na sasa Zanzibar. Kwanini nasi tusisimame tukatetea haki zetu?
Nchini Zimbabwe, pamoja na ukandamizaji mkubwa wa imla Robert Mugabe, MDC walisimama hata kwa kuteswa hadi nchi ikawa haitawaliki kiasi cha Mugabe kulamba matapishi yake sawa na CCM ilivyofanya visiwani. Hivyo basi, matumizi ya mtutu wa bunduki na bandali za pesa hakuwezi kuua dhamira ya kujikomboa ya binadamu anapodhamiria. Nani amesahau mauaji ya mwaka 2001 na mengine yaliyofuatia visiwani lakini bado ithibati ya wazanzibar ikazidi kudhihiri kiasi cha kuiacha CCM ikiwa haina nguo wala la kufanya zaidi ya kufakamia matapishi yake?
Kitendo cha serikali ya CCM kuridhia serikali ya mseto licha ya kuonyesha kuishiwa na kuvuliwa nguo, ni ushahidi kuwa si jasiri kama tunavyoaminishwa. Pia ni ushahidi wa wazi kuwa wanaosema CCM itatawala milele wana matatizo ya akili. Itatawalaje milele wakati kwa upande wa visiwani imeishakwanyuliwa na kunyolewa bila maji?
Kama watanzania tutaacha ujinga na ukondoo na umshumaa, mwaka huu CCM inaweza kupigika pande zote yaani bara na visiwani kutokana na kuwa na wagombea wenye ushwishi mkubwa na rekodi safi dhidi ya wababaishaji na wenye rekodi chafu wa CCM.
Hatuzushi. Kikwete ametekeleza lipi kuhusiana na kupambana na ufisadi hasa ule wa EPA, Richmond, CIS, kuporwa nyumba za umma, kushughulikia wala rushwa, wauza mihadarati, majambazi na wengine ambao Kikwete alikiri kuwa na orodha zao. Muulize amezuiliwa na nani au nini kuwashughulikia? Muulize ahadi zake za maisha bora zimeishiwa wapi? Je kuna maisha bora au uchuro mtupu? Kama atatoa jibu hata moja, basi huna hata sababu ya kupoteza kura yako kuchagua kitu kile kile kilichozidi kukuzamisha kule kule kwenye matatizo na adhabu za umaskini na ukosefu wa kile ulichoahidiwa hadi ukatoa kura yako.
Hakuna haja ya watanzania kuendelea kushikiliwa na genge la mafisadi. Kuna mbadala muhula huu na mbadala huu ni Dk Slaa.
Iwapo watanzania wataamka kitandani walimolala na utawala mchafu na kuupiga chini, basi hawatakuwa tayari kuletawa matokeo ya uchaguzi ya kupikwa ima na tume ya uchaguzi au serikali iliyoiteua ili kuitumia kufua nepi zake. Watasimama imara na kuwa tayari kwa lolote wakijua mwisho wa siku watashinda. Tumeona mifano michache hapo juu ya watu wenye miili midogo lakini mioyo mikubwa walioangusha vigogo na mibuyu tena katili na vichaa kama Zimbabwe. Hata Afrika Kusini haikufikia ilipo kwa lelemama wala mteremko bali kusimama kidete na kupinga jinai ya ubaguzi iliyokuwa ikiumiza sawa na ufisadi.
Kuna haja ya kutumia fursa hii hasa kipindi hiki ambapo CCM licha ya kumeguka na kudhoofika, imeanza kuufyata kama ilivyotokea Zanzibar. CCM kipindi hiki haiwezi kuamrisha serikali yake itumie mtutu kwa kuhofia wakuu wake kujikuta korokoroni huko The Hague. Na hii si propaganda. Ni ukweli kuwa kwa sasa hata madikteta wanaoogopewa kama Yoweri Museveni, Paul Kagame na wengine wamebadili mwelekeo. Badala ya kutumia majeshi na tume feki za uchaguzi kama Tanzania, wanawanyamazisha au kuwaua hata kuwasababisha wapinzani ambao ni tishio kuozea magerezani kama ilivyo sasa kwa Victoire Ingabile huko Rwanda au kuwaua kama ilivyotokea kwa James Kazini Uganda na Andre Kagwa Rwisereka huko Rwanda au Asumani Nzeyimana huko Burundi. Wengine hutishia kuwakamata kiasi cha kukimbia nchi kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Burundi ambapo kiongozi wa upinzani Agaton Rwasa alilazimika kuikimbia nchi ili kuokoa maisha yake.
Huu ni ushahidi kuwa kama umma wa wapiga kura utakataa kuibiwa kura zake hakuna nafasi tena ya kutumia ubabe wa polisi na wanajeshi kama ilivyokuwa ikifanyika uko visiwani.
Hivyo nimalize kwa kuwahimiza watanzania hasa upande wa bara kujiandaa kuingiza serikali ya mseto ambayo baadaye itaondoa huu uoza uliopo.
Kula pesa toka CCM. Lakini kura piga kwa CHADEMA. Mwaka huu tuchague maendeleo na mabadiliko si ukale uoza na mazoea.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 9, 2010.
No comments:
Post a Comment