The Chant of Savant

Thursday 7 July 2011

Ni ujinga kuruhusu posho za makalio


SIKU hizi narapu kuonyesha mzee mzima nisivyo limbukeni kama waishiwa.

Leo nimeamka na Mwenembago akinihimiza niwakabili waishiwa wala ubuge ili niwaonye waache mchezo mchafu kutuibia njuluku zetu kwa kujilipa posho za makalio au ’sitting allowance.’
Rafiki yangu Msomimkatatamaa huziita hizi posho za majungu au rumour mongering allowance. Mie naseme hizi ni posho za ufisadi. Kwanini mtu akae tena kwenye mikochi ya bei mbaya huku akifaidi viyoyozi alipwe badala ya yeye kulipia maraha haya?

Wakati mkijilisha pepo na matanuzi wenzenu wanatanuliwa na dhiki. Je mnawawakilisha wao au matumbo yenu? Kwani tulipowachagua tuliwaambia mwende kusimama? Mbona wafanyakazi wengine, tena wa haja, hawalipwi hiyo mishiko ya makalio? Kwanza, mnakosea kuita posho ya makalio. Mbona akina Steve Wahasira wanauchapa usingizi kwenye mjengo na hamuwapi mshiko wa usingizi?

Kesho mtakuja na usanii mwingine wa kutaka posho za kulala au sleeping allowances. Hapa bado posho za kupayuka au shouting allowances. Pia nashauri zilipwe posho za kumshangilia madam Microphone na za kuogopa kutoa hoja za mashiko au cheering and fearing allowances.

Wenzenu pale kwa nyayo wanalipa kodi wakati nyinyi mnaendela kucheza makidamakinda! Wenzenu hawana vyanzo vya umeme lakini bado hawana mgawo wakati nyinyi mnavyo mmevikali na kukalia ujambazi mbuzi!

Wenzenu wamepiga maarufu ushambenga wa kutumia mashangingi nyinyi mnazidi kujiongezea mishiko kwa kuwaacha walevi wanyongwe na umaskini! Iko siku iso jina hiyo mishiko itawatokea puani. Shauri yenu. Mwenye akili na atie akilini na mwenye masikio na asikie unabii huu wa kweli.

Kwanini waishiwa wetu (wanaopenda kuitwa waheshimiwa wakati hawanayo) wanapenda kujisahau? Mkienda kwenye kupitisha mikataba ya unyakuzi mnayoiita uwekezaji mnapewa kitu kidogo na kitu kikubwa.

Mkiingia mjengoni mnapitisha kila upuuzi kama ule wa Mstaafu Mukulu aliyeleta libajeti la uongo. Nani kawaroga nyie waishiwa ambao ufisadi umewekwa mbele yenu lakini bado msiouone? Na walevi nao sijui wataacha lini ulevi? Angalieni wenzenu wa Senegali.

Juzi juzi wameamua kuingia mitaani na kupambana na shirika la kiza la nchi yao baada ya kuwaweka kizani kwa saa 48 tu. Nyie mmewekwa gizani sasa ni miaka kumi lakini bado hamuamki! Kumbaff nyote.

Walimu, madaktari na wafanyakazi wengine wanakosa mishahara nyie mnazidi kujirundikia miposho ya uongo na ukweli! Ni ulafi na upogo kiasi gani? Hamuona jinsi mahospitali yalivyojaa magonjwa badala ya madawa? Ama kweli mchoyo hana rafiki na rafiki yake ni tumbo lake.

Inatisha kuona huko madongo poromoka mtokako watoto wanakalia mimawe kama manyani wakati nyingi mnaongezeana posho za makalio. Lipeni basi posho za akili kwa walimu na madaktari badala ya makalio yenu.

Msiseme nawatukana. Hasha, nawapa ukweli ambao wengi wameshindwa kuwapa. Mnapata wapi jeuri ya kujilipa posho za makalio wakati wale mnaodai kuwawakilisha wakifa kwa magonjwa ya senti kumi? Hamjui kiza kinafanya wakaliane na kulaliana na kuongeza utitiri watoto ambao hapo baadaye watateswa na uchoyo wenu pia akili zao zitajaa kiza kutokana na kukaa kizani tangu tumboni?

Hapa lazima niwapongeze CHAKUDEMA kwa kuliona hili hata kama kwenye kambi yao kuna fisi kama lile fisi la kisukusi Joni Kibuda. Walevi hawawezi kuendelea kubeba wezi wanaojipa utukufu na uheshimiwa wakati ni wizi wa kawaida. Never, things must be changed. Why should they own everything and give us usufunctuary as the only rights for us? Thubutu yako! Patachimbika bila jembe na patakuwa hapatoshi.

Mnajilipa posho ya makalio kwa utajiri gani iwapo hata kodi yenyewe hamlipi? Muulize kiranja wao kama analipa kodi. Muulize hata baba yao kama ametaja mali zake. Wanaogopa nini kama si kuumbuka walivyo majizi ya kutupwa yaliyojificha nyuma ya madaraka? Msiseme natukana. Situkani. Kama kusema ukweli ni matusi basi natukana.

Nami napaswa kupewa posho ya Kunena ukweli au truthtelling allowance. Kama wao wanapeana posho za majungu, kwanini mie nisipewe ya kupasua jipu? Mimi ni daktari wao ni wagonjwa. Wao wanauhitaji ukweli wangu ila mimi siwahitaji kwa lolote.

Nani anahitaji mipanya kwenye nyumba yake? Nani anahitaji nyani kwenye shamba lake? Mpumbavu huyo tena hayawani mtu. Basi nasi walevi tulipwe posho ya masikio kwa kusikia urongo wenu kila siku.

Nawapa taarifa kuwa Kijiwe kinajiandaa kuja mjengoni kufanya mapinduzi matakatifu hata kama ni kutumia mawe na nyundo kama kule kw akina yakhe.

Tutahakikisha kila mbunge na kiongozi awe hata wa nyumba kumi anataja mali zake na jinsi alivyozipata bila kujali yeye ni rais au rahisi.

Kwani mlichaguliwa kufanya nini huko mjengoni kama siyo kukaa na kujadiliana? Sasa mnalipwa kwa kazi gani?

Tukikotaka hapo tunakwenda kwenye serikali za mitaa zenye mahesabu mabovu na kuchukua allowance ya corruption. Hapa tunachukua kitu kikubwa na kitu kidogo bila kujali ukubwa wa kosa wala wilaya mradi sisi tuchukue chetu mapema. Nani anajua kama kwenye uchafuzi ujao tutarejea kwenye maulaji kutokana na kiama chetu kuboronga kuliko chochote barani afurika?

Hivi kweli wabunge kama Rwakatarehe mwenye shahada ya kugawiwa wanaweza kurejeshwa hata kwa nafasi za ubwete? Mliinyaka aliyotoa kuwa alijaza mifomu ya madili shetani akainyakua. Hivi kuna shetani kama mama huyu nunga anayehadaa wenzake kuwa anaweza kuwapatia waume kwa maombi? Hayo tuyaache.

Acha nijiimbie wimbo wangu wa barua tena.

Mie mwenzenu leo niko mashakani
Nikiangalia nje kaya ikizani
Nikiangalia naona wezi mjengoni,
naamua kuandika hii barua

Barua hii inanisikitisha
Barua hii inanisononesha
Barua hii hebu chukua usome.

Nilimchagua fulani aniwakilishe mjengoni

Akaenda kule akaanza misheni
Naye akaamua kujiwakilisha
Akaanza naye kugombea mishiko .

Nimeamua kuandika barua hii
Barua hii hebu chukua usome
Barua hii kweli inasikitisha barua hii kweli inasononesha.

Hivi lile shangingi si la muishiwa? Acha nimsogelee nimzabe viba… we koma.


Chanzo: Tanzania Daima Julai 5, 2011.