Tuesday, 12 July 2011

Nimeamua kufanya maamuzi mepesi

KWA wale waliofuatia sanaa za wiki mbili ziliyopita watakumbuka: wasanii wetu walivyovunja rekodi kama si radio.

Tujikumbushe waliotumbuiza zaidi kiasi cha kupata fursa ya kuandikwa kwenye safu hii tukufu.

Wabunge wetu watukutu, sorry, watukufu walifungua pazia la sanaa kiasi cha kumzidi msanii mkuu aliyekuwa ughaibuni na mamisabu wake wakitanua kwa kodi za makapuku wa Danganyika bint Bongolalaland.

Jamaa hawa waishiwa walilianzisha kwa kutaka mshiko zaidi wa makalio bila kujali kuwa hata walevi wanastahili mishiko ya ukondoo, kuishi kizani, kuibiwa hata na mataahira na matapeli uchwara, kuishi kwa matumaini huku wengi wakijigeuza matapeli vyangu hata waganga wa kienyeji hata wale wanaojiita viongozi wa dini.

Waishiwa hawa waso haya kuondoa wale wa CHAKUDEMA hawakujua au tuseme walijifanya kutojua kuwa walevi wanastahili kulipwa posho ya woga, unafiki hata uongo. Yes. Kama si uongo kwa walevi kulalama ni kwanini hawachukui hatua kama kweli?

Hapa lazima tukumbuke. Walevi na watesi wao walistahiki kulipwa posho ya utegemezi na usanii wa kikaya. Je tatizo hapa ni ile hali ya kaya kudanganyika kiasi cha kuwa taifa la wasanii kuanzia chini hadi juu?

Hebu angalia hali ikoje mume amwibia mke, mke awaibia watoto. Mlevi anatumia pesa nyingi kuliko mapato yake na hakuna anayeuliza.

Wenye nazo nao hawataki kutaja mali zao. Hawataki hata wasio nazo nao watangaze umaskini wao. Mkuu wa kaya anaibia mabenki na wakurugenzi wa mabenki nao wanayaibia mabenki kwa kufuata mfano wake. Yeye anaiba na kuwekeza kwenye uchafuzi wa kisiasa wao uchafuzi wa kimaadili na madili. Nani anajali?

Hebu tuangalie usanii huu wa kitaifa. Matabibu wanawaibia wagonjwa maticha madenti madenti wazazi, viongozi wa dini wafuasi wao na kibaka kila apitaye. Polisi anaitiba wahalifu na muuza baa walevi.

Tuachane na usanii wa kikaya na kuenga wa mtu binafsi. Leo tutafungua pazia na Ewassa muishiwa wa Mundulia. Huyu bwana alikuwa mkubwa wakati fulani kabla ya kuharibu ofisi kwa ulafi wake.

Ajabu, pamoja na kung'olewa kwa kashfa bado analipwa marupurupu ya ustaafu utafikiri hakufukuzwa! Analipwa kwa stahiki ipi? Ajabu jamaa yake halioni kama ni tatizo.

Hiyo cha mtoto. Kwa sababu walevi ni wa kuliwa na kila jambazi mkubwa na mdogo,Nasikia jamaa bado ana ndoto za kuukwaa ukuu ili afanye makuu kuliko yale ya Richmonduli ambayo yaliwafurahisha walevi kwa kuwaweka kizani ili wazalishe vitegemezi kwa saaana tu.

Juzi Ewassa alitoa mpya kwa kumwambia mshirika wake mkuu kuwa afanye maamuzi mepesi. Alisema rafiki yake na genge lake wanaungua ungojwa uitwao kwa kitaalamu Decisive-Decisons Phobia (DPP).

Kwa ufupi, mtu anayeugua ugonjwa huu huwa na tabia ya kuchekacheka hata kwenye msiba huku akifanya vitu kama hamnazo. Mgonjwa wa gonjwa hili hatari kuliko ukimwi hupenda sifa na ukuu hata kama hana sifa wala udhu. Kadhalika, anayeugua ugonjwa huu licha ya kuanguka mara kwa mara, huishiwa kumbukumbu na aibu kiasi cha kufanya mambo ya ajabu kila mara.

Huweza kuahidi vitu ambavyo ukimuuliza kesho yake hakumbuki wala kujua. Muathirika wa DPP huishi kwa kujilisha pepo na uongo bila kujua kuna kesho. Hupenda kutumiwa na majuha na matapeli hasa kwa kumuahidi pepo zaidi hata penye moto.

Baada ya Daktari Ewassa kugundua ugonjwa wa rafiki yake na kumshauri afanye maamuzi mepesi kwa kumsafisha asifanye hivyo kutokana na ima kusahau au kusumbuliwa na DPP, aliamua kuutangazia umma siri ya siri ya swahiba yake kuwa anaumwa DPP.

Alifanya hivyo kwa kisingizio cha kuwapenda walevi wakati ukweli anawachukia kupita hata manonihino yake. Angewapenda angewaweka kizani bila kosa lolote?

Wengi walishangaa ugunduzi huu wa aina yake. Kwa mara ya kwanza ambapo nyani aliweza kuona kungule!Wengi walidhani Dk. Ewassa angekuwa mkweli na kuelekeza ugunduzi wake kwenye gonjwa lake liitwalo Illegal Wealth and Moneyphilia kitaalamu au (IWM).

Gonjwa hili likimpata mtu huwa mlafi kupita hata fisi na panya. Mwenye kusumbuliwa na gonjwa hili anaweza kuwatoa sadaka hata ndugu zake hata mama yake.

Kadhalika mwenye gonjwa hili huishiwa kumbukumbu na huwa haoni aibu hata akitenda mambo ya kuaibisha kiasi gani sawa na mwenye DPP.

Na hii ndiyo maana mara nyingi waathirika wa gonjwa hili huwa marafiki na baadaye kutokana na kutokuwa na kumbukumbu wala aibu hugeukana na kutishiana hata maisha. Mwenye kuugua gonjwa hili hupenda kuchuma kijambazi huku akijidanganya kuwa watu hawajui chafu yake.

Gonjwa hili ni hatari sana. Kuna kipindi hushambulia kabila zima kiasi cha watu kuwa waroho kiasi cha kuchukua hata dada zao ambao nao huwa tayari kulala na kaka zao mradi wapate kuchuma haramu iitwayo pesa au utajiri. Hapa jamaa zangu kule kilimani mnanipata bila shaka.

Hilo leo siyo inshue. Tundelee. Mwenye gonjwa la IWM naye kadhalika hupenda makuu kiasi cha kusahau ukweli. Gonjwa hili kwa mara ya kwanza liligunduliwa na profesa Juliyasi Mchonga Nyereire kutoka chuo kikuu cha Mwitongole kule Kusoma Mara kwa mara.

Kwa vile Profesa Mpayukaji ni gwiji wa magonjwa ya akili na roho, ameamua kufanya ugunduzi wa aina yake. Ugunduzi wenyewe una matokeo yafuatayo:

Mosi mgonjwa wetu wa IWM atapata kichaa baada ya ndoto zake za Alinacha kustukiwa. Kadhalika mgonjwa wa DPP hatakuwa tayari kukubali ushauri wa mgonjwa wa IWM kwa vile anajua anasumbuliwa na ugonjwa wa akili kama wake.

Kimsingi majaribio ya kisayansi yanaonyesha kuwa wagonjwa hawa wawili watachanganyikiwa na kuchanganyana hadi wavuane nguo hasa kuanzia tarehe 10 Julai wakati ambapo mwezi utakuwa mchanga kiasi cha kusumbua akili za wagonjwa hawa.

Pia utafiti umeonyesha kuwa waathirika wa magonjwa haya mawili ni hatari sana kwa kaya kuliko hata ukame na mafuriko. Maana huwa wanatumiwa na kunguru kuchuma na kuibia walevi.

Kutokana na uzoefu wa siku nyingi, Profesa Mpayukaji napendekeza kuwa wagonjwa wataweza kupata nafuu iwapo watakubali kufanya maamuzi mepesi ambayo ni kusema ukweli kuwa wanaumwa sana na wanahitaji msaada toka kwa waganga wa kweli na matapeli pia.

Ikitokea wagonjwa wakagoma au kujifanya wamesahau kufanya maamuzi mepesi basi walevi hufanya maamuzi magumu na kuwatia nari mchana kweupe.

Hivi ule msafara si wa Njaa Kaya. Ngoja niokote mawe nifanye kama walivyofanya akina Twambombotununu kule Mbe way. Naona kinokia kinaanikiza. Mbona namba kama ya Ewassa! Hello Eddie, How are you my friend? Ushaamua kufanya maamuzi mepesi na kuweka mambo hadharani? Kwa kheri!

Chanzo: Tanzania Daima Julai 13, 2011

No comments: