Wednesday, 20 July 2011

Sasa nimeanzisha Mpayukaji Trust Fund (MTF)

WAPENDWA wasomaji wa kijiwe leo nina furaha si kawaida. Kwanza nafurahia kifo cha kisiasa cha yule jambawazi wa Kagoda yaani Roast Tamu. Pia wakati nikifurahia kifo hiki natangaza vifo vya kisiasa vya Eddie Ewassa na Endelea Chenga vitakavyotokea hivi karibuni katika kijiwe cha Chama Cha Mafisadi wenye magamba.

Ingawa si mada ya leo, tunawashauri walevi wasiridhike na usanii huu hadi gamba kuu yaani aliyepatikana kutokana na ujambazi wa HEPA naye akitoe. Avuliwe kama hataki kujivua. I think you know what I mean.

Pili, ninaleta habari njema ya kuwapasha. Hii ni habari njema kwangu na ukoo wangu ingawa huko tuendako yaweza kuwa habari chafu na mbaya kwa walevi.

Taarifa ya kwanza ni kwamba bi mkubwa mshirika wangu wa Bedroom amepewa ulaji na ndugu yangu mpendwa na mheshimiwa sana mtukutu, mtukufu rahisi wa walevi alhaj Daktari wa kupewa Njaa NK Kaya.

Mtukutu rahisi, sorry mtukufu rahisi, amemteua mshirika wangu kuwa mwakilishi wa walevi kwenye umoja wa mataifa wa walevi kule New Amsterdam kwa Joji Kichaka.

Wale wasiojua historia ya taifa hili jeuri nawaibia kidogo. Sisi wataalamu wa historia hupenda kutumia majina ya zamani. Kwa ufupi New Amsterdam ni New Yoko.

Hivyo ninapoongea ni kwamba nitakuwa nikwahabarisha tokea New Yoko inshallah. Kwa vile mie nahamia kule na mshirika wangu wa Bedroom anihitaji kama hewa na sina kibarua, lazima tukune vichwa nami nipate kibarua cha haja na mashiko.

Katika kutafakari la kufanya, tumekuja na wazo la kuunda Trust Fund ambayo itatuingizia pesa kiasi cha kufanya mie na mshirika wangu kuwa tunakuja kutanua Bongolalaland bila kutumia njuluku zetu.

Pia kuogopa kuitwa kula kulala, tumeanzisha Trust hii ambayo itapewa jina langu ili niwe nazunguka kwa watasha na kuvuna njuluku kama sina akili nzuri.

Hata hivyo, kutokana na kujua tabia yangu ya kupenda kuhonga vimwana, mshirika wa bedroom ameamua awe mwenyekiti wa Trust kiasi cha kunifanya mie nionekane kama kikaragosi hata kama Trust yenyewe imebeba jina langu. Anaogopa nisimalizie mshiko wote kwenye kuwahonga vimwana wa kitasha kule New Yoko.

Ukiangalia jina la kampuni yenyewe, utagundua kuwa inashawishi. Trust kwa kiingilishi ni uaminifu. Nasi tumeamua kutumia sifa hii ingawa nyuma ya pazia ni kinyume.

We uliyepewa siri hii soma kimya kimya na usimwambie mtu nisije nikapigwa talaka kutokana na bi mkubwa kwa sasa kuwa mume nami mke. Si unajua tena. Mwenye nazo si mwenzio aweza kufanya lolote kiasi cha mwanamke kuoa na mwanamume kuolewa.

Tuachane na mambo ya kuolewa na kuoana na talaka. Hayo ni yangu na mamsap wangu. Turejee kwenye ulaji wangu mpya.

Najua watasha wakiona malengo yetu watamwaga njuluku kuliko hata zile wanazomwaga kwa shoga wa bi mkubwa wangu mwenye taasisi ya Ki-siri kali ya MAWAWA yaani Maulaji ya Wake wa Wakubwa aliyoinzisha baada ya mumewe kuukwaa ukuu.

Kwa vile mwakilishi wa rahisi kwenye umoja wa mataifa wa walevi naye ni sawa na rahisi, lazima kuanzia sasa kila mume au mke wa balozi, waziri, mkuu wa mkoa na wilaya waanzishe NGO ili nao kuwa kwenye kundi la ulaji na uheshimiwa.

Na hii ndiyo sababu ya kumwalika sorry, mke wa rahisi kuja kuzindua Trust yetu. Bila kuchelewa hebu tuwape japo kwa ufupi majukumu ya Trust hii tukufu.

Ifahamike kuwa baada ya wafadhili kustukia ufisadi kwenye lisirikali, tumegundua kuwa wanaamini sana Trusts na NGOs. Hii ndiyo maana utagundua kuwa Trusts za uongo na ukweli isipokuwa yetu na NGOs za ulaji isipokuwa MAWAWA, zimeota kama uyoga karibu kila mahali.

Hii imelenga kudaka njuluku za wafadhili na kuzifanyia kweli. Sisi tunakula tukipuuliza siyo kama wale jamaa wa Richmonduli AIPITIELO, HEPA, Meremetuka, SUKITAI, TICKS, TITISIELO, EYA TANZIA na wengine wengi wanaohomola kana kwamba wanawaibia vipofu.

Kwa vile yetu ni Trust Fund, tunawaomba mtuamini hata kama hatuaminiki. Tumejikita kwenye kuhakikisha tunakula na tunawakabili wafadhili kuhakikisha tunapata chetu na pesa ya Madawati kwa ajili ya watoto wa walevi wote wanaoleweshwa na kukalia mawe kama nyani katika karne ya 21.

Tumeamua kushughulikia madawati baada ya kugundua kuwa wabunge wanaopaswa kuyahangaikia wanahangaikia posho ya makalio yao badala ya madawati ya watoto wanaodai kuwawakilisha.

Wabunge wanakalia makochi mazito na kufaidi viyoyozi na kulipwa posho ya makalio wakati wanafunzi wanakalia mawe na hawalipwi posho ya makalio wakati wao ndiyo wanaostahiki kulipwa kwa kuumiza makalio yao kwenye mawe badala ya madawati.

Kwa vile Wazungu wanajali sana elimu maana ndiyo iliwawezesha kututawala sisi watakubaliana na kuingia mkenge wetu wa kuchuma njuluku kwa kisingizio cha kuondoa unyani wa kukaa kwenye mawe na ule wa watawala kuahidi maisha bora wakaishia kuleta maisha mbofu.

Kwa kujua umuhimu wa afya za walevi, tumekuja na mkakati wa kutafuta misaada kwa ajili ya dawa. Tunafanya hivyo kutokana na huruma kwa vile sisi na washirika wetu tunatibiwa nje hata kuangalia mafuta ng’ambo.

Pia tumeamua kushughulikia dawa baada ya kuona watu wakihamanika kwenda Loliondo kutapeliwa na Babu Ambilikile mwasapila kutokana na kutokuwa na dawa za kutosha. Hivyo, hata kama sisi ni wale wale, tunalenga kuepusha utapeli huu kwa kuleta upya.

Ili kuwaingiza Wazungu kwenye mkenge zaidi, tumeorodhesha karibu kila kitu kwenye kazi za Trust yetu.

Tumeorodhesha vitu kama vile vitabu, walimu, madaktari, wawekezaji hata wachakachuaji wa uchaguzi ambao tumewaita wataalamu wa kueneza demokrasia kwenye kaya ya Bongolalaland.

Kwa vile watawala wao wameshindwa kukidhi matakwa yao kama walivyowaahidi, nasi ngoja tuingie kwenye game kama wakombozi ingawa mwisho wa siku watajuta kutuamini.

Ngoja niwahi Airport tayari kupanda pipa kuelekea New Nyoko.

Hivi yule siyo Hassan Maajalala? Mbona anaonekana kama anatoka mitaa ya Roasttamu kama yeye si fisadi?

Ngoja nimfuate nione anaelekea wapi usawa huu.

Kumbe leo ni siku yetu ya mgawo! Acha niwahi kabla vibaka hawajaninyotoa roho.

Chanzo: Tanzania Daima Julai 20, 2011.

6 comments:

malkiory matiya said...

Hongera sana Mhango, huo ni uamuzi wa busara na wa kizalendo.

NN Mhango said...

Bwana Malkiory niponge leo kesho unilaumu. Kimsingi uamuzi wangu ni wa kizalaji zi kizalendo. Mie ni mlaji si mzalendo hata chembe. Wengi wamenipongeza kama walivyompongeza Majaar wasijue nyuma ya pazia ni ulaji kama kawa!

Anonymous said...

Lakini mbona trust fund ni kitu kingine kabisa huku?..Trust fund huku wataelewa unakusanya hela kwa wanao ya baadaye. Unafungua trust fund ili kiasi fulani kiwekwe huko ili mwanao akifikia miaka fulani basi ndio anaruhusiwa kuchukua. Na turst fund wanafungua mamilionear kwa vile inahitaji lawyers and the whole workds. Chairman ni kama appointed person anayesimamia hiyo hela iwapo utaondoka hapa duniani kabla mwanao hajafikia huo umri uliotaka aanze kuchukua share yake basi hao watu ndio watashughulikia jinsi ya kuinvest hiyo hela.

Siku hizi wajanja nao hela imekimbia hivyo mabakuli hayapiti hovyo kama zamani...

Just give you a little hint before you get disappointed.

Kupiga box la mitaani muhimu ukija huku. Utajivunga mwaka wa kwanza lakini baada ya plan A kukimbia plan B ni box la mtaani. Hivyo usilionee aibu kuliko kupoteza muda ukifika tu anza networking. Kama huko unabeba briefcase na kufunguliwa milango ya gari we jifanye hukupitia hivyo vitu ukija huku kama unataka kama unataka hela. Ukijivunga basi subiri mwaka aibu za kibongo zikiisha utalisaka peke yako

malkiory matiya said...

Kwa jinsi unavyochukia ufisadi sidhani kama utapenda kuwa na harufu ya ufisadi ndani mwako!

NN Mhango said...

Ni kijembe ndugu yangu kwa wanaoanzisha NGO na Trusts kwa ajili ya kuibiwa wabongolalanders kama alivyofanya mumewe Mwanaidi Majaar huko New York baada ya kuona anageuka kula kulala kwa mkewe ambaye naye ni tunda la EPA.

Jaribu said...

Naona wabongo hawapati mambo ya tongue-in-cheek. Sarcasm inaharibika ikibidi uwachambulie wasomaji.:-)

Naona mumewe Mwanaidi anamwiga mtangazi mmoja anayekusanya mchango wa madawati kupeleka Malawi. Tofauti ni kwamba huyu ana moyo na nia njema, wakati Bwana Maajar anafanya mradi. Hata Membe anasema BAE wawarudishie hela za radar wanunue mamilioni ya madawati.