Tuesday, 26 July 2011

PUMBA ZA MLEVI MDANGANYIKA


Nichukue fursa hii kujitambulisha rasmi kama mwenyeji wa wasomaji wa gazeti hili. Nimeanzisha safu hii baada ya kuombwa sana na utawala wa gazeti kutokana na kutokuwa na taimu ya kuacha kupiga mma na kuandika.

Kimsingi, safu hii itakuwa kipenzi cha makapuku, walevi na wadanganyika wengine popote walipo kwenye anga hili la wadudi.

CV yangu ni kali. Mie nilizaliwa miaka mingi iliyopita chini ya utawala wa Kaisari wa Kirumi. Kutokana na baba yangu kuwa mlevi maarufu na mama muuza gongo, nilipozaliwa, walinipa jina la biashara yao yaani Mlevi. Nimesoma kwa pesa ya gongo na kukuzwa kwayo. Akili yangu ni ya gongo hata damu yangu. Hivyo nitakachoandika humu kama kitakusumbua usijisumbue kwenda polisi au kuazima kibiriti uchome kibanda changu au bastola kunitoa roho. Nilishajifia zamani hata polisi wanajua hili ndiyo maana wakija Uwanja wa Fisi kuwatoa upepo wauza gongo, madawa na bangi, huwa hawahangaiki nami. Watahangaikaje na jitu lililokwishapigika kulhali?

Niliosoma nao sasa ni wabunge na mawaziri. Hata mheshimiwa Rai--- stoop! Nilisoma naye kule Chalin….. makubwa haya!
Wale akina dada sorry mama niliocheza nao michezo ya kujificha na kujenga nyumba sasa wanaitwa bibi kama sijasahau.

Zama zile najua mkoloni aliyekuwa akitawala nchi yetu alihimiza elimu kiasi cha kuwakamata wazazi wangu na kunipeleka shule. Mwanzoni nilianza vizuri nikiwa na usongo wa kuikomboa familia yangu. Hii ilikuwa ni kabla ya washenzi fulani kunikomoa ili nisiikomboe familia yangu. Nilfanya vizuri kwenye mtihani wa Cambrige kiasi cha kupeana mkono na Malkia wa Uingerezani.

Kutokana na roho mbaya ya waswahili, walipoona nazidi kupaa bila mbawa wakaamua kunipiga kipapai kiasi cha kuishia kwenye vilabu uchwara vya gongo.

Baada ya kuachana na mambo ya shule kutokana na kupigwa kipapai na walimu kuzidi kuwa wanoko, nilijichimbia kwenye unywaji. Shamba langu, ofisi yangu na wakati mwingine kitanda changu vilikuwa baa. Nilikopa sana. Nilikunywa hadi kukufuru. Kuna kipindi mama wa Kichaga aliamrisha nivuliwe suruali baada ya kushindwa kulipia gongo na mapupu kwenye kibanda chake. Niliondoka pale bila nguo isipokuwa Godfather pekee.

Kuna kipindi nilitaka kujitoa roho baada ya kuona maisha yangu yanakosa maana. Nilipokuwa nikitundika kamba mtini ili nijimalize si nyoka akanitoa baruti! Tangu siku hiyo sijawahi kufikiri kujiua tena.

Baada ya jaribio la kujiua kushindwa, niliamua kuachana na gongo. Kwa miezi minane sikunywa gongo wala kuvuta bangi. Afya yangu ilinawiri na wazazi wangu wakaanza kupata matumaini kuwa huenda ningeendelea na kazi ya ukombozi wa familia. Ni kipindi hiki nilipompata aliyekuwa mke wangu bi Domokubwa. Mama alisifika kwa kuchonga.

Mungu ni mjanja. Baada ya kuona nimerudia gongo na kuongezea bwimbwi huku mke wangu naye alianza kubadilika baada ya kugundua kuwa mie si chuma ulete aliyetegemea, Mungu hakutupa mtoto. Maana tungempata angekuwa balaa. Kama angerithi ulevi wangu angekosa maana. Na kama angerithi tamaa ya mama yake kupenda pesa na jeuri ndiyo usiseme angeishia Segerea bure.

Historia yangu ni ndefu kama barabara. Naomba niikatize hapa nizame kwenye pumba zangu. Najua wapo walevi na waharibikiwa wengi kama mimi. Hivyo naamini watakaposoma watafurahi.

Nianze na kisa cha leo. Juzi nilikuwa zangu kwenye banda letu la gongo ambalo sitaki nilitaje ili polisi wasije wakamkamata mama muuza nikaishia kukosa ulabu. Tukiwa tunakamata ulevi si akaja mpambe wa waziri wa Kiza Bill Ngereza. Jamaa alikuwa a na mabulungutu ya pesa kama yale bosi wake alitaka kuwahonga waishiwa sorry waheshimiwa. Aliagiza gongo kwa sana huku akisema ameona wokovu wa kuwapenda walevi na kuwanywesha hadi wafe. Sie kutokana na kudanganyika kwetu na kiu na mawazo tulifakamia gongo kama hatuna akili nzuri. Kumbe jamaa alikuwa na lake. Alitaka kutupa mkanda mzima wa kasheshe ya rushua inayomkabili Devil Jeuri Jero. Jamaa alimtetea bosi wake kuwa hakuwa na habari kuwa kumbe katibu wake alikuwa na mpango wa kuwahonga waishiwa sorry waheshimiwa.

Alimtupia mzigo Bangusilo Jero ambaye inasemekana aliandika waraka huu na kumpasia Milima ya Kigoma kabla ya kupitiwa na Bill mwenyewe. Tusingeyajua haya kama siyo ulimi wa jamaa kuteleza. Kwa vile ulabu ulikuwa umempanda jamaa, alimwaga mtama kibao kwa walevi. Una habari alisema kuwa bosi wake na Jero hawawezi kufukuzwa kibarua kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na wanono. Ingawa alitaja majina ya hao wanono tena wengine wakiwa nambari wani, sitawataja kuogopa kuvuruga amani na mshikamano wa walevi wa Danganyika.

Kwa ufupi ni kwamba hata hiki kiza kilichowageuza walevi mende kimetengenezwa na wenye mamlaka ili wazidi kupata mshiko toka kwa wauza majenereta.

Baada ya ulabu kumtoka kidogo jamaa alihoji ni kwanini wahongaji wengine hawashughulikiwi wala wanaopokea hongo zao ili kupitisha mambo yao? Ingawa jamaa alikuwa kalewa akiongea na walevi, alikuwa na hoja. Nilipofika nyumbani kusema ukweli sikulala. Picha ya jamaa akichonga ilizidi kunijia hadi nikajiuliza swali moja kuu. Je Ngereza ni wa kwanza kuwahonga wahusika hata kama wanajifanya kuwa na hasira naye? Nakumbuka. Jamaa alisema kuhongwa na kuhonga ndiyo siri ya jamaa kupitisha kila upuuzi kuanzia mishiko ya makalio, sleeping allowance, suit allowance na makando kando mengine. Jamaa alisema wazi kuwa wote ni wezi ingawa mimi sisemi wala kuamini hivyo.

Alisema ukitaka kujua kuwa wao ni wezi wakubwa tena wasio na aibu, jiulize kwanini wanajadili kutumia bajaj kubeba wajawazito wakati wao wanapanda mishangingi na madege kila uchao? Huko siendi leo. Nakuachia uamue kama ni kweli au la. Halafu kuna upuuzi huu wa kuwasha umeme usiku wa manane. Nani halali anangoja umeme? Achene usanii jamani mtatugombanisha bure.

Leo nashughulishwa na kiza cha Ngereza na kashfa ya mshiko. Mpaka sasa sielewi Ngereza, Milima ya Kigoma na Jero wanangoja nini wanaharamu hawa! Je wao ni wale wasioguswa? Kama hawaguswi kwanini wao wanawagusa wengine kwa kufichua ulaji wao wa sirini? K wa vile mie ni mlevi wa kawaida, nafikiria kilevi na kubwabaja kilevi. Nasema: wote ni majizi tu hakuna cha nini wala nani ni majizi tena makubwa. Heri wangekuwa walevi kama mimi wangedanganyika na wala wasingemuathiri yeyote isipokuwa wao wenyewe. Utajuaje? Huenda nao ni walevi wa uroho na ulafi. Kwani ulevi ni gongo tu?

Kwa vile sina uchache wa kununulia mapupu, ngoja niachie hapa na kuwahi kwa mama Betty lau anikopeshe mapupu na glasi ya gongo. Kulaleki! Nawasilisha.
Mlevi Mdanganyika
Mafichoni
Akili Kichwani
Chanzo: Dira ya Mtanzania Julai 26, 2011.

No comments: