The Chant of Savant

Saturday 27 July 2013

Walevi wampongeza `Jei Kei’ kuwakabili wanasiasa mufilis


Mwalimu Nkwazi Mhango.
Japo wabaya wa Mkuu wanamuona na kumueleza kama mtu aliyeshindwa vibaya baada ya kuingia madarakani, walevi wanaona ana mfanikio tena ya kupigiwa mfano.
Mfano, amefanikisha kumleta Obamiza kuja kutubamiza mkenge wa Ubungo. Kwani hili si fanikio hata kama ni hasi?
Ili kutathmini mafanikio tata ya Mkuu wetu Jei Kei, unapaswa kuepuka kutumia falsafa isemayo, “fanya nikwambialo na siyo nitendavyo”. Waingereza huita tabia hii Better than thou yaani mimi ni bora kuliko wewe.
Hivyo, lazima ufuate nikwambiayo na siyo nitendayo. Kwa maana nyingine, ukitumia falsafa nyingine ya, “ukitaka kumla kuku usimchunguze alacho”.
Japo Jei Kei alishindwa kutimiza ahadi zake za maisha bora, kurekebisha mikataba ya kijambazi ya uwekezaji, kuimarisha uchumi, kubana matumizi, kupambana na uzururaji na uvivu wa viongozi na kupambana na ufisadi, amejitahidi kusema wazi juu ya masuala mbali mbali anapoamua.
Akiamua kusema huwa hapotezi muda kwenda kwenye kioo kujiangalia kama anayosema yatamgusa nani. Hivi karibuni, Jei Kei alikaririwa na vyombo vya habari akiwaonya wanasiasa mufilis wanaolenga kuigawa kaya kwa misingi ya ukabila, udini na mali katika harakati za kutaka kumrithi kama Mkuu.
Aliwashukia bila kujali kama ni maadui au marafiki zake. Alikaririwa akisema, “nawaasa wanasiasa wasipandikize chuki za kidini au maeneo wanakotoka wananchi, kama ni madaraka yatafutwe kwa njia ya amani kwenye sanduku la kura.”
Hapo, Jei Kei alilenga penyewe, ingawa alichelewa. Kwa wenye kuelewa tabia na staili ya Jei Kei ya kutawala, walibaki vinywa wazi wengi wakimtuhumu kutenda dhambi anayowakataza wenzake kutenda.
Kimsingi, kuna kitu kinaitwa “kuona mwanga” kama alivyofanya Paulo wa kwenye Biblia. Hii hali ipo japo ina utata wake.
Wenye kupenda kuitumia hujitenga na kuchunguza utata wa kwanini mdhambi aone mwanga baada ya kugundua kuwa zake zimekwisha kama si unafiki.
Wengine hufumbia macho upande huu na kuangalia nini wanachotaka kufanikishwa kwa kutumia falsafa hii kongwe na tata.
Walevi wanajua kuwa Jei Kei ni Mkuu wa Kaya mwenye uzoefu mkubwa kuhusiana na `umufilis’ wa kisiasa. Anajua fika kuwa hakuna viongozi muflis na hatari kama wale waliopata uogozi kupitia uongo, ahadi hewa, rushwa, wizi wa fedha za umma, kuwachafua wenzao na kuwaganya wananchi.
Walevi wanajua kuwa Jei Kei anajua fika madhara ya viongozi wa namna hii. Kwani wanapopata nafasi hubariki rushwa na kuendeleza ufisadi bila kujali mustakabali wa kaya na walevi.
Mbwamwitu wa namna hii huwauza hata walevi bila kujali kuna kesho. Walevi wanafahamu kuwa Jei Kei anafahamu wazi kuwa siku hizi uongozi hasa urais ni ufalme na nafasi ya kula bure kwa mhusika, familia yake na waramba viatu wake tena kwa mikono yote bila kunawa.
Jei Kei anajua kuwa viongozi wachovu na mufilis watokanao na jinai ya kugawana watu na kuwachafua wengine hutawala kiujanjaujanja bila kufanya lolote la maana zaidi ya kuwaibia walevi.
Jei Kei anafahamu sana madhara, kwa mfano, ya kuteua watu kutokana na kulipana fadhila, udini, ukabila hata ueneo. Anafahamu fika kuwa viongozi wa namna hii ni kansa na ajali kwa kaya.
Kwani, hawalifanyi chochote bali kuangamiza kaya. Anajua fika kuwa viongozi watokanao na kuwagawa na kuwahadaa walevi ni walafi na vipofu wanaoweza kulala kitanda kimoja na wauza unga, majambazi, mafisadi hata wawekezaji wachukuaji kama ilivyo sasa.
Walevi wanapenda sana roho ngumu ya Jei Kei ya kusema anavyojisikia. Walevi wamepanga `kumtwanga ofa’ ya kanywaji kwa kufanya kile wanachofanya kila siku.
Hakuna alipowakuna kama pale alipowatolea uvivu wanafunzi wanaomimbwa aliposema kuwa ni kutokana na kiherehere chao.
Jamaa hakujali kujua kuwa maisha mabovu, utawala mufilis wenye kuendekeza ufisadi na migawanyiko na wizi unaweza kuwa chanzo cha watoto kupewa mimba mashuleni ukiachia mbali sheria mbovu.
Pia Mkuu aliwahi kuwaambia walevi kuwa hajui chanzo cha ukapa wao pamoja na kulalamikia matumizi mabaya ya ‘njuluku’ zao na uzururaji wa `mabig’ wao.
Ndiyo, `Dingi Riz’ hakuwa na haja ya kujihangaisha kujua kuwa chanzo kikuu cha umaskini wa walevi ni utawala wa kijambazi wa kujuana na kulipana fadhila.
Hakuwa na haja ya kujua kuwa chanzo kikuu cha umaskini wa walevi ni uwekezaji mbovu wa kijambazi na kulinda ufisadi.
Mkuu huwa hajali anayemgusa anapoamua.  Hakuna alipowakuna walevi kama alivyowapigia kampeni na kuwapa kampani wakwapuaji vigogo kama akina Endelea Chenge, Basie Pesatatu Mrambaramba, Eddie Luwasha na Roast Tamu la Aziz? Huyu ndiye Jei Kei asiyeogopa kitu.
Walevi wanajua kuwa Jei Kei anajua fika kuwa utawala wa kujuana hasa kwa misingi ya dini au ukoo ulivyo.
Anajua kuwa viongozi watokanao na rushwa na kila aina ya jinai huwaruhusu watoto wao na wake zao kuuibia umma kupitia biashara haramu kuanzia ya kupata tenda hadi kuanzisha NGO.
Hivyo, Jei Kei anapowanyoshea kidole wanasiasa mufilis anawajua fika. Je Jei Kei ameona mwanga na kupata ufunuo baada ya kushindwa kwenye safari yake ya kuwapeleka walevi Kanani au ni changa la macho?
Yote yanawezekana. Je, Jei Kei anatafuta nafasi nzuri kwenye historia ya kaya baada ya kugundua kuwa wakati umemtupa mkono? Baada ya walevi wasio na adabu wanauliza:
Kwanini alinyamaza muda wote ukiachia mbali kuyafumbia macho baadhi ya mabaya anayowashitakia wenzake?
Je, Jei Kei amejifunza kwenye mtifuano na mchafuano wa mwaka 2005 ambapo baadhi ya waandishi habari uchwara na `mafisi’ kutumika kuwachafua wagombea walioonekana kuwa tishio?
Walevi wanakumbuka ulevi, ukabila na ubaguzi wa rangi uliozalishwa na kampeni hizi chafu ambapo watu wa maana na maarufu kama Dk Salimuni Ahmed Salimuni walibatizwa u-Hizbu na uarabu?
Je, walioasisi uchafu huu na kuutenda wanaweza kuona mwanga leo au ndiyo usanii wenyewe? Je, wahusika wamesahau madhara waliyolisababishia taifa na baadhi ya watu waliowalenga?
Hata hivyo, tumshukuru Jei Kei kwa kujitoa kimasomaso na kusema ajualo tokana na uzoefu wake. Anajua fika kuwa walafi wa madaraka huibia taasisi za umma au kuingia kwenye dili za kijambazi kama EPA na Richmond ima kupata pesa ya rushwa au kulipa fadhila kwa wale waliowawezesha kupata madaraka kwa njia chafu na haramu.
Tusipuuzie ushauri wake, hata kama una utata kutokana na nani ameutoa. Hongera Jei Kei, kwa kuwakabili wanasiasa mufilis.
Salamu kwa walevi wote wa Bariadi, Igunga, Rombo, Bwagamoyo, Kimbushi, Msata, Manushi, Nkoaranga, Monduli, Kibondo, Kayungu, Nyakabanga, Kandegesho na kwingineko.

Chanzo: Nipashe Jumamosi  Julai 27,2013.

2 comments:

Jaribu said...

Huyu jamaa angekuwa Dakta kweli angejua kuwa kukaa kimya kumnasaidia sana zaidi ya kuongea. Kila anapofungua kinywa unatoka utumbo tu!

Anonymous said...

Kweli kabisa bwana Jaribu! Chochote anachoongea yeye ni upuuzi bin pumba. Anahitaji kukaa chini na kufikiria oops nimeshahu sidhani kama ana upeo huo. Mtu kama anawaza kusafiri all the time sidhani kama ataweza kufikiri mambo ya msingi!