The Chant of Savant

Tuesday 16 July 2013

Ziara ya Obama imetufumbua macho Tanzania si salama


Wapo wanaoona kuwa ulinzi mkali wa Rais Barack Obama wa Marekani ni jambo la kawaida. Wapo wanaoona kama ama ni uzembe wetu kama taifa au udhalilishaji. Jibu ni lipi? Tuangalie hali ya usalama nchini mwetu.
Japo baadhi ya wadadisi wameamua kutufanya majuha kusema eti tukubaliane na vimbwanga, vituko vitimbi na vijimambo tulivyoshuhudia wakati wa ziara ya Obama wa Marekani nchini ni vitu vya kawaida, ukweli ni kwamba itifaki ilivunjwa. Kwa nini utawala wetu uliruhusu itifaki ivunjwe?
Je, kwa nini ulinzi wa mtu mmoja tena Rais wa taifa jingine ambaye halipi kodi kwetu wala hakuchaguliwa na Watanzania ulipewa kipaumbele kuliko taifa zima?
Nani amesahau kuwa kwa kipindi chote Obama alichokuwa Dar, nchi yetu ilikuwa rehani? Dar ndiyo moyo wa Tanzania na ndiko ziliko zana zote za usalama na asasi zake.
Ajabu wakati wote wa ziara ya Obama, asasi hizi nyeti kwa taifa ziliwekwa mikononi mwa walinzi wa Obama bila kujali kuwa Watanzania wanahitaji huo ulinzi na usalama.
Kilichotokea kimeonyesha kuwa majeshi yetu yote ni kanyaboya na hayana hata maana. Je, ukweli ni upi? Wamarekani wanajua kuwa vyombo vyetu vya usalama havitekelezi majukumu yake vilivyo.
Wanajua tulivyo na askari polisi wa kutosha kuwapiga na hata kuwalipua wapinzani lakini hatuna askari wa kutosha wa kupambana na wauza unga, majambazi, wafanya magendo, wakwepa kodi, mafisadi na wahalifu wengine wengi tu. Je, hili na lo ni siri?
Wengi wameshuhudia mnyukano wa nani ni nani kati ya mwenyeji na mgeni. Wapo waliofikia mahali kusema kuwa mgeni njoo mwenyeji asote.
Hii ndivyo ilivyotokea wakati wa ziara hii ambayo imewaacha Watanzania wakiwa wamegawanyika makundi mawili yaani wanaoishabikia kwa vile wananufaika nayo na wale wanaoipinga kutokana na kuathiriwa nayo.
Kwa watawala, kuja kwa Obama ni mafanikio makubwa kuliko yote hasa kwa utwala wa Rais Jakaya Kikwete tangu aingie madarakani.
Wapo wanaosema kuwa tangu aingie madarakani, Kikwete amefanikiwa kufanya jambo moja yaani kulidhalilisha taifa mbele ya ulimwengu kwa ‘kujiachia’ kwa Obama.
Vituko vilianza pale magazeti yaliporipoti kuwa Obama alionywa asiguse maji yetu kwa vile si salama. Hili ni kweli. Maji yetu sawa na taifa letu si salama.
Mambo yalizidi kuongezeka tuliposhuhudia madege na meli vikiletwa nchini kuhakikisha usalama wa bwana mkubwa. Wengi walishangaa inakuwaje kusiwepo na usalama nchini wakati rais wetu siku zote yuko salama na misafara yake ya magari?
Kumbe kisiwa cha amani tunachoambiwa ni usanii mtupu! Kumbe tunajidanganya, kudanganya na kudanganywa kuwa tuko salama wakati tuko hatarini?
Wapo waliojiuliza: Kama ‘jeuri’ ya Obama ingepata nafasi chini ya uongozi jabari na wa kujiamini wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Wengi walishangaa na kubaki na maswali kuliko majibu.
Hakuna kitu kilituacha hoi kama kusikia hata mawaziri wakilalamika kuwa hawajui kama wataruhusiwa kwenda kumpokea ‘mgeni’ wao.
Maana wao ndiyo serikali yenyewe. Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe alikaririwa akilalamika, “Hii sijawahi kuiona, hata sisi wenyewe tunateuliwa na wakishayapitia wataamua, nani aende au asiende.”
Tukubaliane. Huu ni udhalilishaji na ukiukwaji wa itifaki. Ni ushahidi kuwa mgeni ana thamani na nguvu kuliko mwenyeji kutokana na kuendeleza ubabaishaji na uzembe.
Ni ushahidi kuwa taifa letu halijawa huru vilivyo. Ni ushahidi kuwa uongozi wetu una mushkeli tena mkubwa. Na hii si mara ya kwanza kwa watawala wetu kuonyeshwa kama watu duni wa mataifa ya Magharibi.
Alipokuja rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, alijigamba kuwa ukiona Clinton amekuja Tanzania jua uchumi unakua. Uongo mkubwa!
Baada ya Clinton kuondoka uchumi haukukua. uliendelea kudumaa. Sijui kipindi hiki tutaambiwa nini!
Kuna kisa kilivuma miaka ya nyuma kuwa siku moja Mwalimu Nyerere alikwenda kwenye ziara ya kikazi nchini Uingereza. Mmoja wa wakubwa wa Uingereza aliyepangiwa kukutana naye alikuwa Malkia Elizabeth. Inasemakana kuwa mwalimu alipokwenda Buckingham Palace kwenye dhifa ya kitaifa, malkia alimpokea huku akimpa mkono uliokuwa umevalishwa glovu. Mwalimu kuona vile alikwepa kuupokea na badala yake alichomoa kifimbo chake na kumpa malkia aliyebaki kutaharuki. Kwa aibu akavua glovu na ndipo Mwalimu akarudisha kifimbo na kumpa mkono.
Iwe kweli au la, kuna somo moja kuwa Mwalimu alikuwa akijiamini na kuamini madaraka yake kama kiongozi wa nchi.
Rais siku zote ni alama ya taifa. Hata chini ya Umoja wa Mataifa, marais wote wana hadhi sawa kwa vile hakuna nchi yenye thamani kuliko nyingine duniani. Mfano mzuri ni pale Obama alipomtembelea Papa mstaafu Bendict XVI.
Hatukusikia Vatican ikifurika Wamarekani kwa kisingizio cha ulinzi wa rais wao.
Hata anapokwenda Israel au Uingereza na hata juzi Afrika Kusini hatukusikia vitu vya ajabu kama ilivyotokea Tanzania.
Kimsingi, ama Wamarekani waliamua kutudhalilisha au ni kweli kuwa nchi yetu si salama japo siku zote tuliaminishwa kuwa ni salama.
Wamarekani wanaweza kuwa na hoja hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ishalipuliwa na mabomu mara mbili tena kwenye mji mmoja wa Arusha na hakuna mhusika hata mmoja amewahi kufikishwa mahakamani zaidi ya usanii kuwa waliofanya hivyo ni ‘Wasaudia’ ambao walikamatwa na kuachiwa muda mfupi baada ya hali kutulia. Wamarekani wameamua kutwambia kuwa “mfalme yuko uchi.”
Na kweli mfalme yuko uchi. Sema tulikuwa tukihadaiwa kuwa amevaa nguo ya thamani wakati amevaa aibu tupu yaani uchi mtupu!
Tanzania haiwezi kuwa salama kutokana na ukweli kuwa tumekuwa tukisikia taarifa za wahalifu wanaotafutwa kama vile Chavda kurejea Tanzania na kuendelea kutanua huku akiwa hatakiwi nchini.
Nani mara hii kasahau kashfa ya yule mhindi Vithlani aliyeiba mabilioni ya shilingi kwa kushirikiana na wezi wa ndani walio na madaraka kwenye kashfa ya ununuzi wa dege la rais ambalo nalo haliishi mafua?
Tanzania inawezaje kuwa salama wakati wauzaji madawa ya kulevya ndio wameshika kani? Hatua gani zilichukuliwa kwa mtuhumiwa wa kutengeneza madawa feki ya kuzuia maambukizi ya ukimwi Ramadhan Madabida na mkewe? Tanzania haiwezi kuwa salama wakati ujambazi hasa wa kuhujumu umma kama kukwepa kodi umegeuka kuwa mfumo wa maisha huku serikali ikiangalia kutokana na baadhi ya wanaoiunda kuwa sehemu ya magenge ya kihalifu.
Hakika ziara ya Obama imefichua udhaifu mkubwa katika mifumo yetu ya utawala na ulinzi; na kubwa ni ukosefu mkubwa wa kujiamini na kujithamini. 
 Chanzo: Tanzania Daima Julai 17, 2013. 

No comments: