Sunday, 7 August 2016

Hapa Maguli nakupa ushauri wako mwenyewe

  Hivi karibuni vyombo vya habari vilimkariri rais John Pombe Magufuli akiwashauri makamanda wa polisi waache tamaa ya kuwakatisha tamaa polisi wa chini yao hasa wanapokamata magari ya wakubwa. Alisema, “Hata akikamata gari la IGP, hata akimata gari la rais asikatishwe tamaa.” Huu ni ushauri mzuri unaolenga kutenda haki kwa watanzania kwa kuzingatia sheria badala ya kujuana, ukubwa na mambo mengine ya kihalifu kama ilivyokuwa huko nyuma. Hapa rais lazima aonyeshe mfano na kufanya mabadiliko ya kiutandaji katika serikali yake. Pia Magufuli anapaswa kutojitoa kwenye ushauri huu; kwani naye ni kiongozi wa umma ambaye baadhi ya matamshi yake yameishaonyesha kuwakatisha tamaa walio chini yake.
Pamoja na uzuri wa ushauri wake kwa makamanda wa polisi, waswahili husema; ukimnyoshea mtu kidogo, vinne vinakuelekea wewe. Magufuli aliliona la wakubwa kuwakatisha tamaa wadogo ili kulinda uovu wa wenzao. Ni bahati mbaya kuwa hakuona upande wake kama kiongozi wa nchi ambaye matamko yake ya hivi karibuni kuwa viongozi wastaafu wanaotuhumiwa kuhujumu nchi watalindwa. Je hakikisho hili linatoa picha na ujumbe gani kwa mamlaka zinazoshughulikia ufisadi kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Je ikitokea TAKUKURU au jeshi la polisi wakagundua ufisadi wa viongozi wastaafu, wake au watoto na marafiki zao wataweza kuwashughulikia wakati bosi wao ameishatoa msimamo wake? Je huku si kuwakatisha tamaa hata polisi hao hao sawa na wale aliokuwa akiwaasa kuaacha kukatisha tamaa wa chini yao? Je baada ya Magufuli kutoa hakikisho husika, ni polisi gani awe mkubwa au mdogo anaweza kuwashughulikia wastaafu ambao wengi wao wanakabiliwa na tuhuma lukuki za kuhujumu taifa? Rejea malalamiko ya Magufuli mwenyewe kuwa nchi ilikuwa inaliwa kiasi cha kugeuka chaka la majambazi. Mifano iko mingi. Angalia wafanyakazi hewa, nchi kuingiza mafuta kwa miaka mitano bila kuwa na mita na mengine mengi ambayo hao anaowahakikisha ulinzi waliyatenda kiasi cha taifa letu kulegalega kisiasa na kiuchumi. Rejea kuumka kwa deni la taifa bila maelezo yanayoingia akilini.
 Ili kumsaidia Magufuli–kama alivyowaasa makamnda wakuu wa polisi–nasi tunamuasa kama mkuu wa nchi; asiangalie huyu ni rafiki yangu, huyu ni rais mstaafu au nini bali awakamate pale wanapotuhumiwa kuvunja sheria. Na rais hana uwezo wa kuwakamata wahusika bila kutumia jeshi la polisi na taasisi nyingine kuwachunguza kuona kama tuhuma zinazowakabili ni za kweli au la. Maana, kutowashughulikia wahusika–licha ya kuwakatisha tamaa wananchi ambao ni wahanga wa jinai waliyotenda hawa na kuwapa kiburi wahusika–ni kuonyesha mfano mbaya kuwa sheria za nchi zinatumika kibaguzi na kiupendeleo kwa kuangalia cheo na hadhi ya mtu. Kama alivyowaambia makamanda wa polisi naye aambiwe “Hata akiwa mke wa rais, tumbua; hata akiwa rais mstaafu tumbua tu.” Huu ndiyo uongozi bora na wa sheria. Kama Magufuli hatabadili msimamo wake kuhusiana na wastaafu waliovurunda basi aache kulalamika kuwa yote anayofanya yametokana na serikali zilizopita. Ajinyamazie na kufanya anapoweza na akishindwa ajinyamazie vile vile badala ya kujichanganya.
Wahenga walisema kuwa hisani huanzi nyumbani. Haiwezekani Magufuli awe na uchunguna askari wadogo wanaokatishwa tamaa na wakubwa zao wakati naye anatenda dhambi hiyo hiyo anayowatuhumu wenzake. Mpaka tunapoandika, kuna dalili kuwa tabia ya kukatisha tamaa bado haijatafutiwa dawa.  Itatafutiwa dawa mujarabu pale maafisa wote wa umma wakubwa na wadogo watawajibika kama tunavyomtaka Magufuli awajibike kwa kutowakatisha tamaa walioko chini yake wala wananchi. Huwezi kusema kwa mfano, rais Mstaafu Benjamin Mkapa anayetuhumiwa kujitwalia Machimbo ya Makaa ya Mawe ya Kiwira yeye na familia na marafiki zake kinyume cha sheria kuwa asiguswe ukawa hujawakatisha tamaa wananchi na walioko chini yako. Huwezi kusema mfano rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyeruhusu wizi wa Escrow, kufungwa mita ya mafuta, utwaliwaji wa UDA, matumizi ya fedha za umma, kuzurura ughaibuni na kuridhia uwepo wa wafanyakazi hewa asiguswe ukawa hujawakatisha umma tamaa. Huwezi kusema kuwa kashfa ya Loliondo inayomkabili rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi asiguswe wakati ana kashfa inayomkabili.
Nadhani ingefaa kama rais ataanzisha mchakato wa kushitakiana na kuitana na kuombana msamaha ili viongozi wastaafu wasamehewe kuliko kuahidiwa ulinzi dhidi ya makosa ya kifisadi na uhujumu wa taifa. Inashangaza kusikia kuwa imeanzishwa mahakama ya mafisadi wakati wakubwa wanaotuhumiwa kufanya ufisadi wakikingiwa kifua na rais. Huu unaweza kuleta hisia za ubaguzi katika matumizi ya sheria.
Tumalizie kwa kumpa rais Magufuli ushauri wake mwenyewe kuwa katika kushughulikia makosa ya jinai kusiwepo na kuangalia ukubwa, uwenzetu, uzee wangu na mambo mengine zaidi ya sheria kama sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili.

3 comments:

Anonymous said...

Salamu Mwalimu Mhango,
Uliyoyasema yote ni ukweli mtu ambao hauitaji majadala wala kigugumizi kwamba Rais wetu kuwakingia Marais wastaafu wenye tuhuma za wazi za ufisadina zinazojulikana na wananchi na imeongezea zaidi kuuweka wazi ufisadi huu mbele ya wananchi pale ambapo -anastahiki kushukuriwa na wananchi-alipotufungua macho sisi wananchi jinsi gani nchi yetu ilivyokuwa inafanywa shamba la Bibi au kichwa cha mwendawazimu kila mtu anajaribu kukifanyia ufundi.Naam Mwalimu Mhango,wananchi tulikuwa tunajuwa kwamba nchi yetu inafisadiwa katika awamu zote hizo tatu zilizopita lakini hatukuwa tunajuwa kwa hatua gani ufisadi huo ulivyofikia kilele ya kutuona sisi wananchi ni Mabwege kwa kuiona nchi ni mali yao na familia zao.

Mwalimu Mhango,tukiifuatilizia hotuba ya Magufuli ya kutoa shukurani zake kwa wanachama wa CCM kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa CCM tunakumbuka kwamba kuna watu ilibidi awashukuru katika kazi yake ya kisiasa mpaka ple alipofikia na kama si watu hao asingefikia pale alipofika,na watu hao ni Marais wote watatu wastaafu.Kwa hiyo kwa nguvu ya chama cha CCM kama nilivyokielewa katika mkutano wao wa kumkabidhi Magufuli uwenyeketi na kwa nguvu za kisiasa ambazo walizoziacha Marais hao wastaafu watatu ndani ya chama kumtaka Magufuli awasimishe wafadhili wake wa kisiasa ni sawa na kumwambia kwamba Magufuli chukua kamba hii ifunge kitanzi ujinyonge!

Kwa maoni yangu Mwalimu Mhango.ni kwamba sisi bado hatujafikia demokrasi ya ukweli na demokras ya kweli ni kuwiva kwa wananchi kidemokrasia,na kama tungekuwa wananchi wa Tanzania tumewiva kidemokarasia kweli pangekuwa hapatoshi nchini kwani wananchi wangedai haki yao ya kwamba viongozi hao waliostaafu walioifisadi nchi ni lazima wafikeshwe Mahakamani na madai hayo ya wananchi ilikuwa kwa kuungwa mkono na vyama vya upinzani au hapana wananchi hao wangedai haki yao hiyo.

Mimi nadhani kwa Magufuli kama mwanasiasa ingekuwa bora kwake kulifumbia macho swala hilo na kutia pamba masikioni bila ya kuongea chochote kuhusu Marais hao watau kwa ufisadi walioifanyia nchi,lakini kutangaza kama Rais wa nchi ambae amebeba bango la kupambana na ufisadi kwamba atawakingia kifua Marais hao wastaafu waasifikishwe mahakamani kwa kujibu mashitaka ya ufisadi ni kwamba yeye mwenyewe ni FISADI wa aina yake kwa sababu anaemtetea mwizi na yeye mwenyewe ni mwizi tu kwa aina moja au nyingine kwani huwezi kumtetea mwizi na ukampa hifadhi ndani ya nyumba yako kisha useme mimi siwapendi wezi.Kwa hiyo na tumwache Magufuli na mafisadi wake akiwakumbati ni juu yetu wananchi kudai KATIBA yetu ambayo itatupa haki ya kuwasimamisha Mahakamani viongozi hao watakaokuwa hai katika maisha yao pale siku moja CCM itakapondolewa madarakani na wananchi kwa njia ya demokrasia.

NN Mhango said...

Anon, usijali; kujibu hoja na comments za wasomaji wangu ni wajibu wangu nambari moja hasa ikizingatiwa -kama ulivyosema- ni wachache wanaotumia muda na fedha yao kusoma blog hii na kuacha michango yao ambayo pia huboresha fikra na mawazo yangu. Hivyo, sitaacha kujibu comments zozote zinatolewa na wasomaji wangu.
Ama kuhusu hili la Magufuli, naona umeeleza vizuri. Japo anajinakidi kuwa hakuhonga ili achaguliwe, kuna ukweli usiopingika kuwa kuna waliombeba. Pia, naweza kusema kuwa Magufuli anamshukuru Kikwete kwa uzembe wake uliompa fursa ya kuanza muda mrefu kujiandaa kutwa urais kama alivyofanya. Kuwashughulikia wastaafu -kama siyo woga, kujuana na kubebana, kunawezekana. Kimsingi, naona vita ya Magufuli dhidi ya ufisadi imeingia doa kwa kuwagwaya wastaafu wote wenye madoa kuanzia Loliondo, NBC, Kiwira hadi EPA, Escrow, UDA na ujambazi mwingine.
Nakushukuru tena kwa mchango wako adimu na adhimu.

Anonymous said...

Mwalimu Mhango umefungia comment yako kwa kusema haya "......
Kimsingi, naona vita ya Magufuli dhidi ya ufisadi imeingia doa kwa kuwagwaya wastaafu wote wenye madoa kuanzia Loliondo, NBC, Kiwira hadi EPA, Escrow, UDA na ujambazi mwingine"
Ukweli wa maneno yako haya si doa au dosari katika vita vyake hivi,isipokuwa historia ya kisiasa itamwandika ni rais ambae alikuja kupambana na ufisadi kwa kwa wale mafisadi UCHWARA na kuwakumbatia mafisadi wa kweli ambao wameishi wao familia zao na waramba viatu wao wakineemeka na kulala usingizi mzuri usio kuwa na ndoto za kabusi katika maisha yao.Kwa wananchi ambao hawakumbwi na ushabiki wa kisiasa katika nchi yetu watamuona Magufuli ni mnafiki tu wa kisiasa kama wangi wa wanasiasa wanafrokuwa daima.Tunakuomba rais Magufuli kama kweli unataka kuandikwa katika historia ya kisiasa kwamba ni mchukia ufisadi na umetangaza mapambano dhidi ya mafisadi basi unatakiwa kuwaua MANYANI,MASOKWE,MAGORILA NA MA-BABOONS BILA YA KUWAONEA HAYA WALA KUWATIZAMA USONI!