Saturday, 6 August 2016

Mlevi ahudhuria mkutano wa Democrat

Baada ya kuboreka na siasa za maji taka pale Idodomya ambapo Chama Cha Magamba (CCM) kilijivua nguo kwa kuruhusu akina Trump uchwara (yule mgombea wa Republican anayesifika kuwadhalilisha na kuwachukia akina mama), kujichafua, niliamua kupanda pipa kwenda zangu kwa Joji Kichaka nilipoalikwa na chama cha Democrat kuwapa ushauri juu ya kushinda uchaguzi. Pamoja na kuwa nilishatia timu Idodomya, baada ya kugundua zengwe na matusi ya akina Trump Mremavu, niliamua kwenda zangu majuu lau kupoza hasira zangu ukiachilia mbali kuunyaka ujiko.
Nilitia timu jijini Philadelphia baada ya kuwa kwenye pipa yapata kama masaa 23. Washirika zangu Hilarious Hill na Bill Kliton kunikaribisha uwanja wa ndeg. Nilikwenda moja kwa moja mkutanoni kumwaga pwenti. Tofauti na akina Trump wa Bongo aka Agust Lyatongolwa Mremavu, mwenzenu nilimpamba mwana mama Hillary badala ya kumponda kwa woga na ujinga wa kizamani.
Katika kukaa kwangu kwa Joji Kichaka na kula pizza na chicken burger na madude mengine matamu, niligundua kuwa wenzetu wademocrat wanaheshimu haki za binadamu. Wanamthamini binadamu kama alivyo bila kujali jinsia yake kama akina Trump na Trump uchwara wa bongo. Nikiwa kwenye ule mkutano niliwakumbusha wenzetu kuogopa wanasiasa wanaotumia ujinsia kutafuta madaraka na ulaji. Hawa wameshindwa na washindwe na kunyong’onyea kama Mremavu ambaye amegeuka kokoro linaloweza kuzoa chochote kijacho kwake hata kama ni uchafu.
Kitu kingine nilichojifunza ni namna wana mama wa kwa Joji Kichaka walivyo na mwamko. Trump alipowalinganisha na nguruwe walimlinganisha na nyoka mwenye sumu kali. Na ukiangalia hapa kuna mantiki–samahani ndugu zangu msiokamata kitimoto–nguruwe ana nafuu angalau analiwa na hana sumu. Je nyoka ana nini zaidi ya sumu na kutoliwa? Hivyo, Trump yoyote awe mweusi au mweupe mbongo au Mjoji Kichaka ajue thamani yake.
Kwa taarifa yenu, kama siyo kuzuiliwa na Bill, nilitaka niende zangu New York na kumfanyia kitu mbaya mpuuzi huyu mbaguzi wa wanawake, waislam, walatino, waarabu, waswahili na kila yeyote asiyekubali upuuzi wake. Eti siku zote anasema yeye ndiye anaweza kuirekebisha Marikani tena peke yake wakati biashara zake zenyewe ni mazabe matupu.
Tukirejea kwa akina Trump Mremavu, hawa wanapaswa si kukemewa tu bali kunyang’anywa ulaji na kufunguliwa mashtaka ya uhaini ambao unatokana na kuvunja katiba ya walevi.
Hakuna kitu kiliniudhi nusu nimalizie uhai wa mgonjwa Mremavu kama kuwashuku wenzake kuwa si warume kwa vile walimkimbia na kumzilia Mjengo Tulia asiyetulia. Yeye ana urume gani wakati anawasifia warume wenzake wakati kimili wanawake ndiyo wanapaswa kuwasifia wanaume na wanaume kuwasifia wanawake kutokana na sababu zinazojulikana. Mremavu aliwashangaa wenzake kususa kama wanawake bila kujishangaa yeye na uroho wake wa fisi wa kupwakia kila kijacho kwake kama mtondoo au kokoro.
Kwa Mremavu Trump kuwa mwanaume lazima uwashambulie wanawake. Ukisikia woga na kutokuwa mwanaume wa kweli ndiyo huku. Mwanaume wa kweli hawabugui wala kuwadhalilisha wanawake. Badala yake, mrume wa kweli hulinda na kutetea haki za wanawake.
Hata hivyo, sikumshangaa Mremavu tokana na njaa na usaka tonge vilivyokuwa vikimsuka kujivua nguo hadharani. Kama amemtusi mama yake, wengine kweli atawaacha? Ama kweli adui yako muombee njaa! Nani alidhani kuwa baba zima lingesimama hadharani na kusarura kama kichanga ili kuganga njaa?
Nimalizie kwa kuwaonya akina Trump Mremavu na CCM kuwa wasipoomba msamaha kwa washirika zetu wa bedroom na maza zetu tunawafanyia kitu mbaya.
Chanzo: Nipashe Jumamosi.

No comments: