Saturday, 27 August 2016

Mlevi kuwa bilionea kupitia bwimbwi

Baada ya kugundua kuwa nyavu za kupambana na uhalifu haziwagusi wauza bwimbwi na mafwisadi wakubwakubwa hasa waliokuwa marahis Mlevi nimeamua kuingia kwenye biashara ya bwimbwi tena bila kificho. Kwa vile mapapa wa bwimbwi ni untouchable, mlevi niogope nini kutia timu kwenye genge hili ili lau nami nichange njuluku ikiwezekana niwe bilionea kama Mo Jewji ambaye nilisikia akisema kuwa amejiunga na club ya mabilionea watakaogawa utajiri wao? Hakuna kilichonishangaza kusikia kuwa Jewji atagawa utajiri wake dunia nzima wakati aliuchuma kayani. Ama kweli, gabacholi wakati mwingine si wa kuamini. Sitashangaa kusikia kuwa Ugabacholini watapewa dau kubwa huku wadanganyika wakiishia kuusoma ukwasi huu magazetini.
Hakuna kitu kingine kilinkata kama kusikia kuwa na yule jambazi wa Kagoda ni bilionea wakati aliiba njuluku za walevi kupitia EPA na ujambazi mwingine. Kesho sitashangaa majambazi kama Ni Zero Kadamage yule jambazi wa Buzwagi aliyekwenda kuingia mkataba hotelini kule Uingerezani akitajwa kuwa bilionea wa Danganyika aka Bongolalaland.
Kama haitoshi, sitashangaa kusikia jambazi mwingine wa UdA ambaye hivi karibuni alibainika kuuziwa kiwanda cha mabilioni ya madafu kwa madafu milioni thelathini juu ya kugawiwa Dart naye akiingia kwenye club ya mabilionea. Hapa usisahau kuwa na mshitiri wake Riz naye siku moja ataitwa bilionea. Kwa wachumi kama mimi, natabiri kuwa Danganyika itazalisha mabilionea wengi kiasi cha kuchanganya dunia. Hapa rafiki yangu Jose Gwaijimmy, Kartortoise, Rwakatarehe, Gamanyue, Mwakasenge na wengine wanaotumia neno la Bwana kuwaibia wachovu nao bila shaka watatia timu kwenye club hii ya wakwasi.
Kwa vile nami nauzimia na kuukamia ukwasi, lazima niuze bwimbwi bila kujali kuwa vijana wetu wanaumizwa nalo. Mwanzoni nilikamia kuuza mibwimbwi baada ya kugundulika kuwa pale uwanja wa ndege wa mzee Mchonga wa Burito madude yalikuwa yanajipitia baada ya wanahizaya kuua mitambo ili kupitisha mizigo yao na wenzao. Baada ya mambo kuchenji, ilibidi nitulize boli na kusaka fursa nyingine ambayo nimeideku baada ya kuangalia historia ya trejecktori ya mapambano dhidi ya utengenezaji ukwasi wa haraka. Bandarini, kwenye mita za mafuta, mipakani, TRA, Banki kubwa na kwingineko ameziba. Kwa vile ameamua kuachia mibwimbwi iendelee kutawala, kwanini bingwa nisiiuze na kuwa bilionea?
Najua wengi wanaona kama ndoto za mchana na matokeo ya ile kitu ambayo huwa navuta. They are dead wrong. Seriously lazima nifanye biashara ya hii kitu hasa baada ya kuona wengi wakiifanya na kuibuka kwa wakwasi wa kutisha na kuogopewa kayani. Hamuoni watu wanavyoangusha mahekalu na migari ya bei mbaya kama Lungumingumi? Nani hataki kuwa bilionea kama kina Jewji na Roast Tamu?
Nina uhakika; hapa nitasepa na kupeta na kutokezea kuwa bilionea ghafla bin vu. Jiulize; tangu itangazwe vita dhidi ya ufisadi na uovu mwingine, mzungu gani wa bwimbwi ameishanyakwa na kunyea debe? Hakuna. Sasa kama hali ni hivyo, kuna haja gani kudharau mitikasi yangu ya kuuza mibwimbwi na kuukata hadi nikaitwa mtukufu, mheshimiwa, mpendwa, bilionea Mlevi mwana wa Mvuta ile kitu? Kwanini wewe unayekandia na kudharau mipango yangu hutaki kuelewa kuwa nikishazinyaka njuluku nitakuwa mwekezaji kama Kisenena ima kwa kununua makampuni kama UdA au ginneries za kuchambulia pamba tena kwa bei ya mchekea kama jamaa alivyofanya hadi kumuudhi dokta Kanywaji aliyetoa amri hivi karibuni kuwa jamaa arejeshe kiwanda lakini akagoma kumwambia arejeshe UdA na Udart aliyogawiwa hivi karibuni? Kwanini Mlevi nilaze damu wakati najua lisirikali linajichanganyasometimes  kama lilivyofanya kwenye kuigawa Udart kwa walioiba UdA badala ya kuwasweka lupango?
Kitu kingine kinachonipa imani ni ile ya kuwa kayani kwetu, ukilala apeche alolo na ukaamka bilionea, hakuna anayekuuliza ulivyochanganya njuluku haraka hivyo. Kwanini hiki kisiwe kishawishi kizuri cha wanjanja kama mimi kutgengeneza njuluk kwa njia yoyote? Danganyika aka Bongolalaland kaya nzuri sana. Angalia baadhi ya wachunaji wanavyomilki hata michopa huku wakipigapiga mikelele utadhani viongozi wa upingaji na wasifanywe kitu hata kuwauliza waeleze walivyochuma ukwasi. Kwanini mimi nilaze damu wakati milango ya kutengeneza ukwasi na kuwa bilionea chapchap kwa njia yoyote iwa halali au haramu iko wazi? My foot! Hii kitu lazima niifanye bila kujali watakaoumizwa nayo.  Mbona viwanda vya fegi vinanyonga wengi na hakuna anayejali wala kuadhibiwa? Mbona uchafuzi wa mazingira utokanao na utapishaji wa vimiminika vyenye sumu unaua wengi na hakuna anayejali? Nani hakuona mafwisadi wa Nida walivyotengeneza njuluku kwa kulangua vitambulisho ukiachia mbali kuwapa hata wasio raia? Nani anajali usawa huu kama wauza bwimbwi na waovu wengine wanaendelea kuwa mabilionea? Lazima niiuze bwimbwi ili kuwa bilionea au ikiwezekana kuazisha Kagoda namba mbili au siyo? Kwanini nisiiunde kama Kagoda one imezalisha bilionea ambaye alipaswa kuwa lupango akingojea kunyongwa?
Leo sitachonga sana. Badala yake nakwenda kusuka misheni ya kufanikisha dili la kuwa bilionea chapchap na kugeuka mwekezaji wa ndani hata kama ni mchuguaji actually.
Chanzo: Nipashe Jumapili Leo.

No comments: