Sunday, 21 August 2016

Magufuli ataibadili CCM au itambadili?

            Rais na mkiti wa CCM, Dk. John Magufuli amekaririwa mara nyingi akilaumu serikali iliyopita kwa kulegalega na kuruhusu uhujumu wa taifa. Amekuwa akisikika mara nyingi akisema; Tanzania ilikuwa imegeuzwa shamba la bibi na genge la watu wachache tokana na ufisadi na uzembe wa wale waliomtangulia. Hata hivyo, jambo moja linawashangaza wachambuzi wengi.  Pamoja na Magufuli kufichua na kulaumu uoza wa watangulizi wake, ameahidi kuwalinda wananchi walipomtaka awafikishe mahakamani. Tokana na hili, Magufuli anawapa taabu walio wengi kuamini kama anasema atakachotenda na kutenda atakachosema bila upendeleo, huba wala ubaguzi wakati ameishaonyesha upendeleo wa wazi kwa watangulizi wake wenye madhambi lukuki.
 Tujiulize; je hiyo serikali iliyolegalega ikaruhusu hujuma kwa taifa iliundwa na chama gani kama siyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichopewa kuiongoza? Je kuna namna Magufuli anaweza kufanikiwa kuibadili Tanzania bila kuibadili CCM? Je Magufuli ataweza kuibadili CCM au itambidili?
Kwa wanaochunguza mwenendo wa Magufuli na timu aliyo nayo, kuna uwezekano CCM kumbadili.  Kwa mfano, wapo wanaoshangaa mantiki ya kubakisha sekretarieti ya CCM iliyosimamia madudu haya yote. Pia, wapo wanaoshangaa mantiki ya kumuacha mtendaji mkuu wa CCM, yaani Katibu Mkuu, Abdrahaman Kinana ambaye aliwahi kutuhumiwa kuhujumu taifa ukiachia mbali kusimamia chama dhaifu na fisadi hadi kilipokabidhiwa mikononi mwa Magufuli. Kampuni ya Kinana imewahi kutuhumiwa kusafirisha nyara za umma.   Nadhani hii ilitoshe kumwashia Magufuli taa nyekundu na kutombakiza kwenye nafasi nyeti chamani.
 Hata hivyo, wapo wanaotabiri kuwa Magufuli ametafuta fursa ya kukifumua chama kwa kumbakisha Kinana akitafuta fursa ya kupata mtu anayefaa. Wengine wanakwenda mbali na kutabiri kuwa Kinana ataondoka kama aliyekuwa Katibu Kiongozi, Ombeni Sefue baada ya Magufuli kumbakisha na akamtumbua baadaye baada ya kupata mtu wa kufaa kwenye nafasi yake. Tunaweza kusema bila wasi wasi kuwa dirisha la kuibadili CCM kabla ya kumbadilisha Magufuli unaweza kuliona kupitia kuendelea kuwepo kwa Kinana ambaye–pamoja na kusifiwa kukiendesha chama–ukilinganisha matarajio ya watanzania kwa chama tawala, huoni cha mno kwa Kinana kuendelea kuwa mtendaji mkuu wa CCM ile ile aliyoiacha ikatekwa na kutwaliwa na mafisadi na magenge ya wahalifu.
Kadhia nyingine inayoonyesha kuwa hadi sasa CCM imembadili Magufuli kabla hajaibadili inahusisha makada wa CCM wenye tuhuma mbali mbali za kifisadi kama vile uuzaji mihadarati, wizi wa mali za chama na umma, uzembe, kujuana, matumizi mabaya ya fedha za umma, ubinafsi, na kadhia nyingine nyingi tena wanaojulika.
Bado Magufuli hatajatangaza kifo cha mitandao ya kifisadi iliyokidhoofisha chama kiasi cha kugeuka kama club ya matajiri kutumia kuliibia taifa.
Kimsingi, bila kukifumua na kukisuka upya chama–jambo ambalo, hakuna shaka, Magufuli anaonekana kukamia kutenda–ataishia kubadilishwa na CCM na kuwa kama wale ambao sasa anawalaumu kwa kukwamisha taifa letu chini ya siasa chafu na za kichoyo za kujuana na kujihudumia kama ilivyokuwa kwa miongi mingi tangu aondoke baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere mwaka 1985.
Tuseme wazi; ni mapema mno kupitisha hukumu kwa Magufuli japo si vibaya kuanza kuiandaa kulingana na kutokana na namna anavyopambana na matatizo sugu ndani ya chama na nchi.  Kwanza, ni kutokan ana ufupi wa muda. Magufuli hajatimiza hata mwaka tangu aingie madarakani kama rais wa Tanzania ukiachia mbali kuwa kwenye uenyekiti wa CCM kwa mwezi mmoja tu.
  Pili ni ile staili yake ya kutotabirika kirahisi. Wapo wanaoona kuwa Magufuli amejipa nafasi ya kuisoma mifumo ya ndani ya CCM ili kuweza kujua namna ya kukibadili chama kabla hakijambadili; hasa ikizingatiwa kuwa CCM ni taasisi kubwa ambayo imechafuka kwa muda mrefu. Hivyo, si busara kukurupuka na kuanza kufyeka kila kitu bila kujua undani na mbadala wake. Muhimu ni kumbukumbusha Magufuli–ambaye watanzani wengi bado wana imani naye–kuwa timming na muda katika uongozi ni jambo muhimu sana. Kama Magufuli atachelewa kuchukua hatua za kukibadili chama, uwezekano wa kubadilishwa ni mkubwa kuliko kukibadili chama.
Tatu, kutokana na uoza wa muda mrefu wa kimfumo, uwezekano wa Magufuli kuchukua muda mrefu kutimiza anayotaka kutimiza ni mkubwa hata ikiwezekana kumaliza muda wake bila kukamilisha kazi anayoanza kwa chama na taifa.
Nne, kitakachoamua kama Magufuli ameibadili CCM au imembadili ni matunda ya kazi yake. Hapa lazima tuwe wazi. Magufuli anaweza kufanikiwa kutekeleza anayoamini yatabadili mfumo mfu na fisadi uliojengeka kwa zaidi ya miongo mitatu. Ingawa, anaweza asikidhi matarajio ya watanzania kutokana na kuchoswa na kuumizwa na mfumo huu.
Tano na mwisho, vyovyote itakavyokuwa, Magufuli ataacha CCM mpya kulinganisha na ile aliyokabidhiwa ikichungulia kaburi. Rejea kutetemeshwa na kada wake, waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyepambana na Magufuli kwenye uchaguzi mkuu akiibuka mshindi wa pili kwa kura 6,072,848 sawa na aslimia 39.97 ya kura zote dhidi ya kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 ya kura zote (BBC, Oktoba 30, 2015). Unaweza kuona kuwa hapa hapakuwa na ushindi wa kishindo wala wa ki-Tsunami kama ilivyozoeleka.
Kwani mwaka 1995 Jakaya Kikwete alipata jumla ya kura 5,276,827 ambazo ni sawa na asilimia 61.17 ya kura zote zilizopigwa (BBC, 5 Novemba, 2010).
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

1 comment:

Anonymous said...

Itambadili
Mafisadi mchezo