Wednesday, 10 August 2016

Kijiwe chakumbushia Escrew, Lingumi na UDA

Image result for lugumi
          


Baada ya kufumka kashfa funga kazi kwenye utwahuti sorry utawala uliopita baadhi zikwa ni Escrew, Lingumi na UDA, na kunyamaziwa, wengi walidhani ujio wa dokta Kanywaji Joni Makufuli kungefanya mambo tofauti na upuuzi uliopita. Kadri siku zinavyozidi kuyoyoma na wachovu kusahaulishwa, kuna kashfa zinaonekana kuanza kuminywa kinamna kama siyo kufichwa ili wachovu wasahau kabisa waendelee na madili.
Mgosi Machungi aliyerejea hivi kaibuni kutoka Ushoto ndiye analianzisha. Anasema huku akiwa ameshikila kichwa kwa huzuni, “Mwenzenu pamoja na kuwaetea saamu toka kwa wagosi, kuna kitu kimoja kiinitia aibu kwei kwei.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchomekea, “Ulifumaniwa nini?”
“Wewe Mbwamwitu acha utani. Unazani Ushoto kuna kufumaniana au kupigana zongo? Usidhani kue mambo yanafanyika Kizaramizi kama hapa ndugu yangu. Kiichonitia aibu ni kugundua kuwa watu wa vijijini wanajua mambo mengi ya maana kwa kaya kuiko sisi wa mjini,” anajibu Mgosi
Kabla ya kuendelea, Mipawa anamchomekea tena, “Una maanisha nini mbona hueleweki Mgosi? Eti washamba wa kwenu wanajua mambo mengi kuliko sisi watoto wa mjini siyo? Ya kweli hayo Mgosi?”
“Usiwe na haaka utanieewa tu. Je wajua kuwa niipofika kue kia mmoja aikuwa akiniiuizia uipofikia uchunguzi wa kufunga hata kunyonga majambazi ya kashfa za Eskow, Ingumi na UDA? Kusema ukwei sikuweza kupata jibu hasa ikizingatiwa kuwa wengi tiishasahau kashfa hizi. Sijui hata kama Dokta Kanywaji anazikumbuka,” anajitetea Mgosi.
“Kama hii ndiyo mada yako, Mgosi hapa una mashiko. Kuna ukweli japo si wote kwenye mada yako kuwa watu wa mjini wakati mwingine ni wasahaulifu kuliko wa vijijini kutokana na kuwa na unafuu wa maisha. Tunaumeme wa kumwaga siku hizi baada ya kuingia dokta Kanywaji. Wengine wanafaidi maji yaliyokuwa yameadimika miaka mingi kiasi cha kuwa bize na wengine kuridhika wasijue mapambano ya haki ni suala la kudumu na kufa na kupona,” anasema Msomi Mkatatamaa huku akibwia kahawa yake.
Msomi anaendelea, “Ni jambo la kushangaza na la kweli kuwa majipu uliyotaja yanaonekana kuanza kumshinda daktari wa majipu. Sijui kuna wanene zaidi nyuma ya majipu haya hasa wale aliowaahidi ulinzi kwenye madhambi yao au ni woga tu.”
Kanji anadakia na kusema, “Veve hapana iko saka dugu yangu. Rahis nasema takamata fisadi vote na funga. Patia yeye nafasi tafunga tu. Pia mimi ona rahis hapana veza kamata fisadi vote. Sasa kama fisadi ile kuba nakula na fisadi kubakuba ya siasa, ikotegeme veve funga yeye?”
Kapende anamuunga mkono Kanji, “Kanji nakubaliana nawe hasa ikizingatiwa kuwa ufisadi kayani haufanywi na watu wasio na ushirikiano na wakubwa. Ima ni ndugu, wake, zao au wao wenyewe kama si wateule wao. Tukizingatia kuwa kashfa tajwa hapo juu ziligusa wakubwa wengi tokana na utawala wa wakati ule wa kujihudumia, sidhani kama zitaguswa.”
Mpemba aliyekuwa kimya muda mrefu anakula mic, “Ami usemayo ni ya kweli tupu. Kama wale walobainika kuwekewa mabilioni kwenye akauti zao bado wamo bungeni wategemea huyu Kanywaji awafanye nini? Huoni akina Joni Chenga, Profwedheha Ana Kajuamlo, Ngeleza na wengine wanaendelea kutesa mjengoni?”
Sofia Lion aka Kanungaembe, “Hata nami ami hapa kanishawishi,” kabla ya kuendelea Mbwamwitu anachomekea, “amekushawishi vipi na ili iweje?”
Da Sofia hajibu; anaendelea, “Nikiangalia UDA yenyewe ilivyotolewa kama zawadi kwa wezi wale wale waliobainika kuitwaa kinyume cha sheria eti kwa kisingizio kuwa hakuna mzalendo mwenye uwezo wa kuendesha miradi mikubwa. Kwani kinachotakiwa hapa ni kufanya biashara yenye faida au kupeana ulaji kizawa? Mzawa mgeni na yeyote kama ni fisadi ni fisadi tu.”
Mipawa anakula mic tena, “Kaya hii kwa ufisadi mimi sina hamu. Umesikia juzi waliotumbuliwa baada ya kupenyeza watu wao kwenye msafara wa marubani ulioendea ndege mpya kule Kanada? Yaani watu hawamwogopi dokta Kanywaji! Ndege zenyewe hazijatua mmeishaanza kuzifanyia kitu mbaya kama mlichoifanyia Air Tanzia siyo?”
“Hata hii imenishangaza. Huu ni ushahidi na motisha kwa dokta Kanywaji kuwa kazi iliyoko mbele yake ni pevu kweli kweli. Kwani, wengi waliomzunguka ni wale wale walioifikisha kaya hapa. Hivyo, changamoto kama hizi zinapaswa kumfumbua macho kujua kuwa wengi wa mafisadi anaopaswa kuwatumbua wamo nyumbani mwake,” anaongezea Msomi Mkatatamaa.
“Tena Msomi umenikumbusha. Nilisoma mahali kuwa kuna mpango wa kuwatumbua vilaza na vihiyo. Hata hivyo, nina shaka sawa na ilivyo kwa kashfa kama hizi tajwa. Kwani nikiangalia vilaza kama Bill Lukuuvii bado vimo kwenye sirikali ya dokta Kanywaji. Je ina maana hajui kuwa huyu jamaa ni jipu na kihiyo ambaye alitajwa kwenye kitabu cha mafwisadi wa elimu au ameendekeza urafiki na kujuana kama si kufanya utumbuaji kibaguzi?” analalamika Kapende huku akiweka kamera yake vizuri mezani.
Kijiwe kilipokuwa kinanoga si wakapita majambazi wa Lingumi, UdA na Escrew wakitoka kwenye kikao cha kumzidi kete dokta Kanywaji. Acha tuwatoe mkuku ili kuwakamata na kuwafanyia kitu mbaya hadi wake zao waapige karata baada ya kujua hiyo kitu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

2 comments:

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,
Katika ufunguzi wa makala yako hii umeandika:"Baada ya kufumka kashfa funga kazi kwenye utwahuti sorry utawala uliopita baadhi zikwa ni Escrew, Lingumi na UDA, na kunyamaziwa, wengi walidhani ujio wa dokta Kanywaji Joni Makufuli kungefanya mambo tofauti na upuuzi uliopita. Kadri siku zinavyozidi kuyoyoma na wachovu kusahaulishwa, kuna kashfa zinaonekana kuanza kuminywa kinamna kama siyo kufichwa ili wachovu wasahau kabisa waendelee na madili""

Kwa uhalisia wa mambo katika nchi ya kwetu ambayo iekuwa katika ufisadi kwa miaka yote hii 30 naamini kabisa kwamba wakubwa wote walioshiriki kuifisadi nchi yetu watampa magufuli wakati mgumu katika utekelezaji wake huo wa kupambana na ufisadi na mafisadi kwa hiyo mbinu hii ya kisiasa inaweza ikatumika ya KUWASAHAULISHA WACHOVU NA KUMINYWA KINAMNA na hatimae kuanza kufifia kabisa kwa kashfa hizo na hatimae kubaki tu katika historia ya nchi yetu kwani kutakuwa na watu ambao watapewa maelekezo ya kuhakikisha kwamba kasha hizo haziibuliwi tena kisiasa aidha watu hao wakiwa wa vyombo vya habari,waongeaji wa kisiasa katika majukwaa mbali mbali tukiachia vyama vya upinzani ambao watachukuliwa tu kwamba wanapiga makelel ya mbwa ambayo hayawezi kuisimamisha garimoshi la CCM lenye mabehewa ya kashfa hizo kuendelea na safari yake.
Na hadhari aliyoihadharisha Mipawa pale aliposema
“Hata hii imenishangaza. Huu ni ushahidi na motisha kwa dokta Kanywaji kuwa kazi iliyoko mbele yake ni pevu kweli kweli. Kwani, wengi waliomzunguka ni wale wale walioifikisha kaya hapa""
Kwa hadhari hii Rais wetu anatakiwa kuwa na hadhari kubwa kwani watu hao watampa wakati mgumu Magufuli kuitekeleza kazi yake kwani bado wao wapo royal zaidi kwa maboss wao kuliko boss waliekuwa nae sasa.Na tuzidi kumuombea Magufuli wepesi wa utekelezaji wa kazi yake hii ambayo ina bahari saba sama walivyosema wahenga.

NN Mhango said...

Anon, sitaki nivuruge mawazo yako na uchambuzi wako wa kifungu hadi kifungu. Japo mambo yameandikwa kilevi, yana ukweli unaoogopewa na wengi. Naweza kusema kwa ufupi kuwa nakubaliana nawe kuwa kama Magufuli ataendelea kuwakingia kifua wastaafu na magenge yao ya ujambazi, ataishia kuambukizwa majibu badala ya kuyatumbua. Siku nikipata fursa nitaizamia hii kwa utuo kama ulivyozamia makala hii.