Tuesday, 1 August 2017

Kanji ageuka Tunduni Liisu wa Kijiwe

Image result for photos of tundu lissu
            Baada ya rais John Kanywaji kumtia kashkash rais Tunduni Liisu wa Kaya Legal Society, kijiwe kimejikuta kikivutwa kwenye kimbembe hiki kisicho na faida kwa kaya bali kuendelea kuzorotesha demokrasia. Hivyo, kama kawa, kijiwe kimeona kitie guu lau kuepusha sintofahamu isiyo na kichwa wala miguu kayani.
            Mpemba leo ndiye analianzisha “yakhe mliona jana Tunduni Liisu alivopokelewa kishujaa utadhani Mandela? Wallahi sikujua kuwa kumbe wachovu wa kaya hii bado hawakubali kuwekwa nfukoni na yeyote hata awe na manlaka kiasi gani.”
            Kapende anajibu “unaongelea siasa za majitaka na woga siyo? Hii picha nami niliiona; na ilivutia sana japo nilifarijika sana kugundua kuwa bado tuna waja wasioogopa yeyote pale wanaposimamia wanachoamini. Sijui kwanini hawa wasiotaka kukosolewa; hata wanapokosea wazi wazi hawakutwambia kwenye kampeni za kampani ya ulaji wa dezo kuwa tukiwapa ulaji wangetaka tugeuke mabubu na mabunga wanayoweza kutenza watakavyo. This is too bad and sad. Acha nichapie kimombo hata kama ni broken kama wale ambao naamua kuwahifadhi kwa leo.”
            Mgoshi Machungi anamchomekea Kapenda hata kabla ya kumaliza na kusema “hata sisi tinashangaa namna wanavyotaka kutifanya hamnazo wasijue nasi tinazo tena zinazochemka kuliko akina Bashite. Sijui kwanini wanapenda kutwanga maji wakitegemea kupata unga. Hivi kwei unaweza kugeuza kaya nzima mabubu na mabunga ukafanikiwa? Subutu. Titasema na kusema na kusema ii muladi tisemacho kiwe na mashiko na kwei tupu. Wanapaswa kujua kuwa sisi ndio timewapa madaaka wanayotaka kutumia kutiumiza na kutinyamazisha.”
            Kabla ya kuendelea Kanji anakwanyua mic “sasa kama hapana taka sisi kose vao, kwanini nakosea? Kwani vanata midomoni yetu iwe ya kula tu? Naweza zuia vatu tembea, andamana kazalika kazalika. Lakini hapana weza funga domo yao. Naveza funga miili yao lakini hapana veza funga domo yao. Hapana nalipa kodi kwa zungumza.”
            Kabla ya kuendelea Mijjinga anamwagia Kanji ujiko “Kanji leo umenizingua; na nimekukubali kinoma mshirika wangu. Ama kweli wewe ni Tunduni Liisu wa kijiwe kuanzia leo! Unaogea utadhani yule mwanafalsafa wa Kiyunani aitwaye Pilato!”
            Kanji hajivungi. Anajibu huku akitabasamu “hapana dugu yangu. Mimi pata vapi Tunduni Liisu. Ile iko rais wa sharia na inasoma sharia sana. Mimi iko mtu dogo sana kama veve. Veve nataka mimi iwe Tunduni ipelekwe pango Swahili gombea mimi? Kama nataka Tunduni Liisu basi mimi changua Gosi.” Anamuangalia Machungi ambaye naye anamtolea macho Kanji.
Kijiwe hakina mbavu namna Kanji anavyoogopa kwenye lupango akiogopa wakware wasimgombee kama mpira wa kona.
            Mgoshi hamkawizi Kanji. Anakula mic “sasa ndugu yangu Kanji hainitakii mema. Hata kama nikifungwa sitapata wasiwasi; hasa ikizingatiwa kuwa mimi ni mwamba asiyeweza kuchezewa wala kutishiwa na wakware vinginevyo ninaweza kupiga mtu zongo. Hata hivyo, wewe unafaa. Si unaona uivononanona na kuvutia?” Kijiwe hakina mbavu tena kwa namna wawili hawa wanavyowashana.
            Kabla ya vicheko kuisha, Msomi Mkatatamaa anatia guu. Anazoza “naona pendekezo la baadhi yetu kuwa kama Tunduni, kama alivyomwita Kanji, limestua wengi. Hapa hakuna cha kuogopa hasa ukijua na kuamini kuwa unachosimamia ni sahihi bila kujali unampinga au kupingana na nani. Kaya hii ni mali yetu sote na si mali ya wakubwa wenye kutaka kutopingwa kana kwamba wao ni Mungu wakati ni waja wa kawaida wenye mapungufu lukuki. Anachofanya Liisu ni ushahidi kuwa yuko mbele hatua moja kuliko hao anaowapinga; nao wakaingia mkenge na kumpandisha chati.”
            Kabla ya kuendelea, Mheshimiwa Bwege anakatua mic “usemayo msomi mwenzangu ni kweli tupu; na mambo nyeti sana. Hakuna kinachonishangaza, kunisikitisha na kunitisha kuona wababe wakiita wanyenyekevu ukiachia mbali waliovuruga kujifanya hawahusiki na uoza unaowafanya wawalazimishe wengine kutowapinga. Sisi siyo mbuzi au hayawani ambao huwa hawabadiliki wala kuwaza kwa kwenda mbele. Hivi inakuwaje waja wanaoonekana kuwa na welewa tosha kumkata Tunda na kumpeleka lupango ili akaeneze sumu kule kama alivyofanya dogo Godbariki Lemaa? Sijui kama wanamkomoa Tunda zaidi ya kujidunga kisu wenyewe tokana na ugumu wa kuelewa.”
            “Kaka unataka kusema kuwa kinachofanyika ni kupanda mbegu ya mapinduzi bila kujua; au tuseme kibri cha kawaida cha ulaji kimesababisha upofu kiasi cha wahusika kujidunga kisu bila kujua?” anauliza Da Sofia Lion aka Kanungaembe.
            Mipawa aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kutia guu “ da Sofia hili liko wazi kuwa wakati mwingine maulaji hulevya na kupofusha kiasi cha waathirika kushindwa kuona vitu vya wazi kama hivi. Huoni mzee wa uvivi wa kufikiri anavyoadhirika kwa sasa baada ya kulewa maulaji hadi akajifanya mjuvi na muungu wakati kichwa chake kinatia shaka! We ngoja tu. Time will accurately tell one day. Kwa taarifa yenu kaya imejaa akina Tunda sema hawajajitokeza kutokana na kutokuwa na nafasi za kufanya hivyo.”
            Kijiwe kikiwa kinashika kasi ukapita msafara wa Tunda Liisu! Acha tumshangilie na kumtaka aje tumpe ofa ya gahawa bila kujali kama njagu wangenuna au kutaka kututembezea virungu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
 

No comments: