The Chant of Savant

Wednesday 23 August 2017

Serikali ieleze ukweli kuhusu kukamatwa ndege


Image result for photos of ndege bombardier
               TAARIFA kuwa ndege yetu iliyokuwa itue nchini kutoka nchini Canada ilikonunuliwa imezuiwa kutokana na deni la mkandarasi, zinatia kichefuchefu, kuudhi na kuzua maswali mengi zaidi ya majibu. Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alidai kuwa ndege yetu imeshikiliwa kutokana na
kuvunja mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Wazo Hill hadi Bagamoyo baina yake na Kampuni iitwayo Stirling Civil Engineering Ltd inayoidai serikali dola milioni 38 na ushei. Kuna mambo ambayo serikali inapaswa kuyaweka wazi. Je, Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ni mali ya nani na kama si kampuni ya Kitanzania iliingiaje nchini au ni yale yale ya PAP, IPTL na madudu mengine? Maswali hayaishii hapa. Je, kwa nini serikali imekuwa kimya na inapoongea inatoa majibu ya kukanganya? Kunani hapa? Mkweli na
muongo ni nani katika sakati hili? Baadhi ya majibu unaweza kuyapata kwa kusikiliza maelezo ya wahusika. Mfano,  Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alikaririwa akisema bila kukiri au kukanusha akisema: “Ninachojua ndege itakuja. Katika makubaliano ilitakiwa ifike Julai, lakini ratiba zao kwa miezi miwili ijayo hadi Oktoba, ndege itakuwa tayari na itakuwa imeshakamilika, ukweli utajulikana baadaye. Wasipoleta watakuwa wame-breach contract (wamekiuka mkataba).” Mbali na Ngonyani, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa, alikaririwa akisema: “Serikali ilipata fununu mapema kwamba kuna baadhi ya viongozi wa siasa walikuwa nyuma ya mpango huo na sasa wamejidhihirisha wazi kuwa wao ndio wapo nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za serikali kwa masilahi yao.” Haya si majibu ya suala linaloongelewa. Hata kitendo cha Kawawa kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kinazidi kuiweka serikali pabaya. Alikiri kuzuiwa kwa ndege hiyo. Badala ya kutoa ufafanuzi wa kina yeye alijielekeza kwenye kutupa lawama zisizo na mashiko kiasi cha kutia shaka uwezo wake wa kuelewa mambo, ukiachia mbali kuitetea serikali yake. Sijui kama mhusika ana sifa zinazotakiwa kwenye wadhifa wake.
Maana, ukisikia maelezo yake, unajenga shaka. Naye Lissu anasema: “Kampuni ya Stirling ilikubali kuweka masharti nafuu ili Serikali isilipe deni kubwa, lakini serikali yetu ikakataa.” Si Ngonyani wala Kawawa aliyekanusha hili. Je, hapa anayehujumu nchi ni nani kati ya wale  wanaosema ukweli na wale wanaokalia ukweli ukiachia mbali kukalia kesi wakati wakijua madhara yake kwa taifa? Je, hapa nani anaudanganya  umma na kwa nini? Je, kama ukweli utajulikana na tukakuta kuwa kweli ndege imezuiliwa kutokana na kesi husika hawa wanaotudanganya watajiwajibisha au kuwajibishwa? Je, Watanzania watakubali kuendelea kuwa na watendaji wasiowajibika kikamilifu kila jambo linapotokea? Je, watakubali kuwaambia wahusika wawapishe watu wenye kujua umuhimu wao kwa jamii na kueleza ukweli kwa kila jambo lenye masilahi kwa taifa bila kuhofia vitumbua vyao? Napenda nitoe ushauri hasa kwa Kawawa na wengineo walioshiriki kwa namna moja au nyingine kutufikisha hapa tulipo. Wajipime kwa waliyosema na wachukue uamuzi mgumu. Maana, kila kitu kiko wazi. Muongo na msemakweli wanajulikana katika kadhia hii. Nadhani mojawapo ya sababu za taifa letu kuchezewa ni kuwa na watendaji kutojiamini. Hivi Kawawa angekuwa mwanasheria aliyekabidhiwa kushughulikia kesi hii tungetegemea nini? Je, wapo kina Kawawa wangapi kwenye ofisi nyingi na nyeti za umma? Mbali na maswali haya hapo juu, kuna maswali mengine ambayo serikali inapaswa

kuyatolea majibu. Mfano, je, muda wote huu serikali ilikuwa ikifanya au kungoja nini? Je, ni kwanini mkataba husika ulivunjwa? Nani waliingia huu mkataba? Je, nini kifanyike?Nadhani tulivyochezewa kama taifa ifikie mahali itoshe. Hapa lazima tukubali kubadilika haraka vinginevyo tutazidi kuumia bila sababu za msingi zaidi ya ujinga na ubinafsi. Hapa lazima serikali iwasake na kuwawajibisha walioingia mikataba hii ya kijambazi; na wale walioivunja bila kuangalia madhara ya kufanya hivyo. Pia lazima tukiri kuwa mfumo wetu wa uendeshaji nchi si mzuri kwenye maeneo fulani fulani, ni lazima tuubadili kutoka kwenye hali tuliyonayo hadi tunakokutaka. Kila kitu sasa kinategemea jitihada na usongo binafsi vya rais badala ya kuwa na mfumo unaojiendesha bila kutegemea jitihada binafsi. Nimalizie kwa kusema; ushikwapo shikamana; wahenga waliasa. Serikali ya Magufuli haina haja ya kunyamaza au kukwepa ukweli wakati hasara husika ilisababishwa na serikali iliyopita. Ieleze Watanzania kinachoendelea hasa ikizingatiwa kuwa fedha zinazotumika kununulia ndege na ndege zenyewe ni za Watanzania ambao kina Kawawa wanajitahidi kuwaweka sawa. Watanzania wana haki ya kuambiwa na kujua ukweli, kuhoji na kutaka waliohusika na kadhia hii wawajibike  kisheria ili kuwa somo kwa wengine. Hii nchi ni mali yao na si mali ya serikali wala yeyote zaidi ya wao wenyewe. Serikali ya Magufuli haiwezi kubeba lawama zote hasa ikizingatiwa kuwa kadhia hii ilianza kabla ya kuingia madarakani. Hata hivyo, haiwezi kuachwa jumla. Tangu iingie madarakani na kujua kuna kesi kwanini ilikaa kimya au ilichukua hatua gani? Haya ndiyo masuala ya kuangalia ili kuondokana na mazoea ya mafisadi na majizi wachache kuendelea kuuibia umma wa watu wetu maskini. Je, ukweli kuhusiana na kukamatwa kwa ndege yetu huko Kanada?
Chanzo: Tanzania Daime J'tano leo.

No comments: