Sunday, 6 August 2017

Mlevi kurejea kuingiza bwimbwi kayani

 
            Baada ya kuisha kwa kashfa ya Bashite na masuala ya kughushi, kuzikwa na mambo kutulia, mlevi napanga kuendelea na kuingiza bwimbwi kayani. Nilisitisha kidogo siku zile nikawa nauza shisha baada ya jamaa kuvamia sakata jingine. Nafanya hivyo kwa kuzingatia kuwa huku kayani mambo hufanyika kisanii tena kwa nguvu ya soda ili ima kupata kiki au kuepusha zali kama ilivyokuwa kwa bashitegate. Mbali na hili, baada ya kugundua kuwa kuna njemba ziliingiza vichwa kibao vya treni kayani, nikajua njia iko wazi kwa kuingiza mizigo. Hapa sijaongelea kuomba kibali cha kushukia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzee Mchonga sehemu ya VIP ili kuficha madude yangu. Kaya inapobakwa na kunajisiwa unategemea nini? Sijui kama mswahili tena mkimbizi wa kiuchumi anaweza kwenda kwenye kaya yoyote ya kigabacholi akaruhusiwa kuingilia VIP launge. Hata hivyo, watahofu nini wakati tuliwapa Asajile Mwaijumba yote sisi tukabaki kubana kwenye madaladala na madongo-poromoka Uswazi tokana na ubunga wetu kama wabongo na kaya nzima ya Danganyika wakati wao wakiendelea kutanua katikati ya miji tangu kupata uhuru?
            Naona yule anacheka na kutikisa kichwa akidhani natania au kuongea kilevi. Sitanii wala sijalewa wala kuvuta. Nazoza ukweli mtupu. Kama hujui kaya hii njoo uniulize mie nikupe darasa la dezo. Kama unadhani nayasema haya tokana na kanywaji na mibangi jiulize: akina Lungumi waliopiga mabilioni ya madafu wako wapi zaidi ya kuendelea kupeta? Nenda kawatembelee akina Saimo Group pale uone wanavyoendelea kupiga njuluku huku walevi wakiachwa kwenye mataa.  Kama haitoshi, nenda kawatembelee akina Roast Tamu la Aziz wa Kagoda s/o EPA ambayo tunaambiwa walioiasisi tuwaache waendelee kufaidi. Hivyo, ninaposema kuwa narejea kuingiza bwimbwi, I am dead serious kwa lugha ya nyumbani.
            Leo nitaongea kwa kutoa ushahidi kwa kila pwenti ninayotongoa. Wanaodhani kuingiza bwimbwi itakuwa vigumu wajiulize: nitashindwaje kuingiza bwimbwi tena linalofichwa hata tumboni wakati wageni wanaingia kayani kana kwamba mipaka yetu haina walinzi wala waja wenye akili timamu? Niko nafanya utafiti kugundua kuwa kama zile mashine alizostukia dingi sometimes back pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzee Mchonga zimeisharekebishwa. Pia, nafanyia research zile scanners za bandarini zilizoshindwa kujua vichwa kibao vya treni nione namna ya kuingizia bwimbwi pale.
            Hakuna haja ya kutilia shaka mpango wangu huu tokana na ushahidi niliotoa. Nitatoa mwingine wa ziada. Kama twiga na wanyama wengine wakubwa walipitishwa KIA, nitashindwa nini kupitisha bwimbwi? Jiulize. Tangu soo hii itokee, ni wahalifu wangapi wametupwa lupango angalau wakalala kule kwa miezi halafu wakacheza na ndata na waendesha mashtaka wakaachiwa kama wale wa juzi pale bandarini? Kusingekuwapo siasa za kutafuta kiki na zimamoto, masuala kama haya yangefanywa yawe ya kudumu. Kila kuchapo mwaletewa picha mpya na kusahau ya zamani kama watoto halafu mnakosoa mpango wangu wa kisomi? Isitoshe, mnaposhindwa kubadili mfumo mkategemea usongo wa dingi pekee mjue hakuna mnachofanya zaidi ya kutwanga maji au tuseme mnafanya kale ka nchezo ka chamaki nchanga aka panya kukimbiza nkia wake. Atankamata? Subutu!
            Ukiachia mbali kujiridhisha tokana na utafiti wangu, nina wasi wasi gani wakati sheria za kaya ni drug friendly ikilinganishwa na umangani na China wanakotoa adhabu ya kunyotolewa roho hadi kufa? Hapa unakamatwa na kutembeza njuluku na kupigwa mvua chache kabla ya kuchomoka kwa msamaha wa dingi. Hata hivyo, kwa dingi wa sasa, huu uchochoro ni kama hakuna. Hata hivyo, yeye si anachomekewa majina ya kusamehe. Ndiyo maana nasema bila kubadili mfumo ni kama tunajidanganya kama siyo kujipa matumaini.
            Juzi nilikuwa naongea na bi mkubwa wangu ambaye ni mwanasheria. Alinihakikishia ufanisi kwa vile wakubwa wamekatalia suala la kubadili katiba kwa kurejea mchakato wa katiba mpya ya kaya ambayo iliuawa na mafisadi waliochelea kustaafu na kunonihino kwenye debe kule lupango. Wakati mwingine natamani kaya yetu ingekuwa kaya kama zile za Brazil, Korea ya Kusini au Pakistan ambapo juzi mapilato walimtimua waziri mkuu baada ya vitegemezi vya kugundulika vilipiga njuluku na kuficha kule Panama.
            Baada ya kufanikisha dili na kurejea kwenye biashara ya bwimbwi, napanga pesa itakayopatikana nifungue chuo kikuu cha Mlevi University of Science and Technology (MUST).
Chanzo: Nipashe J'mosi Jana.

No comments: