Tuesday, 8 August 2017

Kijiwe chashangaa akina Chauda kumilki kaya

            
            Baada ya dingi kuwaijia juu wachukuaji waitwao wawekezaji waliohodhi ardhi ya kaya, kijiwe kimekaa kama kamati kudurusu hali hii.
            Mgoshi Machungi ambaye amerejea toka Tanga alikohudhuria mojawapo ya mikutano ya dingi analianzisha “wagoshi muiisikia namna dingi aivochukia kukuta mashamba kue kwetu yakimiikiwa na wahaifu tena wakifugia nyoka? Hapa kwei amenikuna kwei kwei; na namipongeza sana kwa kuiona hii.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba anchomekea Mgoshi “yakhe ankukuna wapi na vipi mboni hatukuelewi? Maana wewe uchukiavo hili neno nashangaa kuona unavolitumia tena dhidi yako mwenyewe; kunani Mgoshi?”
            “Ami tiheshimiane. Mie nasemea mengine wewe unaeta utani usio na kichwa waa miguu; au unataka timitukane ndipo itashika adabu na adabu imishike? Hapa najua inafikiia mambo ya popobawa. Waa hunipati mie mwana wa Tanga.” anang’aka Mgoshi akionyesha kuchukia wazi wazi.
            Msomi Mkatatamaa ambaye hana mazoea ya kuchangia mwanzoni anaamua kutia guu baada ya kuona mada inakaribia kuharibiwa na utani. Anasema “unaongelea hili dili la zama za mzee Ruxa siyo ambako wanene fulani walimtumia huyu Chavda kutuibia njuluku kwa kisingizio cha kuwekeza wakati ukweli ni kwamba walikuwa wakihomola siyo? Ni bahati mbaya kuwa wachovu wanasahau haraka. Kwanini asitafutwe Chavda kwanza akapelekwa kuimba kwaya na akina Singasinga lupango badala ya kuchukua ardhi na kumwacha aendelee kutumbua fedha zetu kirahisi hivi? Nasikia huwa anaingia kayani na kutanua bila hata ndata wala njagu kumtia nguvuni na kumpeleka lupango akanyee debe kama wenzake.” Anapiga chafya na kuendelea “nikisikia waziri wa udongo anavyohanikiza kuzuia wachovu waishio ughaibuni kunyimwa ardhi nashangaa uwezo wake wa kufikiri. Mnawanyima ardhi wachovu wenu na kukimbilia kuwapa magabacholi?”
            Kapende anakula mic na kudema “kweli inashangaza namna wachovu tunavyokosa ardhi wakati majizi yakijirimbikizia ardhi yetu. Hivi kweli unaweza kwenda kupewa hata milimeta moja ya ardhi ugabacholini na ukawa salama? Sijui nani alituroga kiasi cha kugeuka mabunga hivi au tuseme wapumbavu kama wale waziri aliowatolea uvivu juzi. Naungana mkono na Msomi. Lazima Chavda asakwe na kuletwa kayani ili akapewa zawadi yake sawa na wenzake vinginevyo tutajua hili ni changa la macho la kuwakoa walioko nyuma ya kashfa hii.”
            Kabla ya kuendelea kurap Mzee Maneno anaamua kumpoka mic “hakamatwi Chavda wala nani. Nani hajui kuwa hili lilikuwa dili la wanene wetu wanaowatumia makuwadi wa kigabachori kutuibia kila uchao? Ukitaka kujua namna Chavda alivyomilkishwa kaya nenda kamuulize mzee Ruxa na Joni Mali ya sera utapata jibu sahihi. Unadhani dingi anao ubavu wa kuwagusa hawa wakati alishasema tusiwabughudhi ili waendelee kufaidi maulaji tunayowapa kwa kutupiga?”
            Mipawa hangoji amalize “M zee Maneno nakuunga mkono na nawashangaa mnaomshangaa Chavda wakati tunao vigogo kibao waliojimilkisha ardhi kibao. Unaweza kukuta Chavda hana chake hapa zaidi ya mabwana zake waliomtumia na kumpa chake naye akakitoa kwenda kufaidi huko majuu na ugabacholinikama walivyozoea kufanya. Je nao watanyang’anywa au ni ile danganya toto ya kutaka kutupiga changa la macho? Kama dingi yuko serious basi awanyang’anye hata hawa vigogo wanaojulikana kujilimbikizia ardhi yetu karibu kila kona ili baadaye wauze kwa bei mbaya.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic “kaka usinikumbushe vigogo hawa wasio na utu. Kule kwetu Morogoro karibu kila inchi inamilkiwa na mafisadi hawa wakubwa. Napanga kwenda kwa dingi kuwachomea utambi japo nao waonje joto ya jiwe kama Chavda.”
            Msomi analazimika kurejea “kwa taarifa yenu Chavda hataonja joto lolote hasa ikizingatiwa kuwa alichofanya ni kuchukua ile ardhi na kwenda benki na kuchukua mikopo ya mabilioni na kuishia pale wachovu walipostuka. Hukumbuki alivyopakizwa kwenye ndege na kufukuzwa kayani ili asitoboe siri ya washitili wake wa wakati ule? Sitashangaa kusikia kesi mahakamani toka kwa mabenki yaliyompa mikopo habithi huyu yakitaka yaachiwe yapige mnada ardhi yetu.”
            Mijjinga aliyekuwa akisoma novo anaamua kutia guu “Msomi usemayo ni kweli tupu. Ila kwa homeboy huyu hiyo sahau. Kweli yanawezekana kuwapo mabenki yaliyotoa mikopo kwa kukubali ardhi ile iwe kama poni. Ila kwa yanavyomgwaya homeboy, hayana ubavu wa kujitokeza. Yatakaa na maumivu yake; na mambo yataishia hapo au siyo?”
            Kanji hangoji aendelee. Anakatua mic “hata mimi iko sangaa sana. Hii Chauda nakimbia kaya na kurudi nyumenyume. Kwanini srikali hapana kamata yeye na kudai ilipe fidia kwa kutotumia ardhini mudra refu sana vakati vananchi nateseka bure au iko namna?”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu “jamani, shida yenu nini ardhi au kutaka kuwasumbua wanene waliosuka dili hili? Unadhani dingi hajui? Anajua kila kitu ila ameamua angalau kuwarambisha kidogo nanyi mtulie na kuchapa mzigo au vipi? Nadhani, kama walivyosema walionitangulia, kama kungekuwa na nia ya kukata mzizi wa fitina, hatua ya kwanza ilikuwa ni kumnyaka Chavda ili aeleze ukweli. Hata hivyo, nani anautaka ukweli wake wakati unawavua nguo wenye nguvu? Bila shaka haya ni yale ya mawaziri wapumbavu aliosema dingi juzi.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita manzi moto sana kiasi cha kutusahaulisha tuliyokuwa tukijadili!
Chanzo: Tanzania J'tano leo.

No comments: