Kudos to President Magufuli

Tuesday, 5 September 2017

Katiba Mpya: Barua ya wazi kwa rais John Magufuli

Image result for photos of magufuli
           
 Mheshimiwa rais John Pombe Magufuli,
            Habari za kazi na majukumu mazito ya kuendesha taifa? Kwa heshima kubwa napenda kukuandikia waraka huu wa wazi nikijadili umuhimu wa kuwa na katiba mpya nchini. Naamini utapata fursa, kama si wewe, basi washauri wako kusoma waraka huu kwako kama kiongozi mku wan chi. Leo nitaongelea umuhimu wa kurejea na kurejesha mchakato wa kulipatia taifa katiba mpya ambayo watangulizi wako waliiua kwa sababu ambazo hadi leo hazijulikani kwa watanzania wenye nchi na katiba yao.
            Ndugu rais, wewe kama kiongozi mkuu na mwakilishi wa wananchi, unapaswa kusikiliza sauti za watu wako. Kwanini nasema usikilize sauti na vilio vya wananchi waliokuchagua uendesha serikali yao kwa niaba yao? Mosi, ukirejea wingi wa watanzania waliojitokeza kutoa maoni katika mchakato wa kukusanya maoni, utagundua kuwa wengi wa watanzania wana hamu na katiba mpya. Mbali na hilo, ukiangalia muda na fedha zilizotumika katika zoezi hili, yeyote anayepanga au aliyepanga kuua maoni ya wananchi anapaswa kuchukuliwa kama mhaini, mhujumu na adui wa taifa. Tanzania ni nchi maskini yenye kutegemea kuombaomba na kukopakopa. Hivyo, haiwezi kuzamisha mabilioni ya fedha kwenye zoezi ambalo linaweza kutekwa na kuuawa na miunguwatu fisadi wawili au watatu. Hii ni kashfa kwa watanzania. Ni dharau isiyo kifani kwa watanzania ambao kimsingi ndiyo wenye mamlaka na haki ya kuwa na katiba na si watawala wao.
            Ndugu rais, nadhani umeshuhudia yaliyotokea nchi ya jirani ya Kenya ambapo matokeo ya uchaguzi wa rais yalibatilishwa baada ya kugundulika uvunjaji sheria na katiba. Hili naomba liwe somo kwako kuwa Tanzania nayo inahitaji katiba mpya ili kufanya mambo kisasa na kizamani. Kilichotokea Kenya ni ushahidi kuwa nchi inapokuwa na katiba viraka, inaweza kutawaliwa na viongozi bandia wasiotokana na utashi wa wananchi kama ilivyotaka kutokea nchini Kenya.
            Ndugu rais, najua ulivyo na uchungu na taifa lako. Umeonyesha hili wazi kwa namna unavyopambana na ufisadi na maovu mengine. Hili halina shaka wala mjadala. Hata hivyo, huwezi kufanikiwa kufika unakotaka kulifikisha taifa bila kuwa na nyenzo inayokupa nguvu na msaada wa kufanya hivyo yaani katiba inayokwenda na wakati ikiweka mbele uwajibikaji wa kitaasisi na wa mtu binafsi. Najua namna ufisadi unavyokukera na kukuhangaisha. Ungekuwa na katiba inayotamka wazi kuwa yeyote atakayetenda ufisadi afikishwe mbele ya vyombo vya sheria, wala usingehangaika hata kuwatetea wala kuwakingia kifua watangulizi wao ambao kufanya hivyo, kumetia doa dhima na lengo lako la kupambana na uovu. Ungekuwa na katiba mpya, wala usingepoteza muda kutumia jeshi la polisi kukimbizana na wapinzani badala ya wahalifu kama ilivyo sasa. Ungekuwa na katiba mpya usingekuwa na mizigo kama baadhi ya watendaji wako walioko karibu nawe waliotuhumiwa kughushi ukashindwa kuwawajibisha.
            Ndugu rais, watanzania wanataka katiba mpya. Ni nani huyu anayehujumu azma hii ili wamjue na ikiwezekana kumshughulikia? Kwa nikujuavyo kama mchapakazi na mzalendo wa kupigiwa mfano, utaepukana na vikwazo na vishawishi vya kutaka nawe uwe sehemu ya tatizo katika kusaka katiba mpya ambayo kimsingi ilishapatikana tokana kazi pevu iliyofanywa na tume ya Jaji Warioba. Nadhani, kinachokosekana au tuseme kilichokosekana ni ujasiri na udhu wa kufanya hivyo.
            Ndugu rais, kwa kiongozi mahiri kama wewe aliyeonyesha usafi wa hali ya juu, huna cha kuchelea ili ukwamishe upatikanaji wa katiba mpya vinginevyo kama una mpango wa kubadilika hapo baadaye. Kwa vile wewe ni binadamu, usijisikie vibaya kusema haya. Sina shaka nawe kwa sasa kutokana na udhu ulioonyesha kuwa nao.
            Ndugu rais, sisi binadamu ni viumbe wa muda; tunapita. Ni kama umande wa asubuhi kwenye majani. Hata hivyo, sawa na umande, hurutubisha mbegu ambazo huendeleza pale tunapoachia. Kwa rais anayeitazama Tanzania miaka mia ijayo, hana sababu yoyote ya msingi kukatilia uwepo wa katiba mpya. Hata kama ana marafiki anaodhani wanaweza kuingia matatani baada ya kupitishwa kwa katiba mpya, nadhani Tanzania ni muhimu kuliko marafiki na binadamu wowote hata wawe au waliwahi kushika madaraka makubwa kiasi gani. Nakuomba ndugu rais uige mfano wa Yesu aliyesema kila mtu ataubeba msalaba wake mwenyewe. Biblia katika Luka 14: 27 inasema “na kama huwezi kubebe msalaba wako na kunifuata, wewe si mwanafunzi wangu.” Nami niongeze “kama hutaki uwepo wa katiba mpya, basi wewe si mwenzangu na usinipotezee muda na kuniharibia uongozi wangu.”
            Ndugu rais, nimalizie kwa mambo mawili. Mosi, kuomba urejeshe mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya. Na pili, ueleze taifa tatizo liko wapi ili wakusaidie kulitatua ili taifa lisonge mbele na kuheshimu maoni na mawazo ya umma. Walatini wana msema mmoja maarufu ambao, bila shaka, hata nawe unaufahamu. Vox populi vox dei yaani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Ni shetani gani huyu ambaye anampinga Mungu? Tuseme wote kwa pamoja: Ashindwe na alegee.
Nimalizie kwa kukushukuru; na kama utaweza unaweza kunijibu.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.

No comments: