Kudos to President Magufuli

Saturday, 2 September 2017

Mlevi kuanzisha chuo cha uchungaji na ushehe


          Kama mtume Po alivyoona mwanga akaanguka na kuokoka au mtume Mood alivyobanwa mbavu kule mwambani, nami nimetokewa na Yeye Aliye Juu; ameniamru nianzishe chuo ili kurejesha maadili na kuondoa madili. Hivyo, nitaitwa nabii wa maadili mpinga madili na upigaji.
            Kwa vile wengi wamejivisha utukufu na vyeo vya uchungaji na ushehe kiasi cha kuumiza na kupoteza wengi, imebidi nitangaze uokovu. Naona yule anatikisa kichwa na kusonya.  Anaona ajabu mimi kujadili masuala ya dini. Kwani dini hazijadili masuala ya ulevi na kuupiga marufuku ukiachia mbali kukandamiza mila za Kiswahili na kusaidia ukoloni kuenea Afrika? Kuna jipya gani hapa iwapo siku hizi tunasikia kila kashfa kuanzia zile za ubakaji, unajisi, ngono na kujitajirisha kwa kutumia neno la Bwana God? Unadhani mimi ni sawa na yule shehena anayejiita shehe aliyenusurika kunyotolewa roho na walevi baada ya kukutwa akiiba kiti moto siyo? Au unadhani mie ni sawa na hawa wachunaji wanaohubiri upuuzi huku wakiwaibia wajinga wengi na kuishia kuwa matajiri wa kunuka hadi wanajenga mahekalu na kununua mapipa? Unadhani mimi ni sawa na wale maaskopo makopo waliopokea njuluku za Jimmy Rugetumbuliwa na Singasinga? Mie si sawa na matapeili wanaojifanya kuchambua Biblia kutetea dini fulani wakionyesha ubovu wake wakati waliogopa umande. Kama wewe ni msomi si utumie kitabu chako na cha wengine uwaachie wenyewe? Wakigusa chako unatishia kunyotoa watu roho. Mie ni mtu wa God kweli kweli hata kama ninalewa. Tofauti yangu ni kwamba mimi nalewa kanywaji wala si dhambi kama uroho wa utajiri na uongo unaoitwa miujiza. Muujiza ninaotenda ni mmoja; kutongoa ambayo wengi wanayagwaya kutokana na kuelimika vya kutosha kama mimi.
            Hujawaona wanaodai wanatenda miujiza wakati miujiza yenyewe ni utapeli na wizi mtupu? Hujawaona wachunaji walioutumia kupata vyeo vya kisiasa kama vile uishiwa ukiachia mbali wanaojipachika usomi wakati ni vibashite na vihiyo?
            Kwa taarifa yako love it or hate it, mie nimetumwa na mwenyewe asiyeonekana kuwaokoa walevi toka kwenye ujinga na udhambi utokanao na kutaka kuonja pepo kabla ya kufa. Haiwezekani; lazima ufe ndiyo uione pepo.  Hata hivyo, ukisharejesha namba unadhani utarudi? Hata usipoikuta pepo wala moto, who knows?
            Naona yule anaanza kujinga kusema eti najadili dini. Why? Kama dini zenyewe zimekuwa zikitujadili na kutukana maadili yetu tangu ziliposaidia ukoloni na utumwa kuingia Afrika, nini mbaya kuzijadili hata kuzizodoa? Mie siyo kama huyu shehe aliyeiba kiti moto wala askofu aliyepokea njuluku za escrew. I know what I am doing; na isitoshe mie ni bonge la msomi wa theology na dogmata. Umenipata siyo? Hivi unategemea nifanye nini wakati walevi wanazidi kupigwa na matapeli kama Lungumi, Escrew, UdA na wengine wengi? Hukusikia hata wale tuliowaamini madaraka yetu walivyonyakua ardhi hadi sasa walipofichuliwa na dokta Kanywaji bin Mtumbuaji ambaye siku hizi ameanza kuchoka kutumbua?
            Mie si mchunaji wala shehena anayependa kula na wanene. Kazi yangu ni kurejesha maadili hasa baada ya kugundua kuwa ile katiba mpya ya maadili iliuawa ili kulinda madili ya wanene wa zamani ambao dingi ameamua kufa nao kwa kuwakingia kifua huku akiwaadhibu wadogo zao. Hivi unapochuka ardhi ya Fred ukaacha ya bwana Rukhusa na Uwazi na ufichi unafanya nini zaidi ya kuruka mkojo na kukanya manonihino. Je huku ndiko kutenda haki bila ubaguzi ambao siku zote humsikia Kaisari akijinadi kuwa hatajali chama, dini, kabila wala rangi ya mlevi. Fred anadai alikuwa akimilki hekari 300 na ushei wakati shehe Aliii anamilki 1000 na ushei. Hapa hujamgusa brother Dangerman Dugong Makapi aka Chingaz.
            Ni bahati mbaya kuwa wanafunzi wa nabii Musa aka Mchonga hawakumuelewa kiasi cha kujiingiza kwenye ujinga wasijue mambo huenda yanabadilika. Hawakujua kuwa atakuja dokta Tumbuaji na kuwatumbua kiasi cha kutia mchanga kitumbua chao. Walume wangapi wanaongea pumba tupu kama wewe mchunaji tapeli?
            Enzi za kukua kwetu, hakuna waliokuwa wakiaminika kama viongozi wa kiroho kabla ya kuchipuka wasaka ngawira na wachumia tumbo wanaohubiri na kufanya upuuzi kama ambaye juzi nilimsikia akisema eti wanawake huongea sana kuliko walume na maongezi yao asilimia kubwa ni pumba. Sijui huyu mchunaji anayesifika kwa kupiga kanywaji anaweza kumwambia utumbo huu mama yake asimuachie laana? Kama mkeo ni bomu, usitukana wanawake wote.
            Tokana na kuongezeka kwa kashfa zinazochafua na kuvunja heshima ya dini, nimeamua kuanzisha chuo cha kunoa mashehe na wachungaji ili wapambane na wachunaji na mashehena waliotamalaki kayani wakitenda kila aina ya dhambi.
Chanzo: Nipashe J'mosi leo.

No comments: