Kudos to President Magufuli

Tuesday, 26 September 2017

Miaka miwili bila Mtikila

Image result for photos of mtikila
            Alipofariki mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP) sikupata fursa ya kumwandikia wasfu au kumbukizi. Huwa sipendi kuandika wasfu au ombolezo tokana na athari zake kwangu binafsi hasa inapofikia mtu ninayemfahamu. Huchelea kumsifia sana au kumpunja kwenye yale anayostahiki katika maisha yake.  Hata alipotimiza mwaka mmoja tangu afariki, sikufanya hivyo. Mwaka huu nimeamua kuvunja mwiko.  Hakunaubishi kuwa Mtikila alikuwa mwanasiasa wa aina yake linapokuja suala la kupigania haki za wanyonge tena bila kutetereka ukiachia mbali wakati mwingine kusababisha utata.
            Sasa ni miwili tangu nguli Mtikila atuondoke ghafla tokana na ajali ya gari iliyoacha utata iliyotokea Oktoba 4, 2015. Hivyo, tarehe 4 Oktoba Mtikila anatimiza miaka miwili kamili tangu atutoke.  Sikungoja tarehe kamili aliyotutoka Mtikila. Nimeona niandike kumbukizi hili wiki mbili kabla ya tarehe kamili tokana na sababu nyingi. Mojawapo ikiwa ni kushambuliwa na kuumizwa vibaya kwa mheshimiwa Tundu Lissu anayeonekana kuibuka na kuvaa na kutosha viatu vya Mtikila. Kwani, ukiondoa Mtikila, hakuna mwanasiasa anayeisumbua serikali kama Lissu. Pia hakuna mwanasiasa anayakamatwa na kukabiliwa na kesi nyingi zisizo na kichwa wala miguu zaidi ya Lissu.
Hata hivyo, kabla ya mwisho mwa uhai wake kuonekana kama kupunguza makali yake kisiasa kiasi cha baadhi ya watu kujenga dhana kuwa alikuwa amelishwa kitu jambo ambalo sijui kama lina ukweli. Hata hivyo, Mtikila atabaki kwenye historia ya taifa letu kama mtanzania aliyepigania mageuzi si ya kisiasa tu bali hata ya kisheria. Mtikila anakumbukwa kama mwananchi na mwanasiasa aliyefungua kesi nyingi dhidi ya serikali kandamizaji na kuiangusha mara nyingi tu.
            Nilimjua Mtikila mwishoni mwa miaka ya 80 pale kwenye bustani za Mnazi Mmoja alikopenda kupitia na kusikiliza vikundi mbali mbali vya watu waliokuwa wakibishania mambo mbali mbali ya dini, siasa au masuala mengine waliyoona kama yanastahiki mjadala. Mara chache Mtikila alikuwa akichangia kwa utulivu na hoja nzito; na mara nyingine akiiteka midaharo pale. Mara nyingine akiishia kutazama na kusikiliza bila kuchangia. Mbali na hapo, Mtikila alikuwa jirani yangu maneo ya Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko.
            Pamoja na kufahamiana na kuonana mara kwa mara, hatukutokea kuwa marafiki wa karibu kiasi cha kutembeleana au kukutana zaidi ya kukutana kwenye hadhara mara kwa mara. Kuna wakati tulitofautiana hapa na pale bila kujenga ukaribu wala umbali wala uhasama.  Tulibakia kujuana. Mara ya mwisho, nilikutana na Mtikila alipoamua kumvaa waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye akimtuhumu kujitwalia ardhi ya umma. Nilihudhuria mkutano wake na waandishi wa habari wakati nikiwa Habari Corporation; na huo ukawa ndiyo mwisho wa kukutana kwangu naye. Kwani, baadaye niliondoka nchini. Hata hivyo, nakumbuka; ni Mtikila huyu aliyeitisha maandamano makubwa Jangwani ya kupinga magabacholi kukalia taifa letu. Nilishiriki maandamano hayo yakiwa ni ya kwanza na ya mwisho kwangu hasa baada ya kuonja joto la mabomu ya kutoa machozi.
            Tukirejea kwenye mchango mkubwa na usio na kifani kwa Mtikila kwenye mageuzi ya Tanzania, sijui kama ni wengi bado wanamkumbuka na kumuenzi kama  inavyostahiki hasa kutokana na kujitoa kwake mhanga wakati wengi walikuwa wakiigwaya serikali. Mtikila alijigeuza ghafla kutoka kwenye kuwa mchungaji na kuwa  sauti ya wasio na sauti. Tofauti na wachungaji wa aina yake ambao wengi uchungaji au uaskofu wao hakutokana na mifumo iliyozoeleka, Mtikila hakujiingiza kwenye biashara ya neno la Bwana na kuwa tajiri wa kutisha kama wenzake tunaoshuhudia wakinuka ukwasi na kuhubiri siasa nyuma ya madhabahu kwa kuigopa serikali. Yeye alijitokeza moja kwa moja na kusema wazi alivyokuwa mwanasiasa mchungaji na si mchunaji anayejikomba kwa au kutumiwa na wanasiasa kama ilivyo sasa. Pamoja na elimu yake ya kadri, Mtikila hakujipachia vyeo vikubwa vya udaktari pamoja na kuwa na uwezo kiakili wa kuendana na sifa hii. Pi aliogopa kujiita askofu au nabii. Alibakia mchungaji na ariridhika na nafasi hii. Ni bahati mbaya kuwa ni wachache waliofuatilia na kuiga mfano wake hasa wakati huu ambapo dini, sawa na siasa, imegeuka biashara kubwa karibia sawa na mihadarati.
            Hivyo, binafsi naandika waraka huu lau kumuenzi mpiganaji huyu bingwa wa Ukombozi ambaye historia sahihi ya mageuzi Tanzania haiwezi kukamilika bila kubeba jina lake. Hakuwa mwoga wala mtu wa kunyamazishwa kirahisi. Alisema ukweli kama alivyouona bila kujali nani ageudhika au kuufurahia.
            Kwani, naona kama nina deni kwa nguli huu wa kupigania haki za wanyonge bila woga wala kuoneana au kupendeleana.
            Nilimjua kama mtu aliyekuwa na uwezo mkubwa kiakili hasa akiwa bingwa wa kujenga na kubomoa hoja. Nilimjua Mtikila kama mtu asiyepindisha mambo wala kuteteleka pale alipokuwa akisimamia jambo aliloliamini. Unaweza kusema kuwa staili ya upiganiaji haki wa Mtikila ilihitaji kile ambacho baba wa taifa Marehemu Mwl Julius Nyerere aliwahi kukiita moyo wa mwendawazimu au the courage of the mad kitu ambacho ni alama pekee ya mpambanaji asiye mchumia tumbo.
            Sasa imepita miaka miwili tangu Mtikila aondoke. Hatarudi. Japo kimwili ameondoka, mchango wake utakuwa nasi milele. Kumtendea haki Mtikila, tunapaswa kama taifa kutomsahau. Tumuenzi lau kama ishara ya kutambua mchango wake kwa taifa letu hata kama alikuwa upande wa pili.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: