Mfano, ni wanaume wangapi huwasaidia wake zao kutandika kitanda, kubadili nguo au kuosha watoto, kupika hata kuosha vyombo? Kwa Waswahili wengi, ukiwaambia kuwa hivi ni vitu vidogo vinavyoweza kufanya makubwa katika ndoa, ima watasema umelishwa limbwata au unawaletea uzungu. Unapungukiwa nini ukifanya shughuli hizo hapo juu ambazo, mara nyingi, huachiwa mama?
Mfano, katika zama hizi ambapo ushoga umeshamiri, ni vizuri akina baba kuwabadili nguo na kuwaosha watoto wenu wa kiume ili kujua tabia zao na kuwajengea tofauti za kimaumbile. Utajisikiaje ukigundua kwa mfano, msichana wa kazi, amemharibu mtoto wako hadi anageuka shoga? Haya hayapo? Ni uharibifu kiasi gani unaweza kuuepuka kwa tendo dogo tu la baba kuwabadili nguo au kuwaosha watoto wako wa kiume? Japo ndoa za wazungu zina nyufa nyingi kwa ndani, na nyingi zinaweza kuwa maigizo, zina mafunzo. Hawa jamaa wanapenda au wamejizoeza kusaidiana iwe ni kwa kutaka au kulazimika. Hili hatujui vizuri. Tunadhani tabia ya wazungu kusaidiana baina ya wanandoa imetokana na baadhi ya mambo kama vile ughali na ugumu wa kuajili wasaidizi wa ndani, kutowaamini, na mwisho, mwamko wao kuhusiana na haki na usawa wa binadamu.
Kwa ndoa zao zilivyo, tunaweza kusema mambo hayo hapo juu–––kwa bahati tu makusudi–––– yamewasaidia kuepuka kunyonyana katika ndoa. Hivi huwa unajisikiaje unapokuwa umelemewa na mzigo halafu ukapata msaada kwa mtu mwingine tena saa nyingine asiyekuhusu? Je huwa unajisikiaje unapopewa lift wakati ushatembea au kungoja daladala na kukata tamaa? Vyote hivi vinaweza kukuonyesha–––kama binadamu yeyote–––tunavyochoka.
Katika kuishi kwetu kwa takribani miaka 30 katika ndoa, tumejifunza kuwa hakuna kazi ya mke au mume linapokuja suala la kusaidiana. Tumefanya hivyo baada ya kugundua kujiuliza maswali muhimu mfano, mbona hakuna chukula, barabara, magari au nyumba za kike? Kwanini––––kama lengo siyo kunyonyana––––jinsia na ujinsia uje kwenye kazi au hata kipato wakati mwingine kutokana na mfumo dume? Mbali na kusaidiana kuondosha mmoja kuchoka zaidi ya mwingine, kusaidiana, huleta upendo na kuonyesha kuwa wahusika wanawajali wenzao.
Zama za mama kubeba mtoto mgongoni, jembe begani, na mzigo wa kuni au mavuno kichwani zishapitwa na wakati. Zilifaa zama za uwindaji. Zimepitwa na wakati kutokana na kuwanyonya na kuwazeesha akina mama bila sababu ya kufanya hivyo. Tunadhani wahusika wangejua namna walivyo, au wanavyowazeesha wake zao na hasara itokanayo na hali hiyo, basi wangeacha na kuanza kusaidiana. Wengi wasiojua madhara ya mazoea na utamaduni huu wa kizamani, hawajui madhara yake. Hivyo, kwa wanaosoma makala hii, kama bado umeshikilia ukale huu, umepata la kujifunza au kuwafunza wengine.
Tumegusia kutandika kitanda au kuosha vyombo. Je hicho kitanda nani anakivuruga kama siyo nyinyi? Kama ni nyinyi, kwanini kazi ya kukitandika iwe ya mtu mmoja? Je hivyo vyombo, nani anavichafua kama siyo nyinyi, watoto au wageni wenu? Je kwanini iwe haki na mazoea kwa mmoja wenu pekee kuachiwa kazi hiyo? Mkisaidiana kufanya usafi na mambo mengine, siyo tu mnaokoa mna na lawama za kichinichini, bali mnaongeza upendo na kujali baina yenu.
Tokana na wengi kuona vitu hivi kama vidogo visivyo na maana wala madhara, uozoefu unaonyesha kuwa vile vitu vidogo tunavyoona kuwa ni kazi ya mama, akisaidia mume, vina maana na hata madhara pale haki inapokosekana. Akina mama wanajua fika namna vitu hivi vinavyowafurahisha na kuwaridhisha kuwa wanapendwa na kuthaminiwa. Vidogo hivi vinavyoweza kuzaa makubwa yenye neema au nakama katika ndoa. Kwa wale ambao hawajajaribu kufanya vitu hivi, tunawashauri wajaribu waone namna vinavyofanya ndoa ifane na maisha kuwa mazuri na rahisi. Mkeo ni mwenzako, mwenzi wako na mshirika wako tofauti na dhana potofu kuwa mke ni msaidizi wako. Haya yemepitwa na wakati.
Tumalizie. Hata ile dhana ya kikale kuwa Mungu alimuumba Adamu kwanza na akamtoa Eva kwenye ubavu wake ili awa msaidizi wake tunaipinga japo hatutaki kuingilia mambo ya dini. Hata hivyo, kama mambo haya yamewaharibu watu wetu, tutafanya nini kujilinda na kujitetea. Tia akilini.
Chanzo: Mwananchi J'pili leo.
No comments:
Post a Comment