How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday 15 October 2024

Nyerere, Tumetoka Kutegemeana Hadi Kutekana

Mwl Julius Kambarage Burito,

Shikamoo baba wa taifa. Naamini huko uliko wala hupumziki kutokana na yanayotupata mafyatu wenzako. Hivyo, naandika toka mafichoni sasa. Naona umestuka. Ndiyo. Niko mafichoni. Hata ninapoongea ni kwa sauti ya chini ili wasije kugundua. Mwanao naogopa kutekwa, kupotezwa, hata kuja huko haraka bila kutaka wala kutarajia ili lau niwasaidie mafyatu wanaofyatuliwa na mafyatu wanene na wale mafyatu wanaowateka. Japo nimekuwa nikikuhabarisha kinachoendelea kama si moja kwa moja ni kupitika kwa Madaraka, hili sikuwahi kukujuza. Hata Madaraka hajakujulisha kutokana na kuwa bize na mambo mengine ya kifamilia hasa kumuangalia bi Mkubwa wako. Sikukujulisha  hili tokana na kudhani kuwa kadhia hii ilikuwa ni wingu linapita. Baada ya kuona wingu lenyewe halitoki bali linageuka donda ndugu, heri nikijuze lau utuombee. Usishangae kwanini kuomba wewe uwaombee walio hai badala ya wao kukuombea.

Huku, siku hizi, hakuna waombaji bali wapigaji wajitiao kufanya miujiza uchwara yaani kuwaibia makapuku wajinga na waliokata tamaa mbali ya uvivu wa kufikiri. Siku hizi, waombaji wanaombea wanene badala ya kuwapa vipande vyao.  Nao, siku hizi wamekuwa sehemu ya wanene kiasi cha kuchanganya religion na politics.  Inakera na kuchanganya. Maana, tofauti ya wanene wa neno na wapiga ramli hakuna. Dini zimegeka duni. Uongozi umegeuzwa uongo. Woga umegeuka ujasiri na heshima imegeuka aibu. Hayo tuyaache.

Najua uliamzisha, kujenga, na kutuachia kaya ya Ujamaa na Kujitegemea. Kama nilivyowahi kukujuza, baadaye iligeuka kaya ya uhujumaa na kujimegea. Sasa imeongeza sifa nyengine. Ukipata unene, unaugeuza mali ya ukoo wako, marafiki, jamaa, na kwenu. Unaweza kujenga uwanja wa ndege hata kijijini mwako na mafyatu wasikifyatukie wala kunung'unika Unaendeleza ulikozaliwa hata ukiacha maeneo mengi nyeti.Tumetoka kwenye kutegemeana na kujaliana kwenda kwenye kutekana na kupotezana na kuuana. Badala ya kuwa Wajamaa tumegeuka watekaji na wahujumu wa roho na mali za mafyatu. Ukiwauliza wanene kuhusu utekaji na unyotoaji roho vilivyoanza kuzoeleka, wanazoza bila aibu kuwa siyo kayani tu bali dunia nzima. Kinachotisha wanatekwa mafyatu wa chata fulani. 

Kadhia hii ilianza pindi yule jamaa uliyemfyayua asiwe rahis baadaye akawa kuachia ngazi. Ghafla bin vuu, alirithiwa na jamaa aliyemzidi ketu na kumtumia. Hapo ndipo urais ulibadilika ukawa uungu hadi urahisi baada ya kuwa nyenzo ya kupigia njuluku za mafyatu. Rahis alijigeuza na kugeuzwa hadi kuitwa mungu. Tokana na hali hii, kila aliyetofautiana na mungufyatu huyu alipatizwa ikwemo kutekwa kupotezwa au kuuana. Kwa waliomsifu hata mambo ya hovyo, kama ambavyo ungeyaita kwa ukali, unaula bila kuguswa na yeyote hata awe na kifua kikubwa kiasi gani. Tofauti na zama zako tumejengewa woga kujikomba kujipendekeza kusifiana ha kuhadaana. Japo hata wakati wako woga ulikuwepo huu umepitiliza. Siku zile tulijali kudumisha na kulinda ufyatu. Siku hizi ufyatu umezikwa. Vinaabudiwa vitu hasa unene kama tikiti ya kula dezo. Mafyatu wanadhalilika, kudhalilishwa, na kudhalilishana hakuna mfano.

Mwl. unawezaamini kuwa tuna mafyatu wanaoonea fahari kuita au kuitwa chawa? Baaada ya ujinga huu kuanza kuzoeleka, tunangoja kuona kunguni wadudu wengine wanyonyao wakigeuka masuperstars. Siku hizi, kuna utitiri wa vyombo vya habari. Hata hivyo, havina meno. Kila yakiota ima yanang'olewa au midomo kutiwa kufuli. Siku hizi, kale ka mchezo ka kuhoji kila kitu kamekufa. Ingawa kalianza wakati wa enzi zako kinamna, siku hizi ndo usiseme. Kuhoji au kushuku hata kuchukia siyo haki tena. Kwanini uchukie na kuwachukiza wanene? Kwanini uwahoji au kuwashuku wakati wao ndo wabeba na wenye maono na hata maoni. Badala yake, tunaimba mapambio. Siku hizi, hatufikiri. Ukijitia kufikirifikiri ili uhoji, unatekwa na kupotezwa, na hakuna anayejali wala kukamatwa. Wanafikiri wabeba maono kwa ajili yetu. Siku hizi kuna miujiza ya kisiasa. Juzi nilishuhudia kitegemezi cha mnene kikitoa misaada ya mamiloini nikanusurika kufa kwa mshangao na woga. Nihoji nipotezwe. Nimezee nife kwa presha. Hayo sasa ndo maisha yetu. Baada ya kuzidiwa kete, siku hizi, naandika mashairi lau kujiliwaza ila siyo kusifu visivyosifika. Siku hizi, hata makombo yanaitwa chakula kipya. 

Tunaweza kuhamisha mafyatu kupisha wanyama au wawekezaji watuwekezee njuluku ingawa nazo hatuzioni na kuzifaidi isipokuwawanene wachache wenye meno..

Siku hizi, tunajenga vitu na kubomoa ufyatu. Tunajisifu kwa kuwa na vitu hata kama ni masikini wa ufyatu. Mafyatu wako tayari kufyanya lolote hata kama ni kudhalilishwa ilmradi tonge liende kinywani japo si wote. Hiki ndicho chanzo na siri ya mafyatu kushabikia kuiitwa na kuwa machawa. Bado kunguni na viroboto hata mbu kama si nune.

Mwisho, kuna aina fulani ya uchangudoa wa kimaadili unaoanza kukubalika hata kuzoeleka. Zamani mlipambana na ufusadi. Siku hizi tunaupamba na kupambana na wanaopambana nao. Siku hizi tunajimegea badala ya kujitegeme. Kwa leo, kwa faradhi na taradhi, niishie hapa.

Basi lala salama Mwalimu.

Chanzo: Mwananchi leo

No comments: