How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday 13 October 2024

Wanandoa Si Njiwa wala Chui

Kuna imani kuwa njiwa ni viumbe wenye mapenzi ya kweli. Ni wapole na wapenda amani. Mara zote, utawaona wawili wawili, akiongezeka basi jua ni makinda yao mawili ambayo nayo yakishapevuka, huondoka wawili wawili kwenda kuanza maisha yao ya wawili katika uwili huu wa kuvutia. Kutokana na maisha na tabia za njiwa, viumbe hawa wanahusishwa na sifa zote nzuri kubwa zikiwa ni amani, upendo, na usafi. Wanazo nyingine nyingi tu.
            Kwa upande mwingine, kuna ndoa ya hovyo ambayo hakuna yeyote angepeda kuwa nayo. Hii ni ndoa ya chui. Kawaida, chui wanakutana wakati wa kujamiiana. Mama akishatunga na baba kutungisha mimba, wawili hawa wanamalizana kila mmoja kivyake.  Hawa wanyama ni wanyama wapenda milki au territorial. Wanaishi kwenye maeneo yao kila mmoja na lake. Inapotokea mwingine akaingia kwenye eneo lisilo lake, atafukuzwa hata kuumizwa na mwenye eneo. Hivyo, chui, kimsingi, hawana ndoa zaidi ya kujamiiana na kila mmoja anachukua hamsini zake. Hata hivyo, hawa ni hayawani walionyimwa utashi ingawa hata njiwa ni wanyama ambao huenda upendo na ustawi wao si chaguo bali matokeo ya majaliwa yao.
            Sasa tuje kwa binadamu. Kwanza, kiakili, binadamu si wanyama ingawa kibaolojia ni wanyama. Hivyo, wana vitu viwili vya ziada yaani akili kubwa na utashi ambavyo wanyama hawana ingawa bado vitu hivi vinaweza kutumika vizuri au vibaya kulingana na mazingira, malengo, na sababu za wahusika kufanya hivyo. Kwa binadamu, japo siku hizi ni chaguo, ndoa ni lazima. Maana, bila ndoa, idadi ya watu katika eneo au nchi fulani hata duniani itapungua. Hivyo, pamoja na mambo mengine, ndoa ni kiwanda cha kutengeneza watu kwa ajili ya kesho japo siku hizi mambo yamebadilika kiasi cha watu kuoana kwa ajili ya kuishi pamoja bila kuzaa. Huu nao unaitwa uhuru hata haki ya binadamu ambayo haiulizi kama wazazi wa hawa wanaoamua hivi nao wangekuwa kama wao, wao wangekuwa wapi. Leo, hili halitushughulishi. Kwa wale waliokwisha kuoa na kuolewa, hakuna jambo lenye furaha kama kuingia kwenye taasisi hii. Jambo hili, mara nyingi, huwahushisha watu zaidi ya wawili ingawa wawili ndiyo wenye shughuli. Hii ni kutokana na ndoa kuwa kiungo baina ya familia hata jamii. Kadhalika, hakuna jambo linatia karaha na kusikitisha kama kuvunjika kwa ndoa. Hii ni kutokana ukweli kuwa wawili walioingia kwenye mahusiano ya maisha kwa malengo ya kuishi pamoja hadi mauti, wanapofikia kugeuza kibao kiasi cha upendo kuwa chuki, madhara yake si madogo wala ya muda mfupi.
        Siku zote, ndoa huanza na mapenzi na chaguo lililo bora japo laweza lisiwe. Katika macho ya wahusika, anayechaguliwa ndiye anayeonekana bora na wa kufaa katika wengi. Hivyo, tunaweza kusema kuwa ndoa nyingi huanza baina ya njiwa na kuvunjika baina ya chui. Hivyo, basi, ieleweke, wanandoa ni wanandoa na si njiwa wala chui. Yawapasa kulijua hili na kuwa tayari kukubaliana na madhaifu na ubora vyao ili kuweza kuishi na kutumiza ahadi na nadhiri walizojiwekea.
Jambo la kujiuliza ni kwanini ndoa huanza kwenye unjiwa na kuishia kwenye uchui? Hakuna jibu moja wala rahisi hasa ikizingatiwa kuwa maisha binadamu ni mchanganyiko na mkusanyiko wa mambo mengi yawe ndani au nje ya wahusika. Kama wataweza, japo hili wamefanikisha wachache kulinganisha na walioshindwa, wanandoa wajenge ndoa yao kama njiwa ili kuepuka kujenga ndoa ya chui. Hapa zinahitajika juhudi za makusudi kulifikia lengo hili pia, ni kazi ngumu inayochukua muda mrefu.
        Mwisho, lazima kuzingatia kuwa, licha ya kuwa taasisi, ndoa ni mchakato wa maisha wenye kila aina ya changamoto na vikwazo ambavyo wanandoa wanapaswa kuvijua na kutafuta namna ya kuvigeuza kuwa fursa wakijua kuwa wenzi wao siyo njiwa wala chui bali binadamu na wanandoa wenye kila aina ya mapungufu na ubora kadhalika. Shikilieni yaliyo bora na kuachana na yasiyo bora. Angalieni na kushikilia mambo yanayowaunganisha kuliko yanayowatenganisha mkijitahidi sana kuwa njiwa na kuepuka kuwa chui.
Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: