The Chant of Savant

Wednesday 19 December 2007

Dini,unafiki,uganga njaa,utapeli na ufisi chini ya CCM


Mchungaji Rwakatare; dini na siasa inawezekana?


Nkwazi Nkuzi Mhango

Mhango ni Mwalimu, Mwandishi wa habari, mwanaharakati wa Haki za Binadamu,

Mtunzi, Mshairi, na mwanachama wa chama cha watunzi cha Newfoundland and Labrodor-Canada-WANL aishiye Kanada.


KUMBUKUMBU zangu zinaniambia kuwa wanasiasa wetu wamekuwa mara kwa mara wakituhimiza tusichanganye dini na siasa. Wamekuwa wakituaminisha na kututisha kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuchanganya mafuta na moto. Bado nakumbuka wimbo wa mpiga debe maarufu wa siasa fichi, zilizovishwa joho la dini na roho mtakatifu, Faustine Munishi. Munishi, sawa na watawala wetu, alitahadharisha kuchanganya dini na siasa kwa kulinganisha na mafuta na maji ambayo ‘reaction’ yake huwa mlipuko mbaya na wenye madhara makubwa sana. Kadhalika wakuu wa serikali ya chama tawala, CCM mara nyingi wamekuwa wakitahadharisha juu ya hatari ya kuchanganya dini na siasa, hasa yanapoibuka madai ya makundi ya dini dhidi ya serikali na yanayokinzana na serikali. CCM juzi ilimtangaza rasmi Gertrude Rwakatare ambaye ni mchungaji baada ya kuanzisha dhehebu lake. Amepewa ubunge baada ya kufariki Waziri mdogo wa zamani Salome Mbatia. Kweli kufa kufaana. Kwa mtu anayefuatilia na kuamini maagizo na tahadhari za watawala wetu, alistuka na kushangaa inakuwaje? Je, kwa mchungaji, tena anayekubalikana na wafuasi wengi, kupewa ubunge si kuchanganya siasa na dini? Je, siasa na dini ni hatari zinapochanganywa na watu wasio na mamlaka wala uhusiano na waliomo madarakani? Kwa mfuatiliaji wa mahubiri ya Rwakatare maarufu kama “kuambukiza utajiri” atashangaa ni jinsi gani Rwakatare anaweza kuwa mwanasiasa na kubaki na udhu wa uchungaji. Nina nia njema kabisa na Rwakatare aendelee kuwa mchungaji wa kuaminika, lakini kwa siasa tena siasa tatanishi kama za Tanzania, ni namna gani mama huyo anaweza kuwa mwanasiasa na mchungaji akaendelea kuaminika? Mchungaji Rwakatare, bila shaka anajua ubabaishaji wa wanasiasa wa Tanzania. Likitokea suala la uongo ni wao, ufisadi wao, dhuluma ni wao, je, mchungaji huyo anaweza kuambukizwa ugonjwa huo ambao kwa wanasiasa ni sawa na malaria ambayo kila mmoja lazima augue? Je, yaliyosemwa na Horace Kolimba (sasa marehemu) kuwa CCM imepoteza mwelekeo na Mwalimu JK Nyerere kuwa CCM imeporwa na matajiri na sasa viongozi wa dini ndiyo yanatimia? Hivi leo Kardinali Pengo akiwa mbunge tena wa upinzani, hali itakuwaje? Inakuwaje mchungaji awe mbunge? Je, kati ya Mungu na siasa atamtumikia nani? Maana huwezi kuwatumikia mabwana wawili. Inatia shaka zaidi kwa mtu anayesimama mbele za watu kuhubiri upendo, usawa na haki kukumbatia chama na siasa za kijambazi kama zinazoendeshwa na CCM kwa sasa ambako rasilimali za umma na maadili ya umma vimehujumiwa na kikundi cha watu wachache. Mfano mzuri ni Kenya, ambako mchungaji wa kujipachika aitwaye Pius Muiru anayesifika kwa kuwadanganya Wakenya kuwa angewaonyesha Bwana Yesu, asifanye hivyo, anagombea urais! Pia tumekuwa na mchungaji Christopher Mtikila ambaye naye kama wenzake, huwa haishi utatanishi. Kwanini wachungaji hawa wasivue magwanda yao ya kidini na kuvaa ya kisiasa au kuachana na siasa wakamtumikie huyo Mungu wao? Je, wanachofanya watu hawa ni kuonyesha uongo wa watawala wetu ambao wamekuwa wakituhofisha kuchanganya dini na siasa wakati wao na viongozi wa dini wanakula sahani moja? Jiulize ni mara ngapi watawala wanaojulikana kwa ufisadi na jinai zao wanakaribishwa kuchangia miradi ya dini bila kwanza kuulizwa walivyozipata mali zao? Katika kitabu changu kinachotegemewa kuchapishwa hivi karibuni kiitwacho “Saa ya Ukombozi” kitakachochapishwa na mtunzi maarufu wa kitabu cha Mwalimu Mkuu, Paschally Mayega, nitadurusu “ndoa” hii ya watawala na viongozi wa dini wanaotumia madaraka yao kuwapotosha wananchi. Hivi sasa ipo tabia si kwa Mchungaji Rwakatare, bali kwa baadhi ya wachungaji ambao wameamua kuwachezea wananchi viini macho kwa kujivika utukufu wakati ukweli wanachotafuta ni mali na madaraka chini ya roho mtakakitu huku wakijionyesha kama wana roho mtakatifu. Hivi mtu kama Rwakatare anayejulikana kwa mahubiri yake mazuri na matamu, atashindwa kuwashawishi wafuasi wake kuiunga mkono CCM kwenye uchaguzi? Je, huyu atakuwa na tofauti na masheikh waliowahi kukemewa na CCM kuwa walikuwa wakitumia misikiti kuhubiri siasa zenye kukinufaisha Chama cha Wananchi (CUF) kwenye chaguzi zilizopita? Au tuseme dini na siasa vinapochanganywa kwa maslahi ya CCM vinaacha kuwa na athari tunazotahadharishwa nazo? Je, hapa nani anamdanganya nani, hadi lini? Je, huu si uoza wa kitaasisi ambapo CCM imejipenyeza kwenye vyombo vya habari, madhehebu ya dini, vyama vya michezo, biashara na nyanja zote za maisha? Huu ni unazi mamboleo ambao mwisho wake si mzuri kama tutauachia uote mizizi. Si siri kuwa kwa kiongozi wa dini kufanya siasa sawa na kuitumia nafasi hiyo kuwahujumu walio wengi. Kama wanasiasa wafanyabiashara wanaotumia nafasi zao kuuibia umma na kujineemesha, viongozi wa dini kwenye siasa wanaweza kutumia nafasi zao na ushawishi wao kupata misamaha ya kodi na upendeleo mwingine huku wakiwagawa wananchi kulingana na wanavyotaka. Kuna haja ya kuwabana wakatamka wazi kuwa siasa na dini vinachanganyika kwa wote bila kujali itikadi ya mtu. Kuna haja ya kuruhusu vyama vyenye muelekeo wa kidini kushiriki siasa kama wajanja wachache wataruhusiwa kutumikia dini na siasa kwa wakati mmoja au kuwapiga marufuku kama vilivyopigwa marufuku vyama vya kidini, kikabila na kijimbo hata kijinsia. Kama jinai hii itaachiwa iendelee kutamalaki kwa vile wahusika wanakula sahani moja na watawala, kuna siku umma utaasi na kufichua unafiki na uongo huu wa wazi. Tujalie Rwakatare angekuwa ameupata ubunge kwa tiketi ya chama cha upinzani, CCM isingeacha kuibua rungu lake la kuchanganya siasa na dini kumpatiliza na kumshikisha adabu. Tunasema hivi kutokana na ushahidi wa wazi. Nani mara hii kasahau maneno ya Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye alipowaambia wafanyabiashara waliokuwa wamejiunga na upinzani kuwa wakitaka mambo yao yawanyookee wajiunge na CCM? Na kweli baada ya maneno haya kutamkwa tuliwaona wafanyabiashara kama Thomas Ngawaiya na wengine ambao biashara zao zilikuwa zimedoda kujiunga na CCM na mambo yao kuwanyookea. Tunakumbuka Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alivyogeuka bubu kuhusu kadhia ya mauaji ya Bulyanhulu baada ya kutishiwa kunyang’anywa jumba lake. Hivi sasa UDP haina tofauti na CCM B! Na kwa salata na jinai hii, bado inapewa ruzuku toka kwenye hazina ya umma kwa ufisadi inaoufanya. Hitimisho. Hakika ubunge wa Gertrude Rwakatare uwe kichocheo cha kuikataa hadaa na maangamizi ya maslahi ya umma yanayosababishwa na maslahi ya kisiasa ya kikundi kidogo cha watu. nkwazigatsha@yahoo.com

No comments: