The Chant of Savant

Wednesday 12 December 2007

Miaka miwili Ikulu na matokeo ya utafiti wa Kijiweni na REDET

BAADA ya REDET kuja na matokeo ya utafiti juu ya maoni ya wanakaya juu ya utendaji wa Mkuu, na Kijiwe kimetoka na matokeo yake.

Ni miaka miwili tangu tuukwae uongozi wa kasi mpya nguvu mpya na ari mpya. Tuliahidiwa Kanani tukaambua balaa.

Tulitoa kura tupate maendeleo na maisha bora. Sasa tunahangaika na kuendelea katika kutoendelea huku maisha yakiwa bora maisha badala ya maisha bora! Tumo msambweni tukilalama na kutumiwa kama wanyama wa mizigo!

Matokeo ya utafiti yafuatayo yaliendeshwa na Kidet au Kijiwe Democracy and Transparency.

Tofauti na REDET, Kidet si NGO ya ulaji wala kujikomba kwa yeyote.

Chini ya wakurugenzi wa Kidet, Profesa Mpayukaji Msemambovu na Profesa Msomi Mkatatamaa, yafuatayo ndiyo matokeo ya utafiti uliohusisha walevi, vibaka, wachumia tumbo na wajigongaji-bootlickers and choirsingers.

Hawa tumewapata kwenye mabaa, madanguro, vijiwe vya kahawa na vya kuuzia bangi na gongo. Kwa upande wa wanasiasa na wachumia tumbo tuliwapata kwenye mikutano na makongamano ya kuelezea na kutafsiri Li-bajeti la Iron Lady akisaidiwa na Mr Eddie Lwasha.

Wajumbe wa kamati ya Kidet walitolewa mkuku maeneo ya wazito kwa kupigiwa zegere la mwizi huku walinzi na mbwa wa getini wakitoa mpya kwa kutishia kuwanyotoa roho wadodosaji wetu.

Kidet ilizunguka kaya nzima kwa mtaji wa pesa ya kahawa na kuibuka na yafuatayo.

Kwanza, wanakaya waliokuwa wakimmwagia ujiko Mkuu wanaonekana kubadilika vilivyo. Wanasema wazi kuwa amewaangusha na kuwasaliti. Utafiti unaonyesha kuwa kiwango cha kuungwa mkono na kuaminiwa kimeshuka kutoka asilimia 89 hadi 39.

Katika nyanja ya uongozi bora, Mkuu ameibuka na asilimia 11. Asilimia hizi amezipata kutokana na kuweza kuunganisha nyumba zake na marafiki kwenye ulaji wake.

Ukilinganisha na asilimia nyingi alizokuwa nazo miaka miwili iliyopita, ni kwamba Mkuu ametoka kapa kwenye uongozi bora. Amefanikiwa kwenye kutosema ukweli kulikoweza kuwafanya wananchi wasiingie mitaani baada ya matarajio yao kupotea.

Pili kwenye uwajibikaji ameambulia asilimia tano au kutoka kavu kabisa. Hata hizi asilimia tano amezizoea kutokana na kuwajibika kwa marafiki na familia yake.

Tatu kwenye eneo la maendeleo, Mkuu ameendelea sana kuanguka kutokana na kuelekeza maendeleo kwenye jamaa zake na chama chake huku wanakaya wakikosa maendeleo kabisa. Kitaalamu amepata asilimia zinazotafsirika kama HOVYO. Yaani Hakuna organizasheni, visheni yeyote na open policy. Uchumi umezidi kuendelea katika kifo cha kuporomoka na kutegemea takwimu za wajanja fulani.

Kwenye eneo la mipango, Mkuu amepata alama tisa ambazo kitaalamu zinatafsiriwa kama CHOVU yaani Choka mbaya, hali holelea, ovyo, vurumai kiutawala na ufisadi.

Kutengeneza ajira: Mkuu amepata alama maarufuku kama CHOO. Yaani chakavu, hasara, ovyo na ombaomba.

Tahadhari: Msomaji inabidi uvumilie kupambana na maneno (terminologies) magumu kutokana na hali halisi ya mambo na kwa miaka miwili mafanikio yaliyotokea ni hasi.

Kwa mfano, kumekuwa na mafanikio kwa kundi dogo la wanasiasa na wasaka ngawira wengine ambao wamefanikiwa kuzidisha utajiri wao na kukuza mazingira ya kuiibia kaya kama vile kusaini mikataba mingine feki huku ikiundwa tume ya ulaji kwa nia ya kuwazuga wanakaya na kuwachanganya wapingaji. Rejea kutaka kunyakuliwa kwa Kabwela ambaye chama chake kimeonyesha ukomavu kwa kuliepa zengwe zima.

Matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa baraza la ulaji la mawaziro limefanikiwa kumpiga mweleka mkuu Mkuu kwa kutofanya kazi yoyote zaidi ya biashara hasara ya kunyakuwa na kutengeneza njuluku.

Waziri aliyetia fora miongoni mwa waliotia fora ni Kadamage akifuatiwa na Eddie, Miramba aliyetia fora kwa kusamehe njuluku.

Pia yumo Kingungo Ngumbaru Mweupe aliyetia fora kwa kupayuka na kuzomewa. Mwingine ni Forofwesa Petero Msulwa kwa kutia mtima nyongo kwenye njuluku za wasomi wa vyuo vikubwa.

Mwingine aliyeshika nafasi za juu kwenye kupiga mieleka ni waziro, Banado Maembe aliyetia fora kuwadanganya walalanjaa kuwa mambo yanakwenda bien kiasi cha kumwagiwa ujiko ugenini huku wajumbe wa nchi za ugenini walioko kwenye Kaya wakishangaa na kusema wazi kuwa si kweli waziro alihadaa umma naye akajihadaa pia!

Katika taasisi zilizochangia mafanikio haya ya maanguko zipo taasisi tatu zilizotia fora. Ipo Apitielo, Richmonduli na Do-wans. Hizi zilifanikiwa kutengeneza njuluku kwenye sekta chovu ya nishati ambapo ilitangazwa na kuzimwa kuwa bei ya nishati za mataa zingepandishwa bei ili kufidia njuluku zilizogawiwa kwa magwiji hao wa ulaji.

Hali ya mambo ilifurahisha sana hadi kiongozi mmoja wa nchi ya Kanata au Kijiji kuzoza mbovu kuwa nchi yake isilaumiwe kwa upotevu wa njuluku na maslahi kwenye mawe yenye thamani yaliyonyimwa thamani kutokana na taratibu za kijambazi za wakuu wa Kaya.

Mapendekezo ya KIDET.

Mosi - Mkuu kuvunja genge la ulaji na kuunda kitu kipya chenye njemba zinazojua kupiga mzigo zenye roho takatifu tofauti na zilizopo zilizo na roho takakitu.

Pili - baada ya kuvunja genge la maulaji na kuwatimua wahusika, Mkuu kwanza ataje mimali yake na familia yake huku wahusika wakifikishwa kwa Pilato ili wafungwe na kunyang’anywa mimali waliyokwanyua.

Tatu - chama cha maulaji (CCM-si chama cha Mapinduzi uchwara) kivunjwe au kurejeshwa kwa makapuku waliokianzisha wakati wa nabii Musa.

Nne - elimu ya uraia itolewe hadi kwenye mabaa na madanguro huku maandamano yakiingizwa kwenye katiba.

Tano - njuluku zilizopatikana kutokana na ufisadi, mikataba, uuzaji wa magogo, uuaji wa wanyama vitalu na migodi zilizotoroshwa zirejeshwe nchini. Hapa kampuni la Deep Green wa magrini lilitia fora kwa kutoroshea njuluku nje ya nchi hasa kwenye visiwa fulani.

Sita - wanakaya wasipewe aiskrimu takrima kwenye uchaguzi wala ahadi hewa na za hovyo.

Saba - kiongozi atayeunguza kwa kuongopa atiwe bakora hamsa na kushushwa jukwaani huku akizuiliwa kushiriki siasa maisha.

Saba - wabunge wazururaji wapigwe marufuku kuzurura Bongo na wakija kwenye vikao vya kijiwe wawe na vibali maalum. Pia mishahara yao na ya mawaziro ipunguzwe na kulingana na ya walimu na walinzi.

Nane - kumetolewa suluhu ya migogoro ya miungano kama ule wa Zenj. Muungano uvunjwe ili kuepuka migogoro na mitafaruku huku kiranja wa Zenj akichaguliwa na wanakijiwe wa Zenj kwa maelekezo toka Zenj si Idodomya.

Kitu kingine kilichobainika kwenye utafiti ni kuchoka kwa katiba ya ‘kaya’ ambayo licha ya kuwa na viraka ni ya mwaka 47. Kidet inapendekeza iandikwe mpya kwa kasi mpya, ari mpya, nguvu mpya na watu wapya.

Tisa - Kidet inapendekeza kosa la ukeketaji wa kimawazo liingizwe kwenye ‘penal code’ au kanuni ya jinai na adhabu ndogo ya miaka 50 itolewe kwa watakaotenda kosa hili.

Yote tisa. Kumi: Ni kwamba Mkuu aanze kuwajibika kuendesha kaya badala ya kuwaachia maswahiba na warongo wachache kumchafulia kwa kula bila kunawa huku wakijidai wanawajali wanakaya wanaowatafuna kama keki.

Kidet ina mpango wa kuchapisha kitabu chenye kurasa 1000 kuelezea upya jinsi Kaya inavyoweza kurudishwa kwenye hadhi yake aliyoiacha Musa kabla ya Farao na Delila kuinajisi Kaya takatifu ya watulivu na wenye mapendo vitu vinavyoanza kutumiwa na mafisadi kuwaumiza wanakaya.

Taarifa hii imeandaliwa na Profesa Emiritus Mpayukaji Msemambovu wa Kidet. P.o Box Mafichoni kwa Mfuga mbwa.

mpayukaji@yahoo.com

No comments: