The Chant of Savant

Wednesday 26 December 2007

Siku Boyz II Men walipotumbuiza mbele ya mkuu kijiweni




JUZIJUZI, mkuu wa kijiwe chetu alikuwa ziarani kwenye matanuzi kwenye nchi ya Joji Kichaka Porini, kinara wa kupambana na ugaidi na silaha za maangamizi (WMD).

Nimechagua ubeti huu kwanza baada ya kuusikia na kunikumbusha mkasa na msiba mzima wa njuluku za walipa kodi.

Bado pamoja na kuutwika kwangu ili mawazo yaniishe najiuliza mantiki ya mazingaombwe haya yote!

Je, hili nalo ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuvutia wawekezaji na wachukuaji? Tutajuaje. Huenda na vijana hawa wa Boys II Men wanataka kuwekeza kwenye kusifu ‘mazuri’ ya nchi yetu na awamu hii!

Nikiwa ndiyo natoka kuutwika nilianza kujiimbia lau niliwazike kama mkuu na msafara wake.

Here we’re
at the end of the lies,
things indeed are,
that we’ve gone astray.

But all in all,
I am above all.

Though I’ve to heed the call,
the people are tired of me.

When I came to States,
in the country of riches,
I met with these guys,
The so-called Boys.

They entertained me.

With full of smiles,
I forgot all lies,
though in me,
full of butterflies!

Danganyika my land,
the land of peace.

Some say.

You’re in pieces!

I have my kasi,
I have my buddies
eddie Nazi and Azi.

“We koma, tena ukome kabisa. Hujui siku hizi ung’eng’e si lugha ya siri kama zamani! Hata kama mkuu wetu kijiweni alikwenda kutanua, ulitaka afanye nini iwapo ana nafasi ya kujinafasi? Acha wivu wa kike wewewee!” Nilistukia naongea peke yangu kama chizi! Kumbe na ulevi ni uchizi!

Yes. Ni uchizi hata uwe wa mamlaka. Ulevi ni ulevi tena ni uchizi.

Baada ya kuzideku snaps za mkuu wetu wa kijiweni na vijana wa Boys II Men zilizopigwa na wapiga picha wetu vimbelembele na malimbukeni wenye majina kama ya supu, nilijihisi kupagawa.

Nilijiliwaza kwa kukumbuka nilivyokuwa nikitanua miaka ya 90 enzi za Boyz II Men wakati nikimfuatia mshirika wangu wa bedroom ngomani.

Nilijikuta nikiwakumbuka akina Marc Nelson, Nathan Morris, Michael McCary, Shawn Stockman na Wanya Morris. “Vijana mlitesa kimakwelini wajameni,” nilistukia nikijisemea kabla ya kulamba mweleka kutokana na ulabu.

Ngoja niimbe ubeti huu ambao ulimuingiza kwenye moto mshirika wangu.

Naanza kuimba tena kwa mapozi huku bangi langu likitoa moshi kama dege bovu.

“Well, I can't sleep at night without holding you tight
Girl, each time I try I just break down and cry
Pain in my head oh I'd rather be dead
Spinnin' around and around.”
Naangalia huku na huko na kuendelea kwa pozi kwa sana.

”Ntintiii ntiiitintiii tititi tititi we’ve to goooooo!”
Naanza kuwaza dili. Kutokana na unguli wangu wa kubuni mikakati ya kupona. Naanza kuunda dili baab kubwa.

Nimo mbioni kuunda tuzo ya kiongozi bora wa Kiswahili kwa kutanua na kuruka majuu. Itaitwa Super smart Global-trotter African Ruler of the year.

Najisemea. “Kama Mo ameibuka na tuzo ya kiongozi bora wa Afrika, basi mimi naondoka na mtawala bora wa Afrika katika mambo ya makamuzi.”

Tofauti yangu na Mo ni kwamba yeye kwa kutumia mitandao yake, anakwanyua huku na kupeleka kule. Mimi nitatoa pesa halali ya mauzo ya kahawa pale kijiweni kwangu.

Nitatoa tiketi ya shuttle kwenda kuvinjari kwenye sayari ya Mars. Huwezi kumpa mtu trip ya kwenda Maldives au Island of Man. Hapa ni duniani na isitoshe hakuna jipya zaidi ya kwenda kuficha mishiko ya walipa kodi. Upo mshirika hapo?

Mshindi wa tuzo hii atafaidi sana. Ataruhusiwa kuandamana na maswahiba zake wote, mshirika wa bedroom, vichipukizi vyake, nyumba ndogo, na wapambe wengine hata wawe uchwara. Yeye nao watatesa na kuwa viumbe wa kwanza kujivinjari kwenye sayari hii nyekundu.

Hata Bill Gates na Carlos Salem pamoja na ukwasi wao, hawana jeuri ya kutumia hivi. Wakifanya kosa hili, board of directors za kampuni zao zitawafikisha kwa pilato kama rafiki yangu Conrad Black anayenyea debe kwa kuiibia kampuni yake.

Mzee Warren G Buffet namjua sana. Yeye zake ni kwao Nebraska akiendesha gari chovu utadhani siyo bilionea!

Kwa kutoa pesa yangu ya kahawa kwenye tuzo hii, nitaepusha vimbelembele kuzoa ujiko kwa kumsingizia kuwa mkuu anakwanyua na kufuja njuluku za kodi ya madafu. Kwanza nani afuje vijipesa vya madafu visivyoweza hata kukubalika kwenye nchi jirani zaidi ya mawe yake?

Mkuu poa, kijiwe chako hicho, we kamua wenye wivu wajinyonge.

Mara naanza kuimba. “Wenye nongwa wajinyonge sasa - wenye wivu wajikill.”

Mijitu isiyosoma husema eti mimi ni chizi! Mimi siyo chizi. Ni msomi wa haja. Hivi mijitu hii haioni ninavyotaka kuisaidia na kuleta mapinduzi ya kuokoa njuluku za umma?

Hivi haioni aibu wala kuhisi kichefu chefu kuona mkuu na wapambe wake hata wasio na hadhi wala personality kupanda madege ya kibiashara na kukaa kwenye madaraja ya kifalme - Royal Class?

Kwa vile nyinyi hamjawahi kusafiria ungo na mwewe kama mimi na mkuu na wapambe wake. Acha niwaambie. Ukiwa angani, unaletewa chakula na kinywaji na wasichana warembo wanaotabasamu waitwao Air hostess au wenyeji wa hewani. Ni moto ile mbaya. Wanacheka utadhani wale wa peponi!

Siku hizi madege mengi yana mtandao. Unaona kila nchi unayopita wakati ukisafiri angani kama mwewe.

Nilipokuwa nakwenda kwa Gordon Brown nilipanda mwewe wangu pale NIA na kupita KIA, JKIA huyo zangu Heathrow terminal No.27.

Njiani niliwaona wapambanaji wa Kisudan wakiongozwa na marehemu John Garang Atem de Mabior kwenye milima ya Abyei.

Niliona kasri la Muammar Gaddafi pale Tripoli kabla ya kuona mahekalu ya mabosi wa mafia kule kisiwani Palemo, Utaliano.

Hata Castel Gandolfo anapotanulia Papa nilipaona nikiwa angani. Unafanya mchezo na pipa nini? Hujui utamu wake ndiyo uliwafanya hata akina M7 na Kagame kung’ang’ania maulaji!

Turejee kwenye starehe za Boyz II Men. Mkuu wetu wa kijiwe, kwanza alisikiliza midundo kabla ya kupiga snap ya ukumbusho. Ama kweli Bongo kweli bongolala!

Najikuta nikikumbuka Maiko Jekisoni alipokuja na mipua yake ya kuchonga akapokelewa na mzee wa Ruxa utadhani naye alikuwa politician!

Zama za Mchonga upuuzi kama huu haukuwepo. Yeye zake ilikuwa ni kuwapokea akina Jimmy Carter, Mwenyekiti Mao Tse-Tung na wakubwa wengine si hawa wapiga kelele wa siku hizi.

Nani angemsimamisha Mchonga na wanaume waliovaa hereni utadhani mashoga? Thubutu yako!

Mzee yule alikuwa kiboko bwana. Alikuwa masikini jeuri siyo omba omba kwenye suti kama nilivyoona akina fulani. Baya zaidi tunadanganywa kuwa upuuzi kama huu ungekuwa dili la kutuondoa kwenye mazabe na mizengwe tuliyomo! Jamani acheni hizi tushastuka hata kama mnajifanya hamjali wala kusikia.

Hii inanikumbusha chizi mwenzangu mmoja aitwaye Ansibat Ngurumisha na falsafa zake za nyani kujambia jiwe na kusema, “hata kama umeminya umeipata.”

Naendelea kujisemea. “Naona tuzo kwa mtawala mtanuaji nuksi. Kwanini hii njuluku nisimpe mchonga peni mmoja atakayefichua uhalifu badala ya watu wenye roho mbaya wanaoweza kutanulia pesa ya wachovu huku wachovu wakitanuliwa na ukapa?” Najiuliza.

Kabla ya kuendelea kupanga mikakati yangu mara nakoswa koswa na daladala linalotoka wangu wangu kusaka abiria lau kieleweke.

Nikiwa najiweka vizuri kuendelea kupanga mipango hii ya ukombozi, mara kilonga longa changu kinalia.

”Halloo.” Najibu.

Kumbe ni rafiki yangu wa Inteligence. Alikuwa akinifahamisha kuwa mkuu amegoma kuwatimua mafisadi kwa vile wanaliletea taifa la watu wake faida. Kisimu chenyewe hakina chaji!

Mwe twafa! Richmond utatoa umeme bila Tanesco kutulangua?

Special salaams kwa wapiganaji wenzangu Freddy Macha-Kitoto na Ansbert Ngurumo. Kudos and Alluta Continua guys.

Mpayukaji@yahoo.com

Source: Gazeti la Tanzania Daima J'tano 26 Desemba 2007

1 comment:

Anonymous said...

Kaka wape.
Wape wape vidonge vyao. Wamezidi ujuha na ulimbukeni. Rais mzima naye anakuwa limbukeni na shakunaku!
Kweli mwaka wa kukosa ni wa kukosa. Kikwete-alijisemea Lipumba hafai kuwa hata balozi wa nyumba kumi. Lowassa naye jambazi la majambazi eti waziri mkuu! Kweli nchi ya Mwalimu Nyerere imebakwa na kunajisiwa mchana kweupe!
Msema kweli