Thursday, 6 December 2007

Tutashikiliwa mateka na CCM hadi lini?

MAHATMA Gandhi katika kitabu cha 'Gandhi; his life and message to the world,' Louis Fischer 1954, ukurasa wa 52 aliwahi kusema: "Kama unaamini kuwa Italia ni taifa lenye furaha kwa sababu Waitalia wanatawala Italia, uko kwenye kiza kinene."

Gandhi aliyasema maneno haya kama kejeli na suto kwa Wahindi waliomshinikiza kuwa baada ya kupata uhuru awafukuze Wazungu.

Kwa maana ya kifalsafa, Gandhi alimaanisha kuwa mvunja nchi ni mwananchi na kikulacho kiko nguoni mwako.

Nchi inaweza kudai kuwa iko huru wakati ukweli ni kuwa iko utumwani. Zamani kulikuwa na utumwa, hatimaye ukoloni katika namna tofauti na sasa.

Mifumo hii michafu ya dhambi wakati ule ilitambulika kirahisi kwa nje kutokana na kusimamiwa na kuyanufaisha mataifa ya kivamizi.

Baada ya mataifa mengi kujikomboa, kwa kuwatimua wavamizi, umma uliaminishwa kuwa umepata uhuru uliokuwa ukiukamia na kuupigania hata kwa kumwaga damu. Afrika kwa ujumla na hasa Tanzania, ni mojawapo.

Punde tu baada ya uhuru, yaani kuondoka kwa wavamizi, uliingia ukoloni mpya. Ulikuja ukoloni mbuge na mbalanga ambao ni mchanganyiko wa wakoloni wa awali na wazalendo waliokabidhiwa uhuru. Hiki ni kizalia cha ukoloni mkongwe. Ni mwendelezo wa jinai ile ile.

Badala ya wakoloni kuwa wageni peke yao, ulijengeka uswahiba baina yao na vikundi vya wazalendo wachache na walioendelea kuzikalia nchi huru kwa niaba ya mabwana zao.

Miaka ya 60 hadi 90 Afrika ilishuhudia majanga makuu mawili. Yaani serikali za kijeshi au vyama vya kiimla. Makundi haya mawili, yalizalisha majambazi ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya bara hili.

Kulikuwa na mabwana wawili wakati ule, Urusi kwa upande mmoja na Marekani kwa upande wa pili chini ya dhana ya vita baridi (cold war), vita ambayo ilipiganwa mbali na ardhi ya mabwana hawa. Ilipiganwa Angola, Vietnam, Msumbiji, Congo, Nigeria (Biafra) na kwingineko.

Wakati wakoloni uchwara wakiwatumikia mabwana zao kuzibakana kuzidhoofisha nchi zao wenyewe, hali ya umma ilizidi kudhoofu. Uhuru taratibu uligeuka udhuru. Historia ni ndefu.

Tukirejea Tanzania mwaka 1961 hadi 1967 tuliendelea kuwatumikia Waingereza. Hali hii ilimchukiza Mwalimu Nyerere kiasi cha kuasi mwaka 1967 kwa kutangaza Azimio la Arusha chini ya siasa ya Ujamaa kwa nia nzuri.

Tulianza kujenga jamii ya kijamaa yenye kuheshimu utu na mambo taratibu yalitengamaa. Maana si haba huduma muhimu zilipatika huku utu wa mtu ukithaminiwa kwa usawa.

Kitendo cha kutangaza kujenga ujamaa kilialika maadui wawili, wakoloni wa awali na waroho na walafi wazalendo.

Bahati mbaya Mwalimu aliamini kuwa wazalendo wote walikuwa watu kama yeye asijue kulikuwa na mbweha na fisi.

Walafi hawa taratibu walijipendekeza kwa Mwalimu kiasi cha kuwaamini na kuwapa vyeo. Kosa kubwa. Walianza kutuguguna na kuficha mali za wizi huku wakitunafiki kwa kujionyesha kama wajamaa halisi majukwaani wakati ni mbwa wa kawaida. Kutaharuki mambo yeshaharibika. Nyerere alichukia na kung'atuka.

Baada ya kung'atuka mabwana hawa ndiyo wakawa wamefunguliwa mwaka 1992 chini ya Azimio la Zanzíbar. Historia ni ndefu.

Tukirejea kwenye kichwa cha makala, ni ukweli usio na shaka kuwa kikundi cha watu wachache kiitwacho CCM kimewateka Watanzania na kuwatesa hadi kuchanganyikiwa. Kimevunja misingi ya nchi aliyoipigania Mwalimu. Kimejumuisha mabepari na matajiri wa kila aina na kuuteka na kuuhujumu uhuru wetu. Tutatoa sababu tusionekane tunatukana.

Kwanza, kimekosa mwelekeo, dira, sera, visheni na kanuni. Muulize hata mwenyekiti wake kuwa sera ya chama ni ipi. Muulize mwanachama yeyote kwamba anashirikishwa vipi kukiendesha chama na vitu kama hivyo. Atatoa macho kama mjusi aliyebanwa mlango.

Atajibu nini iwapo chama sasa ni ngazi ya kupatia madaraka na ulaji wa bure? Si tena kile cha Mwalimu kilichokuwa nyenzo ya ukombozi. Hakijitangazi kama zamani.

Kwanini kujitangaza iwapo rushwa inaweza kutumika kupata uanachama au madaraka?

Kinajitangaza kwa ghiliba, rushwa (takrima) na jinai nyingine. Kimekuwa chama kama kokoro, kinahudumia yeyote awaye ilimradi awe na pesa. Na huu ndiyo mzizi wa kuharibika kwa chama. Ulizia miiko ya mwanachama na ya uongozi.

Pili, kimeishiwa mbinu za kisiasa kiasi cha kutegemea njia haramu ili kuishi, hasa madarakani.

Rejea kutokuwa tayari kubadili katiba isiyoendana na matakwa ya nchi ya sasa, wizi na uvurugaji wa uchaguzi.

Tatu, ni kufilisika na kukaukiwa na watu wenye sifa za kukiendesha kisiasa na kihalali kama alivyofanya Mwalimu. Hakina watu waadilifu kama kina Nyerere, Edward Sokoine, Horace Kolimba na wengine. Waliobakia hawana madaraka wala hawasikilizwi, ukiachia mbali kukata tamaa kuona chama chao kilivyogeuzwa cha ovyo.

Nne, kama kansa, kimewaghilibu hata wasomi kiasi cha kuwa watu wa ajabu. Usishangae kuona kwa mfano majaji, maprofesa, maofisa wengine ambao nafasi zao haziwaruhusu ama kuwa na kadi za vyama au kujikomba, wakiishi kwa kuganga njaa kwa kukubali kutumiwa na CCM.

Tulishuhudia siku za nyuma, Mwanasheria Mkuu wa Zanzíbar anayeitwa Jaji akiacha kiti na cheo cha ujaji kwa kwenda kuchukua fomu kugombea ujumbe wa NEC.

Hivi jaji mwenye kushabikia chama au kuwa mwanachama anaweza kutoa haki? Hii si mara ya kwanza. Kwani IGP aliyestaafu Omari Mahita alikuwa shabiki na mwanachama wa CCM wazi wazi, akiwa kwenye ofisi ya umma si ya chama na hakuchukuliwa hatua zozote!

Huu ni ujambazi wa kisiasa unaoendeshwa na chama tawala dhidi ya nchi na wananchi wake kwa sababu ya kufilisika na tamaa za watu wachache. Ni usaliti kwa Mwalimu.

Si kosa kusema kuwa CCM sasa ni chaka la mabepari na walaji. Rejea mfano kuwaona walioua mradi wa mabasi ya wanafunzi kuchaguliwa kuwa wabunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM. Rejea utajiri usio na maelezo wa viongozi wa CCM. Rejea kushamiri kwa tuhuma za wizi na ubadhirifu wa pesa ya umma unaofanywa na serikali ya CCM. Rejea matajiri kujipatia ubunge kupitia CCM kwa kuwahonga viongozi wa CCM na wapiga kura.

Hivi hawa wabunge wenye asili ya Kiasia, waliotoka shule jana, wakaishia kuwa wabunge kama si takrima, wana sifa gani? Rejea kutegemea mtandao kuhujumu vyama vingine vya upinzani.

Nafasi haitoshi, historia ni ndefu. Tutaendelea kuwa mateka wa CCM hadi lini? Anayedhani Tanzania ni taifa lenye furaha kwa vile wanaongoza Watanzania, yumo kwenye kiza kinene.

nkwazigatsha@yahoo.com

No comments: