Friday, 8 February 2008

Kwako Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Je umeamua kuzaliwa upya au?

Laiti ungetoa hotuba kama dreams of a Goon!

Kwanza nikupongeze kwa kuunda tume ya Mwakyembe na kukubali kuwajibika kwa waziri wako mkuu wa zamani Edward Lowassa mbali na kutangaza mkakati mpya kabambe kwa ajili ya taifa letu.

Ukisoma hotuba ya rais wakati wa kuomba kupewa muda aweke mambo sawa na kukubali kujiuzulu kwa rafiki yake na waziri wake mkuu, kama itafanyiwa kazi neno baada ya neno kuna mambo mengi yanaibuka. Je ni maneno matupu au tutegemee matendo?

Pili je rais asipofanya aliyoahidi kipindi hiki tena kwa hiari yake wananchi tufanye nini.

Hakuna maneno niliyoyapa uzito kama, "Tatu, nawahimiza viongozi wote waliojihusisha na ufisadi wowote wa kimsingi kama kwenye mikataba ya madini, Netgroup Solutions, Uuzaji wa Mashirika na Raslimali za Umma, Ununuzi wa rada na ndege ya Rais, Ununuzi wa vifaa vya Jeshi, Mikataba na TANESCO kama IPTL, Kiwira, nk, wakiri kwangu kimaandishi kushiriki kwao na kuorodhesha mali walizopata kutokana na matendo hayo. Wakifanya hivyo sitawachukulia hatua za kisheria ila nitawasimamisha kazi ya umma na kurudisha mali ya wananchi panapohusika."

Je hapa rais mstaafu Benjamin Mkapa, mkewe, mwanawe, na maswahiba zake wa TanPower, ANBEN, Fosnik watanusurika? Je Kikwete ameamua kumpiga mtama Kikwete aliyekuwa ametekwa na wapambe kiasi cha kuyapindua maneno na nadhiri zake dhidi ya kumfungulia mashitaka na kumchunguza Mkapa? Yetu masikio na macho.


Hebu soma maneno haya na uyapigie mstari. "Pili, natangaza kugandisha (to freeze) akaunti zote za mali za wale waliohusika na shutuma za Richmond , na BoT, pamoja na kushika rehani mali zao zote zisizohamishika kwa nia ya kurudishia serikali mali yoote ambayo inaweza kuwa iliibiwa na washutumiwa. Ili wasife njaa serikali itaendelea kuwalipa nusu mshahara hadi uchunguzi au mashtaka kumalizika" Je rais ataruhusu umma utangaziwe ni mali gani na zipi ziko wapi na za nani zitakuwa-frozen ili kuepuka mizengwe ambayo tumeishazoea?

Juzi tuliambiwa Jeetu Patel yuko Dubai akitanulia pesa yetu. Je hawa ambao wanatuhumiwa na hawajakimbia nchi atatuhakikishiaje hawafanyi kama Jeetu? Na je atatoa oda akina Jeetu na Ballali warejeshwe mara moja ili washughulikiwe?

Ningeomba nimsogeze mbele zaidi kumtaka na mkurugenzi wa TAKUKURU-Edward Hosea awajibike mara moja huku mawaziri kama Andrew Chenge, Basil Mramba, Edward Lowassa wawekwe chini ya ulinzi/ uchunguzi mara moja.

Pia isisahaulike. Watu kama Rostam Aziz aliyetajwa na Bangusilo Ibrahim Msabaha mbali na kutajwa na vyombo vya habari mara kwa mara asiponyoke. Hapa Habari Corporation lazima imulikwe zaidi na zaidi.

Pia kwenye ofisi yake rais kwenye kitengo cha habari kuna mtu aliyeteuliwa hivi karibuni. Amelalamikiwa sana. Naye madhara ya kazi ya kalamu yake si kidogo ahusike mara moja.

Kwa vile rais ameamua kuwa rais wa watu badala ya kuwa adui wa watu kama tulivyokuwa tumeanza kumchukulia. Azidi kwenda mbele. Afagie kuanzia chumba cha kulala. NGO ya mkewe isimamishwe mara moja.

Na si hilo tu. Afanye kama Bingu wa Mutharika aliyewafikisha mahakamani wale waliojidai walihoga ili achaguliwe. Kama nasi kwetu kama inavyosemekana hili lilifanyika-na inavyoonekana lilifanyika hata kama ni kwa faida ya rais basi wahusika wachukuliwe hatua sawa na waharifu wowote bila kujali ukubwa wala ushawishi wao kwake. Hapa ndipo kesi ya Ditopile Mzuzuri inapofufuka na kutaka uchunguzi upya.

Leo tunawajua watu waliochezea uchumi wetu. Bahati nzuri rais amewataja. Ametaja Net Solution na mengine. Amesahau NBC, IPTL, mbuga za wanyama, TRA, Bandari na kwingineko.

Kama rais ameamua kuisafisha nyumba yake. Basi aombe taarifa toka kwa umma ili mambo yawekwe hadharani. Kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kuudhihirishia umma kuwa Kikwete ameamua kuzaliwa upya.

Kitu kingine alichokitaja rais ni kuiondoa nchi kwenye utawala wa kiimla. Hii maana yake ni kwamba aridhie haraka kuandikwa upya kwa katiba ya nchi. Maana kinachogomba hapa siyo personality bali mfumo mzima unaohitaji kuwa overhauled. Kwa kuandika katiba upya, tutawabana watawala wote wanaoondoka madarakani kwa kashfa kama Mkapa na Lowassa wasiendelee kuchezea pesa zetu kwa kulipwa malipo ya kustaafu wakati hawakuwahi kutufanyia kazi. Kwa sasa wanatuibia sawa na yaya aliyemuua mtoto wako ukamzawadia gari na nyumba.

Bila kuandika katiba upya, yote itakuwa bure sawa na kupaka rangi bahari au upepo. Nani chizi afanye hivi au akubali kufanyiwa hivi?

Sehemu nyingine ambayo ni mama wa yote haya ni CCM. Siyo uzushi kuwa CCM inanuka na imetekwa na wasaka ngawira. Kama alivyosema marehemu Horace Kolimba, CCM imepoteze mwelekeo. Iko wapi miiko ya uongozi?


Tufikie mahali tufanye kama nchi za wenzetu. Nitatoa mfano kwa Kanada ninapoishi. Huwezi kununua gari au mali yoyote bila kuonyesha ulivyopata hiyo pesa. Tusidanganyike na ubinafsishaji na uongo wa uchumi wa kisasa alioozoea kutufungia kamba Mkapa. Kuna uchumi wa kisasa kama wa Marekani au Kanada duniani? Huku watu wanaogopa ufisadi. Si wananchi wa kawaida wala si viongozi. Kila mmoja anaogopa ufisadi. Maana kwa mifumo yao si rahisi kuficha chumo la wizi.

Leo tuna watu matapeli matajiri wa kutupa ilhali tukijua walivyopata kwa njia za wizi. Hawa nao washughulikiwe kuanzia mwenye kumilki dala dala hadi kiwanda.

Mapato ya watanzania yafahamike na kudhibitiwa vinginevyo tunapoteza muda.

Pia mradi wa vitambulisho vya umma uharakishwe huku kila ofisi zikiwa computerized haraka sana. Huku kinachofanya iwe vigumu mtu kuuibia umma licha ya mfumo ni matumizi ya Kompyuta. Kila mwananchi mwenye kitambulisho au mkazi wa kudumu wa Kanada taarifa zake ziko kwenye national data base. Huwezi kukwepa kitu hapa. na ndiyo maana hata wahindi waliozoea kuja Tanzania ni mataxi drivers na wafagizi hapa.

Tufikie mahali tutumie elimu yetu vizuri. Tuchunguzane na kutiliana shaka kuanzia rais hadi Matonya. Rais kama atadhamiria kufanya haya sina shaka ataleta mapinduzi na ukombozi kwa mwananchi vinavyoweza kuliondoa bara letu kwenye makucha ya akina moneybags wa ndani na wa nje.

Leo tunawacheka wakenya. Hakika yaliyopita Kenya yangepita Tanzania nchi ingesambaratika. Kinachoendelea kuwastiri ni uchumi wao ingawa nao unamilkiwa na mbweha wachache wa ndani na kihindi.

Tukirejea kwa Kikwete, wapo watu hata kama ni kwa kujikomba waliandika kuwa ni tumaini lililorejea ambalo baadaye lilitolewa kwenye kuwa a man of the people kwenda kuwa enemy of the people. Basi tunataka tumaini hili lirejee haraka sana iwezekanavyo. Rais aseme anachomaanisha na kumaanisha anachosema vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji.

Kitu kingine muhimu na lazima. Ziundwe taasisi huru za uchunguzi na usalama wa taifa zinazochunguzana kama M6, Scotland yard. Hizi ziwe mamlaka huru zisizozidiana mamlaka wala kuingiliana. Hapa ndipo wakubwa watashika adabu. Maana hakuna atakayejua anayemchunguza.

Tusisahau bunge na mahakama kuwa huru dhidi ya utawala. vyombo hivi virejeshwe kwenye maagizo ya Montesqui ya separation of powers kama mwongozo wa utawala bora.

Pia watumishi wa taasisi za kupambana na kuzuia rushwa-TAKUKURU wachunguzwe wote halafu ivunjwe. Maana kama iliweza kuisafisha Richmond tena kwa kutumia pesa ya umma, ni mshiriki wa ujambazi-conpirant.

Ukitaka kumuua nyani usimuangalie usoni kama ilivyotokea kwenye sakata la Richmond.

Pia tujenge taasisi huru za habari. Hii maana yake ni kwamba vyombo vya habari viwe fourth estate kweli kweli. Visihujumiwe kwa kunyimwa matangazo kama ilivyokuwa simply because vinaisema vibaya serikali. Nani atakusema vibaya kama unatenda mema. Ingekuwa hivyo basi Yesu na Mohamad wasingekuwa maarufu sasa.

Nihitimishe kwa kumkumbusha rais kuwa moto aliouanzisha kwa kuanzisha tume ya rais ya Mwakyembe ni sawa na msumeno. Unakata kule na kuno. Awe mkweli na tayari kuyapokea mageuzi na changamoto zake.
Mungu ibariki Tanzania.

Nkwazi Nkuzi Mhango,
St. John’s NL
Kanada.

No comments: