Thursday, 7 February 2008

Sifa, sura na matendo ya Lowassa Kasi mpya msambweni.Tulisema na kuandika. Tulikumbushia na kushinikiza. Mwanzoni tulionekana kama wachonganishi na wambea wa kawaida. Tulizodolewa na kutungiwa majina na tambo na mashairi kila aina. Ama kweli hekima ya siafu kufia kwenye mzoga imedhihiri!

Hakuna siku simu yangu ilipata kazi kama tarehe 6 Februari siku moja baada ya chama cha mapinduzi kinachounda serikali tawala ya awamu ya nne kutimiza miaka 31.

Bado nakumbuka jana yake nilikuwa nimetoa changamoto kwa taifa kuwa CCM inaweza kuchagua kuendelea kubinafsishwa kwa watu wabinafsi na wafanyabiashara wa roho na miili ya binadamu. Nakumbuka Kijiwe na ukenge wa kuiona mvua na kukimbilia baharini. Nakumbuka mstari wa mwisho kuwa wabunge wamfichue habithi aliyeko nyuma ya Richmond ambaye nimekuwa nikimsaka na kumpa vijembe vyake.

Nilionya: umefika wakati wa wana-CCM wenye mapenzi na nchi yao kukipoka na kukirejesha chama chao mikononi mwa umma kama alivyokiacha mwanzilishi wake marehemu Mwalimu Julius Nyerere ambaye nadhani huko aliko atakuwa mwenye furaha na matumaini.

Nani amesahau tulivyoonya kuwa mambo ya serikali hayapatani na mambo ya urafiki? Bado nakumbuka nilivyohanikiza kupinga kuteuliwa kwa waziri Mkuu, Edward Ngoyai Lowassa swahaba mkuu wa rais Jakaya Kikwete na wale wote waliopata madaraka kwa mgongo wa urafiki au jeuri ya pesa yao.

Sasa imebainika kuwa Edward Lowassa alishinikiza kuridhiwa kwa kampuni tata ya Richmond kupewa tenda kinyume kabisa cha sheria na matarajio ya wengi. Amelazimika kujiuzulu. Huu ni ushahidi tosha kilichogunduliwa na tume ni kweli. Imebaki ni kitendawili ilikuwaje mtu mwenye cheo na dhamana kubwa kiasi hicho kuridhia kampuni ya mfukoni kupewa tenda ya kitaifa!

Maneno yangu na watu wengine kama Ansbert Ngurumo na wengine yalionekana kama kutafuta sifa hata kunyimwa ulaji katika genge jipya ndani ya ikulu. Niliuita mfumo huu ukuku, usindano, ufisi, unepi na majina mengine mengi tu.

Namshukuru Subhana sikukata tamaa wala kutetereka. Mpayukaji kama ada, nilizidi kupayuka nikihakikisha neno Richmond, IPTL, ANBEN na madudu mengine hayakauki mdomoni wala kwenye ukurusa wangu hasa Jicho la Kijiweni.

Nisiwachoshe kwa nilisema nini. Kwanza licha ya kutumia Kijiwe kuuamsha na kuuleta mbele ya hadhira mzimu wa Richmond, nilitunga kitabu kiitwacho "Nyuma ya Pazia" ambapo mhusika mkuu ni waziri mkubwa aitwaye Edmond Mpendamali Mwaluwasha wa nchi ya Mafuriko ya utajiri yenye mafuriko ya umaskini ambaye anaiingiza kampuni feki ya Richmen kwenye nchi ili kujenga mabwawa ya maji wakati ni kampuni ya kutengeneza dawa za kuulia wadudu.

Waziri huyu ambaye ni swahiba wa Rais, akishirikiana na waziri Niziro Mulangila Kadamage na katibu wa wizara Geryy Tamaa Mgonjwa na wengine, wanaliingiza taifa la Mafuriko kwenye matataizo. Uchafu huu wa kutisha unafichuliwa na gazeti maarufu la Chimbuchimbu hadi unaitikisa nchi na mwisho wa yote umma unashinda.

Stori ni ndefu. Nilichofanya ni kuandika kitabu kama alivyofanya Mwalimu kwenye Hatima ya Tanzania baada ya kuona mambo si mambo. Kitabu hiki Mungu akijalia, kitasomwa nchi nzima karibuni.


Tukirejea kwenye dhima ya kuandika waraka huu maalumu, sitaacha kuwapongeza waandishi wa habari na kamati iliyowaletea watanzania faraja kwa kupiga pale pale siyo -to beat around the bush. Tumetumbua jipu.

Nimefarijika kuandika. Ni kwa sababu watu wetu wameamka na kuanza kuiona njia waliyoonyeshwa na Musa-Mwalimu Julius Nyerere. Wameukataa urafiki na unafiki. Wanataka watendewe kama walivyoahidiwa na siyo kutendewa kama vihongwe. Wameukataa ukuku dhidi ya ufisi niliokuwa nikiongelea kwenye makala zangu. Wamejitenga na usindano na uumbwa kushona nguo nyingi na kulinda mali nyingi lakini mbwa na sindano wakaishia kuwa uchi na maskini wa kutupwa. Wamefanya mapinduzi ya kifikra mchana kweupe.

Tulisema na tutasema: serikali ya awamu ya nne lazima ijitofautishe na ile ya awamu ya tatu. Iturejeshee nchi na heshima yetu vilivyokuwa vimewekezwa kwenye mifuko ya watu wenye uchoyo na ufisi huku wakitugeuza sindano na kuku atagaye mayai vicheche wakajichukulia halafu wakarudi kumaliza hata na vifaranga vilivyonusurika kwenye wizi wa mayai yake.

Kilichofanyika ni watanzania kusema tena kwa herufi kubwa: TUNAITAKA NCHI YETU NA RASLIMALI ZAKE. TUNAITAKA KAMA TULIVYOPEWA NA MUNGU NA TUNASEMA ASIYETAKA KUTUPA NCHI YETU AJIANDAE MAANA HII NI NCHI YETU SIYO YAKE WALA MAMA YAKE.

Leo nina furaha japo jana sikulala. Ningelalaje iwapo simu zilikuwa zikishindana kunipongeza na kunipa sura ya mambo yanayoendelea? Nakumbuka simu ya kwanza ilitoka kwa Uingereza kwa swahiba na mpambanaji mwenzangu, Ansbert Ngurumo. Tuliongea masuala haya kwa zaidi ya saa nzima. Nilijaribu kujilaza kidogo kufanya tafakuri. Mara Martin Malera akanipigia kunipa mhutasari wa impasse iliyokuwa ikiendelea nchini mwangu.

Hii niiache; ilikuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida. Tukija kwenye kilichofichuliwa na kamati maarufu ya Mwakyembe, hii ni ndumo; kuwa sasa watawala wanaojificha nyuma ya madaraka na vikorombwezo vyake, wakae chonjo mambo yamebadilika.

Ni tangazo; kuwa madai yetu na madeni yetu lazima yalipwe tena leo leo. tumemsaidia Kikwete mara nyingi dhidi ya vinyamkera waliomzunguka wengi wakiwa wenzetu wakiimba utukufu badala ya utukutu. Leo haki imedhihiri. Tulianza na Ballali sasa moto utawaka hadi wote tunaowajua wanaong’ang’ania kwenye ofisi zetu wakizifanya zao kana kwamba sisi ni hayawani.

Tunataka Richmond iwekwe msalabani. Tunataka na ule mzimu mama na baba wa wizi wa pesa zetu IPTL ufufuliwe na kudurusiwa upya. Tunata ANBEN, Tanpower, Fosnik na madudu mengine tuyajuayo vifanyiwe kazi. tunamtaka mwanzilishi wa machukizo haya, Benjamin Mkapa kwenye mahakama ya umma. Lazima naye kama Fredrick Chiluba, avuliwe kinga; ili haki itendeke. Tunataka; sasa tumbane zaidi Kikwete aunde serikali ya watanzania na siyo ya marafiki.

Tunaitaka Tanzania kama ilivyo. Tunata serikali ifanye kazi iliyoahidi kuifanya badala ya mazingaombwe, kujuana, kulindana na kulipana fadhila. Hakika watanzania wameamka na kuitwaa nchi yao kwa njia ya amani. Tumejifunza yaliyotokea Kenya na hatuwezi kuwa vipofu na vichaa kuumwa nyoka kwenye shimo moja mara mbili.
Sifa, sura na matendo ya Lowassa Kasi mpya msambweni. Ni kichwa cha makala hii. Je yaliyoibuliwa na tume ya Mwakyembe yametufundisha nini? Siyo kila ving’aravyo ni dhahabu na lisemwalo lipo; kama halipo laja. Na kubwa zaidi ya yote ni asiyesikia la mkuu mguuni huota tende. Mwalimu Nyerere alitwambia: kuna watu wana mali nyingi walizojilimbikizia kwa njia zisizoeleweka. Leo tumejaza watoto wa wakubwa BoT. Leo tuna matajiri majambazi ambao sifa ya kuufikia ukwasi huo ni kujuana na wenye madaraka. Lakini wanafanya kosa. Maana, wenye madaraka ni umma ambao unapoamua hakuna wa kuuzuia. Tujikumbushe yaliyotekea Poland, Romania, Iran,Afrika ya Kusini na kwingineko.

Kitu kingine tunachoona ni somo ni kwamba rais kuanzia sasa aanze kuusikiliza umma badala ya wapambe na walamba viatu ambao wengi wanatumikia matumbo yao wakimtumia rais kama kifaa. Tunamtaka rais arejee kwa waliomchagua. Tunataka wote waliohusika na wizi wa pesa yetu sisi watu maskini wawajibike na mali zetu zirejeshwe kuanzia pesa, vyeo, majumba na mstakabali wetu kama taifa na jamii. Hakika haya ni mapinduzi adhimu ya kifikra dhidi ya ulafu, unafiki, usanii na kila aina ya ghilba na hadaa.

Mwenzio akinyolewa tia maji. Je hili la Lowassa ni mwanzo wa mwisho wa siasa za biashara na usanii katika ofisi za umma? Je atakayefuata ni nani? Je Lowassa alikuwa peke yake na ni wa mwisho? Je kuna mkubwa zaidi yake? Je huu ni mwanzo wa mwisho au mwisho wa mwanzo? Time will tell and I am sure it will rightly and accurately tell.


Siwezi kumaliza makala hii maalumu bila kumpongeza na kumpa pole Edward Lowassa ambaye kwa kung’amua ukweli aliamua kujiuzulu bila kusukumwa sukumwa kama baadhi ya mawaziri wake wanaoendelea kukaa maofisini ili waharibu ushahidi na hatimaye wanusurike. Nasema hawatanusurika hata kwa chembe. Nasema hawana pa kujificha. Nasema wasijidanganye wakadhani watatudanganya kama ambavyo wamekuwa wakifanya. Hakika za mwizi arobaini.

Kwa rais Kikwete, asiyekubali kushindwa si mshindani na we learn through mistakes. Kaa. Tulia. Anza alifu na ujiti kabla umma haujageuza meza dhidi yako. Wewe uliwaaminisha wananchi unawafaa. Uliapa peke yako na siyo na marafiki wala watangulizi wako. Basi kaka rejea viapo vyako uchape kazi. watanzania siyo wapenda makuu. Ukirejea kwenye mstari wanaweza kukusamehe. Lakini jua kabisa CCM haina cha mswalie Mtume lazima ibadilike kabla haijabadilishwa kutoka aliye hai kwenda marehemu.
Hakika ni ushindi tushangilie na kuimba lakini tusibweteke kwani mapambano ndiyo yanaanza. Na ni mapambano magumu na ya muda mrefu. Hakika yaliyojiri ni mwanzo wa mwisho wa ngebe. na hakika Sura na tabia ya Lowassa kasi mpya msambweni. Je tutegemee nini zaidi.
Mungu ibariki Tanzania.
Alluta continua.

1 comment:

Anonymous said...

Bwana Mpayukaji,
Nimetokea kuwa muumini wa makala zako kali.
Ni kweli watanzania huenda wameanza kusikia na kuchukua hatua.
Lowassa na Rostam Aziz walikuwa kikwazo na hatari kwa taifa letu.
Rostam rudi kwenu Iran ukafanye ugaidi.
Lowassa rudi Arusha ukauze maziwa.