Monday, 4 February 2008

Mkapa, Kikwete, ufisadi na kelele za inzi!


JIKUMBUSHE kelele za inzi zinapokuwa kwenye mzoga, halafu akaja mbweha au mbwa ama hata kicheche kuushambulia mzoga huo. Inzi huhanikiza na kupiga kelele kama silaha pekee waliyonayo wadudu hao.

Hata hivyo kelele za inzi huwa hazimzuii mvamizi kula mzoga atakavyo na wakati mwingine huwala inzi hao na wasifanye kitu! Hawa ni hayawani isitoshe wadogo wasio na misuli na vikumbo kuweza kupambana na mvamizi.

Jaribu mfano mwingine wa vyura pale tembo avamiapo bwawa kunywa au kuoga na kuyachafua maji. Vyura, kama inzi, nao hupiga kelele hadi mswahili akawazodoa; kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji.

Mswahili huyu huyu, bingwa wa falsafa na hata mafumbo, haishii hapo, husema; kelele za mlango hazimnyimi mpangaji usingizi.

Ukiangalia mazingaombwe, usanii, ujambazi na kila hadaa vinavyofanyika 'kuwanusuru' watuhumiwa wizi wa mabilioni ya pesa kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA), bila shaka unaijiwa na picha hizi tatu.

Ni somo gani unapata hapa? Kwanza ni uhovyo wa inzi, vyura na mlango. Pia ni uonevu wa tembo, mbweha, mbwa, vicheche (mvamizi).

Pili ni hekima. Tusifanye mambo kama mahayawani. Tusiridhike na kelele ilhali 'wabaya wetu wakiendelea kuukatua mzoga, kuchafua na kunywa maji au kuuchapa usingizi. Je nasi tumekuwa wa hovyo kama wao? Je tumekuwa katili kwa vizazi vijavyo kwa kuendekeza woga na kelele ilhali mambo yanazidi kuharibika?

Kujibu maswali haya vizuri, jiulize, mbali na kelele na ngebe, watanzania wamefanya nini kuzuia mzoga wao kushambuliwa na wanyama tajwa wanaojulikana kwa uchoyo na ulafu wao? Wamefanya nini pale waliyemtegemea atende haki kwa kumkabidhi ofisi na zana zote za dola ameamua kuzitumia dhidi yao kuwalinda mafisadi?

Je, kwa msimamo wa Rais Jakaya Kikwete, kwa mfano kusema wazi hatamchunguza mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, si kuusaliti umma na viapo vyake vya ofisi? Maana wahenga husema; asiyevuta kamba nasi si mwenzetu ilhali Waingereza wakisema; 'show me your friend I shall tell you who you are', ama nionyeshe marafiki zako nikwambie wewe ni nani? Je, katika hili Kikwete ni nani? Sitaki nimjibie.

Taarifa za vyombo vya habari kuwa uchunguzi wa kashfa ya BoT, jina la rais mstaafu linajitokeza mara nyingi si za kuacha kama taarifa tu, bali onyo kuwa Watanzania hawajiandai kupambana na ufisadi wala kurejesha mali zao zilizomo mikononi mwa mafisadi, ambao kwa bahati mbaya wengine bado wamo kwenye ofisi za umma, wakiharibu ushahidi.

Inashangaza udhati wa Kikwete kuweza kulala usingizi hata kujitahidi kuwaridhisha wananchi; 'ntapambana na ufisadi' wakati ukweli ni kwamba kinachofanyika na kinachosemwa ni tofauti kama usiku na mchana au mbingu na ardhi! Je umma haujaona mchezo mzima?

Niliwahi kuuliza; kama Mkapa ana kinga na mkewe, mwanae na washirika kwenye makampuni yao nao wana kinga? Mbona hawakuwa marais hata kwa sekunde moja? Au ni yale yale ya ufalme wa mlango wa nyuma? Au tuseme ni yale yale ya waarabu wa Pemba?

Kwa nini hatutaki kuwaambia watawala kuwa, hii ni nchi yetu na siyo yao wala mama zao? Kwanini tunaogopa hata kuchukia kama tumeshindwa kuondosha kwa mkono?

Leo ufisadi wa BoT umebebwa na Dk. Daudi Ballali, gavana wa BoT wa zamani, utadhani alikuwa peke yake! Kwa nini tunachezewa mahepe mchana kama watoto wadogo nasi tunaupwakia uongo na matusi haya?

Tuliwahi kuuliza na kudodosa alipopata na alivyopata mali zinazosikika kuwa za Mkapa, kama vile majumba ya Lushoto, Upanga na mengine ambayo bado hayajajulikana. Tulidhani umma ungetumia hojaji zetu kudai haki kwanza na kama madai hayasikilizwi basi uchukue mali zake au hatua mujarabu. Lakini wapi?

Tuliwahi kuhoji; nani anamfanya nani bwege? Tulihoji; kazi ya rais ni nini na ipi iwapo anatuzodoa tena hadharani; hawezi kumchunguza Mkapa achilia mbali kumfikisha mbele ya haki? Je, hatujawa inzi tena waliokufa? Ajabu ya nchi yetu, tuko tayari kuandamana hata kupambana na FFU kwa mambo madogo kama kashfa za kidini na mengine, lakini hatuna mshipa wa kusimamia haki zetu zitendeke na kulindwa?

Je, rais na watendaji wake wanajua uhovyo wetu kiasi cha kututendea mambo ya hovyo hivi? Je, kwa kutenda hivi wahusika nao hawajawa wa hovyo kiasi cha kuwa na nchi hata jamii ya hovyo? Je, mwelekeo wa hali hii ni nini kama siyo miaka mitano ijayo kushuhudia makubwa kuliko hata haya ya Mkapa? Je, hatujawa kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi kuonya mzee Ruksa? Hatujawa inzi wafu?

Ajabu ya maajabu, vijana wetu wengi wamegeukia jinai kama ujambazi, hata uchangudoa ambao kimsingi vinaweza kuondoa uhai wao ilhali kudai haki halali kumetelekezwa! Kiongozi na shujaa wa Mau Mau kule Kenya, Dedan Kimathi aliwahi kusema; heri kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti. Tuko wapi sasa?

Nchi jirani ya Ethiopia, kuna kabila la Oromo ambalo kwenye lugha yake ya Oromia kuna methali isemayo; 'heri kuishi siku moja kama simba kuliko miaka mia kama kondoo.' Je, sisi hatujawa kondoo tena wa shughuli ya fisi?

Kuna haja ya kuwatolea uvivu watawala wetu na kuwaambia Tanzania si yao peke yao, ni yetu sote kwa sawa. Badala ya kunung'unika na hata kumlilia Marehemu Mwalimu Nyerere au kuotea atakuja malaika kutukomboa, tuamke na kurejesha nchi yetu mikononi mwetu.

Inashangaza na vyombo vya dola vyenye watendaji kama polisi na idara nyingine vimeridhia uhovyo huu wa inzi!

Kama Kikwete alituahidi kututumikia na siyo kututumia kama ilivyo, basi atutumikie. Kama ameshindwa, kwa nini tusitafute mwingine ambaye yuko tayari na mwenye uwezo wa kufanya hivyo badala ya kuishi kama inzi?

Tumekuwa tukimuogopa Kikwete hata waziri wake mkuu, tunawaandika kwa kuzungusha, tunatumia lugha za kinafiki za mheshimiwa rais angefanya hivi au vile.

Jamani, tumwambie hata kama atachukia kuwa anakotupeleka na anavyotuswaga sivyo tulivyo kubaliana, tulimchagua awe mtumishi wetu si bwana wetu kama ilivyo. Anayebishia hili aangalie utendaji mbovu wa Serikali ya Awamu ya Nne tangu iingie madarakani.

Ajiulize ni mangapi tuliyokubaliana yametimizwa zaidi ya danadana na mazingaombwe kama wengine wanavyoita. Je, kwa Mkapa kuendelea kutuchezea na kutudharau, haimaanishi bado anatawala kwa mlango wa nyuma? Je, nani anapenda kuwa na hali ya ukatuni (Caricuture).

Maswali ni mengi! nani anautaka 'u-joice' wowowo! Mkumbukeni joyce wowowo akinengua baada ya amchezeshaye kutia madole kwenye kijisanduku naye akamwaga burudani lakini kwa mikatiko ya matusi. Je tumekuwa wa hovyo kushabikia matusi haya? Kwa nini hataki kukubaliana na ushauri unaotolewa na wengi ukimtaka avunje ukimya, Je, atafanya hivyo? Je, kama Mkapa na Kikwete wataendelea mchezo huu, utabiri wa mawe kusema kwa namna tofauti na inzi ya kwenye mzoga utatimia taratibu?

Kwa nini Mkapa anaonekana kuwa na kiburi? Je, ni kwa kujua sisi ni inzi au ukubwa wa kinga ya Kikwete? Je, kwa nini Kikwete naye anaridhia kadhia hii kama hana mpango wa kuitenda hata zaidi ya hii? Siku njema huonekana asubuhi, si jioni. Sasa ni zaidi ya miaka miwili tangu Kikwete akabidhiwe nchi. Je kuna ishara gani kutokana na matendo ya awamu yake?

Kikwete asijesema nampakazia. Akinipa sababu zenye siha hata mbili za kwa nini Mkapa asishughulikiwe na yeye hana mpango wa kuwa Mkapa mwingine miaka ijayo, nitaacha kuuliza swali langu kuu, kwanini Kikwete na Mkapa lao lisiwe moja.

Muda umeisha, Mkapa anapaswa kujitokeza, azungumze kuhusu tuhuma hizi zinazoelekezwa kwake, asiliwalazimishwe Watanzania kuamini kuwa wakati wao wanapiga kelele za kumtaka atoe maelezo hukusu tuhuma hizo, yeye anawacheka badala ya kuomboleza.


Source: Tanzania Daima, Februari 3, 2008

mpayukaji@yahoo.com

No comments: