The Chant of Savant

Wednesday 20 February 2008

Rais Kikwete asijisifu kumkaribisha Bush

ZIARA ya Rais wa Marekani, George Bush, ni turufu kwa Rais Jakaya Kikwete na wote wanaoona karibu.

Nasema kwa wanaoona karibu kutokana na jinsi Bush alivyopokewa kwa mbwembwe, unyanyasaji na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Nasema hivyo kutokana na mambo yalivyokuwa. Wapo walioandamana kupinga ujio wake ingawa nao walikuwa na hoja dhaifu ya kidini badala ya kitaifa.

Kutokana na mazoea na hali halisi nchini mwake hata nchi nyingine alizowahi kuzuru, sijawahi kuona mitaa ya Toronto ikifungwa eti kwa sababu kaja Bush! Sijawahi kuona hata mitaa ya Maine, ikifungwa eti kwa sababu yupo Bush, tena kuwatembelea wazazi wake.

Julai mwaka jana, alipokuwa Kennebunk port, Maine na mgeni wake Rais wa Urusi, Vladimir Putin, nilikuwa Buffalo. Sikuona ‘ujinga’ kama huu ulioonyeshwa na watawala wetu Dar es Salaam ambapo barabara zilifungwa huku wananchi wanaokwenda na kutoka kwenye shughuli zao halali wakikosa huduma ya lazima ambayo ni matokeo ya kodi zao!

Tukija kwenye hoja ya kutojivuna hata kumkaribisha Rais Bush, ningekuwa Kikwete nisingehangaika na mtu ambaye kila nikimtembelea huishia kukutana na watu wadogo au hata nikikutana naye huwa ni kwa muda mfupi, tena wa kusimamiwa, kusachiwa na kuharakishwa.

Ningeacha kumkaribisha Bush kutokana na anavyozichukulia nchi zetu kina yakhe. Si siri kuwa rais wa nchi zinazoitwa changa japo si changa anapotembelea Marekani huchukuliwa kama ombaomba yeyote wa kawaida. Ajabu nao watawala wa namna hii kwa kukosa kujithamini na kujiamini hukubali kuchukuliwa hivyo huku nao wakijichukulia hivyo!

Kwa mtu ambaye amesikiliza na kuyaelewa maneno ya Bush kuwa hatatoa misaada kwa wezi, anabaki kuishangaa ithibati ya watawala wetu. Anaposema hatatoa misaada kwa wezi, kwanza ni wezi wapi zaidi ya hao anaowapa hiyo misaada, tena yenye masharti?

Je, hapa si kudanganyana ili dili lipite? Mbona sasa kasaini mkataba wa mabilioni ilhali wanaopewa wanajulikana walivyojiibia hata kwenye Benki Kuu yao? Rejea wizi wa BoT kwenye fuko la EPA ambapo utawala wa Kikwete unazidi kushikwa kigugumizi.

Nigeukie kwa umma wa Watanzania waliodhalilishwa na kudhulumiwa haki zao kama kufungiwa barabara, kubughudhiwa, kuingiliwa mawasiliano yao ya simu, ukiachilia mbali kuletewa majeshi ya kigeni kwa kisingizio cha kulinda usalama wa rais wa Marekani, nao wanaonekana kushabikia jinai hii!

Nilitegemea kusikia waathirika wa kulipuliwa Ubalozi wa Marekani mwaka 1998 wakiandamana kudai fidia stahiki ilipwe tena haraka kwa waathirika.

Nilitegemea kuona waandamanaji wakimshinikiza Bush ambaye anaonekana kama baba wa watawala wetu, awawajibishe kwa kushindwa kushughulikia ufisadi ambao kimsingi ndicho chanzo kikuu cha uhohehahe wetu.

Nilitegemea kuona waandamanaji wanaomshinikiza mgeni huyo wa Rais Kikwete atende haki nchini Iraq, Afghanistan, Palestina na kwingineko ambako Marekani inafanya dhuluma.

Nilitegemea kusikia shinikizo kuhusiana na Marekani kuziunga mkono tawala zandiki kama zile za Rwanda, Uganda hata Kenya. Lakini bahati mbaya haya hayakuwa masuala yenye umuhimu!

Ningekuwa Kikwete ningekaa mbali na Bush kwa kuchelea kurudiwa kilichotokea mwaka 1998, ambapo Balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania zilishambuliwa na wanaodhaniwa kuwa Al-Qaeda kutokana na uswahiba wetu na Marekani.

Sikuona wala kusikia hili kutokana na watu kuona mambo madogo kama makubwa na makubwa kama madogo.

Nani hajui kwamba kuwa karibu na Bush ni kujitangazia vita na Al-Qaeda? Nani hajui kama misaada mingi itolewayo na Marekani huenda kwa taasisi zisizo za kiserikali ili iliwe na watumishi wa Kimarekani wanaosimamia taasisi hizo?

Nani hajui kuwa misaada ya Marekani huambatana na masharti magumu? Nani anaitaka Marekani wakati huu ambapo hata Marekani yenyewe imeanza kuchoka kiasi cha kupigwa kumbo na China?

Anayetaka kujua ninachomaanisha, aangalie jinsi China inavyofanya biashara ya kulipa fedha taslimu wakati Marekani ikifanya mikopo, tena ya masharti magumu. Si hilo tu, Marekani inazinyonya nchi changa kwenye biashara kupitia Shirika la Biashara la Dunia (WTO) kwa sauti kubwa kwenye taasisi za pesa za Kimarekani kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ambazo huvunga kuwa za kidunia wakati siyo?

Je, ni kwa nini Bush ameipendelea Tanzania kipindi hiki? Je, ni kwa sababu ya kugunduliwa madini mengi? Je, ni kwa sababu ya kupitisha madini na silaha kwenda na kutoka DRC, Rwanda na Uganda?

Inatia aibu kiongozi wa taifa linalojiita baba wa kupigania haki za binadamu kuwa shahidi wa uvunjaji wa haki hizo kama kufunga barabara na kuzuia watu kuendelea na shughuli zao.

Nani anataka kero kwa shilingi mbili za ofa? Isitoshe wananchi wa kawaida wa Tanzania hawajawahi kunufaika na misaada zaidi ya kuwa waathirika kwani ni kodi zao zinazotumika kulipia faida kwa madeni hayo, ukiachia mbali watawala wao kuwatumia kuombea.

Ziara ya watawala wa Kimarekani imethibitisha kuwapo udhalilishaji na unyanyasaji hata kwa watawala wetu wenyewe. Rejea wakati wa ziara kama hiyo aliyoifanya Bill Clinton mwaka 2004, ambapo mbwa wa Kimarekani walilinusa hata gari la Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye naye kwa upofu wake alidai: “Ukiona Clinton kaja ujue uchumi unakua.”

Ebo! Uchumi utakuwaje wakati utegemezi na kujikomba ndiyo vinapamba moto huku rushwa na ufisadi vikigeuzwa halali? Kwa nchi yenye rasilimali kama Tanzania, aihitaji ziara ya Bush na mabunda yake ya pesa chafu kuwanyanyasa na kuwadhalilisha Watanzania.

Inafanyika hivi kutokana na utapia mlo wa mawazo na kuendekeza utegemezi. Ukilinganisha hizo dola milioni 700 alizokuja nazo Bush na manyanyaso yake na zile zilizoibwa BoT, Richmond, IPTL, TICTS, NBC, Net Group Solution na uchangudoa mwingine, utaona uhovyo na utaahira wetu vilipo.

Huu nao ni ukoloni mamboleo, ambapo rais mzima aliyechaguliwa na wananchi, anayetambulika kisheria kujidhalilisha kwa sababu wanapokea rais wa taifa kubwa duniani.

Hakika, ningekuwa Kikwete ningepambana na ufisadi vilivyo ili kuokoa fedha nyingi, tena ya stahiki na heshima kuliko kunyenyekea manyanyaso na udhalilishaji kwangu na watu wangu, ukiachilia mbali kuiweka nchi yangu kwenye hatari ya kuvamiwa na magaidi.

Marekani inatumia pesa nyingi kujilinda na ugaidi ilioutengeneza na ambao inafaidika nao. Je, sisi tunazo pesa na zana za kujilinda kutokana na ugaidi? Hakika huku ni sawa na mtu mlevi kushikamana na jambazi ilhali anatafutwa na polisi ili wakiwanasa wawasulubu pamoja. Hebu angalia ni kwanini napinga ziara ya Bush nchini Tanzania. Soma nukuu yake.

“Lengo la kusaini mkataba huu ni kuhakikisha nasaidia zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria na ukimwi pamoja na kuwemo maeneo mengine yanayohitaji msaada.

Hata hivyo si kwamba mkataba niliosaini utaishia hapa, bali nitahakikisha natoa msaada, ikiwezekana mara mbili ya huu, nia ni kuona magonjwa Tanzania na Afrika yanakwisha ndani ya kipindi cha miaka mitano,” alisema Rais Bush.

Ujinga mtupu! Nani anaweza kuondoa magonjwa Tanzania na Afrika ndani ya miaka mitano? Ondoeni umaskini na ufisadi kwanza, mengine yatajiondokea yenyewe.

Kwa mtu anayejua matatizo ya Tanzania vizuri, kipaumbele kisingekuwa ukimwi ambao ni tatizo la mtu binafsi likilinganishwa na kutokuwapo uwiano wa kibiashara kimataifa, kupambana na ufisadi na kukuza kilimo na mawasiliano.

Hapa kilichofanyika ni kuelekeza pesa kwenye shughuli ya ovyo na kuacha za muhimu kama kukuza uchumi na kupambana na ufisadi na kusimika utawala bora, ambavyo kimsingi ndivyo vikwazo vya maendeleo ya nchi.

Mpumbavu alipewa msaada wa suti kali huku watoto wake wakikosa chakula na pesa ya shule akashangilia! Au ni ujuha ule ule wa kuuza ng’ombe kugharimia kesi ya kuku?

Naomba kutoa hoja.



Source: Tanzania Daima Februari 20, 2008.

No comments: